Zaidi ya Shilingi Milioni 15 za madeni ya maji zimelipwa na wadaiwa zaidi ya 280 katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, hiyo ni kutokana na ofa ya Rais Samia Suluhu kwa wateja wote ambao wanaodaiwa na kumesitishiwa huduma ya maji na Mamlaka za Maji nchini.
Ofa hiyo imelenga kuhakikisha kuwa wateja waliositishiwa huduma ya maji wanarejeshewa bila faini, pamoja na kukaa na Mamlaka hizo kujadili namna ya malipo ya madeni yao kulipwa kidogo kidogo kadri ya makubaliano yao.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA), Baby Lucas Biko amesema tangu ofa hiyo ilipotangazwa kuanzia tarehe 8 hadi 31 mwezi Mei, jumla ya wateja 287 wamelipa madeni yao ambayo ni zaidi ya Sh milioni 15 na tayari wamerejeshewa huduma, huku jumla ya madeni yote ambayo Mamlaka ilikuwa inadai ni zaidi ya Milioni 22.
Amesema wateja wanaendelea kulipia madeni kidogokidogo kulingana na makubaliano waliojiwekea na Mamlaka hiyo, huku akiwataka kumalizia madeni yaliyobakia ili kufurahia huduma ya maji safi, na kwamba wako tayari kuendelea kushirikiana nao kwani ofa kama hizo hutolewa mara kwa mara.
Mkurugenzi amezitaja faida za kulipia ankara za maji kwa hiari na kwa wakati kuwa ni pamoja na kusaidia kuepuka malimbikizo ya bili, ambayo husababisha kusitishiwa huduma ya maji na kulazimika kulipia faini endapo mteja atahitaji kurejeshewa huduma, jambo ambalo huleta usumbufu zaidi.
Kwa wale ambao wamepitwa na ofa hiyo, amesema SOUWASA ipo tayari kuendelea kujadiliana na wateja kuona namna ya kuwasaidia ili waweze kurejeshewa huduma ya maji, kwani ofa kama hizo hutokea, hivyo wakisikia wanatakiwa wachangamkie fursa hizo.
Kabla ya ofa hiyo, zaidi ya wateja 2,400 walikuwa wamesitishiwa huduma ya maji, ambapo baadhi yao wamefanikiwa kulipia na wengine wanaendelea kadri ya makubaliano maalum na Mamlaka hiyo.