Ndugu zangu,
Watanzania leo tunavuta pumzi huku tukielekeza
macho na masikio yetu katikati kabisa ya nchi
yetu tuliyozaliwa na tunayoipenda. Ni Dodoma.
Huko itapatikana leo hatma ya mwelekeo wa
mchakato wa kupatikana kwa Katiba Mpya ya
Nchi Yetu.
Hata hivyo, kuna ishara mbaya kuwa
tuliowatuma Dodoma wako katika hatari ya
kukwamisha mchakato mzima kwa kujikita
kwenye kupigania kisicho na maslahi ya nchi hii
kwa miaka 50 au 100 ijayo.
Watapigania yaliyomo kwenye vifungu vya 36
mpaka 37 za Kanuni za kuendesha Bunge hilo
Maalum. Inahusu namna watakavyofikia
maamuzi, kuwa iwe ni kwa kura za faragha au
dhahiri. Ndio, inahusu kura za siri au kura za
wazi. Ni' vifungu vya kifo' maana ndivyo
vitakavyoamua, kwa namna moja au nyingine,
uhai wa mchakato mzima wa kuitafuta Katiba.
Tuliowatuma Dodoma wamejigawa katika
makundi ya ' Sisi' na ' Wao'. Wanatafuta
kushindana na kupata mshindi badala ya kutafuta
muafaka wa Kitaifa. Na hakika, kama alivyopata
kusema Rais wa Nchi, Jakaya Kikwete, kuwa
kwenye kushindana huko hakuna atakayeshinda.
Tutashindwa Sote. Na huo ndio UKWELI.
Hakika, huu ni mtihani mgumu ulio mbele yao
tuliowatuma Dodoma. Wakishindwa mtihani huu,
basi, ishara zinazoonekana ni za mkwamo wa
jumla wa mchakato mzima. NI AIBU.
Tuliowatuma Dodoma hawajachelewa kuitafuta
hekima na busara kutunusuru na aibu kubwa ya
taifa iliyo mbele yetu. Tuliowatuma Dodoma
wawafikirie pia watoto wa kesho na wa vizazi
vijavyo katika nchi yetu tuliyozaliwa na
tunayoipenda.
Na ushauri hapa ni heri kukubaliana
kutokubaliana, na hivyo, kusitisha kwa muda
mchakato huo, kuliko kulazimisha kwenda
mbele. Ni ushauri pia, kuwa ni heri kuyatafuta
maridhiano kwanza kabla ya kuingia kwenye
majadiliano, kuliko kuyatafuta maridhiano baada
ya kuingia kwenye mapigano na kujeruhiana. Ni
busara basi, tuliowatuma Dodoma wakaunda
Kamati Maalum ya kuyatafuta maridhiano wa
vifungu hivyo. Na ifahamike, kuwa MARIDHIANO
ndio msingi wa UHALALI wa mchakato na hata
Katiba yenyewe.
Tusipotanguliza busara, hekima na maslahi ya
taifa, yumkini yaweza ikawa kama yale aliyopata
kuyasema miaka 60 iliyopita, mwandishi yule
mahiri, Mtanzania mwenzetu Shaaban Robert,
aliandika; Wasadikika wana desturi ya kutafuta
fimbo baada ya kuumwa na nyoka. Tumekwisha
umwa na nyoka wa matendo yetu mabaya ya
zamani.
Nyoka mwenyewe amekwishakimbia. Hapatikani
kwa kujilipiza kisasi, lakini, sumu yake imebakia
katika jeraha tulilolipata. Sasa, shauri lililo jema
ni kuzuia sumu hii isienee miilini mwetu ikaleta
kifo.
Maovu yana hatari kubwa kukaa kati yetu.
Tumedumu nayo kwa muda mrefu. Hayakutuletea
faida ila hasara, huzuni na kilio siku zote.-
Shaaban Bin Robert.