Maneno matupu hayavunji mfupa. Vitendo ambavyo vimetokea baada ya Mwl. Nyerere kung'atuka na baadae kufariki vinaonyesha ni jinsi gani serikali za ccm zilizofuatia zilivyowavunjia heshima waasisi wetu.
Mwl. Nyerere ameonyesha kusikitishwa kwake kwa viongozi wa ccm katika kitabu chake Our Leadership and the Destiny of Tanzania (1995) p.14-15 kwa jinsi walivyoua Azimio la Arusha na kuondoa miiko ya uongozi.
Tunachokiona sasa ni muendelezo wa kutaka hali hiyo ya kuasi maadili ya waasisi iendelee. Ni wakati huo baada ya Mwalimu tumeona ni jinsi gani Mtanzania wa kawaida alivyozidi kuwa masikini, huduma za jamii kupungua au kuisha kabisa na usalama wa raia kuwa tete. Sambamba na hilo, tumeona ni jinsi gani rushwa, dhuluma, wizi, upendeleo, usultani, ukosefu wa maadili, uuzaji wa madawa ya kulevya, ujangili (nikitaja vichache tu), vilivyo endelea na kufanywa na hao hao viongozi wa ccm.
Ikumbukwe kwamba Mwl. Nyerere alishatamka kuwa alishafanya makosa, na kama Watanzania wako tayari kuyarekebisha, wanaweza kuyafanya marekebisho bila pingamizi lolote. Huwezi kufanya marekebisho yeyote bila kutambua ni wapi kuna hitilafu na kuitamka wazi. Hivyo basi, kutambua makosa yaliyopita ili kurekebisha hali kuwa nzuri si kukosa heshima.
Hata hivyo, kufumbia macho makosa ambayo yataleta madhara makubwa, kwa ajili tu ya faida ya watu wachache binafsi ni ukosefu wa heshima na unafiki mkubwa.