Mwakalebela: Yanga Itacheza Mechi Tarehe 15 — Sheria Iko Juu ya Kila Kitu
Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Fredrick Mwakalebela, ameibuka na kutoa kauli nzito kuhusu sakata la mchezo wa marudiano kati ya Yanga na Simba uliopangwa kuchezwa Juni 15, 2025.
Akizungumza, Mwakalebela amesema anaamini kwa asilimia mia moja kwamba Yanga itashuka dimbani kucheza mechi hiyo kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
“Mimi naamini Yanga itacheza mechi tarehe 15. Kwa sasa hakuna tena mjadala, kwani shauri lilishakwenda hadi Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), na uamuzi wake ulikuwa wazi – mamlaka ya kupanga ratiba na kushughulikia masuala ya mpira ni ya shirikisho, si ya klabu,” alisema Mwakalebela.
Mwakalebela ameongeza kuwa klabu yoyote, hata iwe kubwa kiasi gani, haina mamlaka ya kupinga ratiba iliyoandaliwa na chombo rasmi cha kusimamia soka nchini. Ametahadharisha kuwa kutoshiriki mechi hiyo kutakuwa ni kuvunja sheria za mashindano, jambo ambalo linaweza kuisababishia Yanga adhabu kali.
“Sheria zipo na lazima ziheshimiwe. TFF walipewa mamlaka yote na CAS. Sasa kama timu haijitokezi, sheria itafuata mkondo wake – iwe ni faini, kufungiwa au hatua nyingine. Hilo halihitaji mjadala,” aliongeza.
Kauli ya Mwakalebela imekuja wakati kukiwa na sintofahamu miongoni mwa baadhi ya mashabiki na viongozi wa Yanga kuhusu uhalali wa tarehe ya mchezo huo. Hata hivyo, uamuzi wa CAS kutupilia mbali rufaa ya Yanga dhidi ya ratiba ya TFF umeweka bayana kuwa mchezo huo upo halali na unatakiwa kuchezwa kama ulivyopangwa.
Credit @crownsports__tz