Mimi,Petro Eusebius Mselewa,Msomi wa Sheria,mtanzania mtu mzima mkazi wa Kibaha,Pwani NATAHADHARISHA Wajumbe wote (pamoja na viongozi wao) wa Bunge Maalum la Katiba kwa kusema ifuatavyo:
1. Kwamba, nikiwa ni mfanyakazi wa Serikali ninayekatwa kodi kila mwezi kuchangia maendeleo ya nchi yangu yakiwemo ya kupata Katiba mpya.
2. Kwamba, malipo ya posho na marupurupu mengine wanayopewa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba nayachangia kupitia makato hayo na mengine kupitia kununua bidhaa zenye kodi ya ongezeko la thamani.
3. Kwamba, Wajumbe wa Bunge Maalum wako Dodoma kama wawakilishi wa watanzania wote na si vyama vyao vya kisiasa au taasisi watokazo.
4. Kwamba, Bunge Maalum la Katiba limekuwa na mweneno usiovutia hasa kubishania vitu visivyo vya msingi,kupiga kelele Bungeni, kukejeliana na kutusiana.
5. Kwamba, siku zilizopangwa kwa suala la kujadili na kuipisha Rasimu ya Katiba mpya,kwa mwenendo ulivyo sasa Bungeni, hazionekani kuwa zitatosha.
6. Kwamba, mifarakano inayoendelea na kushamiri kila uchao ni dalili mbaya za kupata Katiba mpya inayokidhi matakwa na matarajio ya watanzania.
HIVYOBASI, Wajumbe wote wa Bunge Maalum nawatahadharisha na kuwaambia kwamba:
1. Mfanye mambo yaliyowapeleka hapo Dodoma kadiri ya majukumu yenu na maslahi mapana ya Taifa.
2. Watanzania hawashindwi kuwaondoa hapo Dodoma kwa kusitisha au kuondoa kabisa mchakato huu
3. Watanzania bado wana imani nanyi ingawa uvumilivu wao unakaribia mwisho
4. Mchukue hatua stahiki kuepusha mifarakano ya kitaifa inayoweza kuzaliwa na matendo na maneno yenu hapo Bungeni Dodoma.