Kutoka kitabu, kwaheri ukoloni kwaheri uhuru
Mzee Faraji
Nilipata kusikia kutoka kwa mmoja wa Marais wa zamani wa Zanzibar, kuwa manunguniko na madai ya Wazanzibari yaliyoanza katika miaka ya 70; kuhusu kuvunjwa mkataba wa 1964, kwa manufaa ya Tanganyika; madai hayo yalikuwa yakiwaudhi sana viongozi wa Tanganyika.
Hivyo siku moja Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, akamwambia Raisi wa Muungano (wakati huo) Mwalimu Nyerere, kwamba kwanini hawavunji mbali muungano ili wapumzike na “kelele” za Wazanzibari? Inasemekana Mwalimu Nyerere alimjibu kwa kumkatalia kwa kusema mengi pamoja na “…tukiwaachia tu, utaona jinsi mapesa ya Waislamu na Waarabu yatakavyo miminika Zanzibar…hapana, hatuwaachii.”
Laiti shida ya Mwalimu Nyerere ingelikuwa nae anazitaka pesa hizo kwa ajili ya Tanganyika, kisa kifuatacho kisingelitokea. Kwa mujibu wa kisa hiki kama kilivyosimuliwa na Rais huyo wa zamani [wa Zanzibar], Mwalimu Nyerere, wakati huo akiwa ameshastaafu, alipita akiwa safarini, katika uwanja wa ndege Jeddah, Saudi Arabia. Balozi wa Tanzania aliyekuwepo Saudi Arabia ilimlazimu ki-protokoli, kwenda uwanja wa ndege kuzungumza nae katika muda wa transit.
Pamoja na mambo mengine, Balozi huyo alimwambia Mwalimu Nyerere “…katika nchi hizi kuna mapesa mengi, na jamaa yaelekea wapo tayari kutusaidia mipango yetu mingi ya maendeleo, ilimradi tu, tuwaombe.” Nasikia Mwalimu alimjibu kwa mkato na kwa kiasi cha kuonekana kakasirishwa: “Hapana. Acha kabisa!”1
Ni dhahiri, mpishi wa mapinduzi na muungano, Mwalimu Nyerere, alikuwa ameacha “grand design” [mpango mkubwa] katika kuipata Zanzibar, bila shaka si kwa manufaa ya nchi (Tanganyika na Zanzibar), bali kwa manufaa ya wale wasiowatakia mema Waislam (pamoja na Waarabu ambao wengi wao ni Waislam).
Niliwahi kumuuliza mmoja wa Maraisi waliopita wa Zanzibar kama aliwahi kuuona waraka asilia [wa Muungano baina ya Zanzibar na Tanganyika] uliotiwa saini tarehe 26 April 1964, akaniambia hapana, hajawahi kuuona. Nikamuuliza tena, je, yule uliyemuachia nafasi yako unaweza kumuuliza kama kawahi kuuona? Akanijibu: “hapana haja ya kumuuliza, kwa sababu nafahamu kuwa nae pia hajauona.”
Kwa kawaida nchi inapotaka kujiunga na Umoja wa Mataifa (UN), hutowa taarifa ya mwezi mmoja na kisha kuwasilisha maelezo/vielelezo na vithibitisho kuwa ni nchi (yenye sifa ya kuwa na Utaifa), inayostahili heshma ya uwanachama huo. Nchi zilizokuwa zinapata uhuru wake toka ukoloni zilitoa taarifa ambayo tarehe yake ya mwisho ilisadifia na tarehe ya kupandisha bendera mpya.
Hivyo nchi iliyojisajili UN na kupewa kiti, bila shaka ilipobadili nafasi iliyoiondosha uwananchi wake, haikuondoka katika umoja huo bila ya taarifa yoyote. Bila shaka patakuwepo maelezo na vielelezo vilivyokubalika kiti chake kurudishwa, bendera yake kushushwa katika mlingoti wa UN, na majukumu yake kame vile michango n.k., kufutwa.
Vipi leo nchi kama hiyo isiwe na hati halisi ya makubaliano ya muungano ambayo wananchi waliona Sheikh Karume na Mwalimu Nyerere wakisaini na kupeana April 26, 1964? Na vipi nchi isiwe hata na zile nakala halisi za vielelezo japo vile vilivyopelekwa UN kuhusu suala zito la utaifa wake? Au hata ushahidi wa kisheria kuwa hakuna nchi inayoitwa “Tanganyika” au yakuwapi maelezo/vielelezo kuhusu kuongezeka kwa mambo ya muungano na nani alotia saini kwa niaba ya Zanzibar? Ni saini yake au ni ya nani na kwa ushahidi gani wa kisheria?
Wenye kuumizwa na yote hayo khasa ni Wazanzibari na si Watanganyika. Mapinduzi ndo yalioipinduwa nusu ya jamii ya Zanzibar ilioshinda uchaguzi [wa Julai 1963]. Mapinduzi ndo yaloleta muungano na kuyapinduwa makubaliano ya mwanzo ya muungano. Mapinduzi ndo yaliokifuta kiti cha Zanzibar UN kwa nia ambazo Wazanzibari bado hawajazitambuwa.
Mapinduzi ndio yaliomuondowa Al Hajj Aboud Jumbe madarakani, na kilichomponza khasa Mzee Jumbe ni pale alipolianzisha Baraza la Misikiti Tanzania (BAMITA); yakamtia ndani Maalim Seif Sharif Hamad; na ndiyo yaliyopelekea Dk. Salmin Amour akataliwe kuiingiza Zanzibar/Tanzania katika OIC na kuiakhirishia Zanzibar kutojiunga na taasisi hiyo. Ndiyo yaliyoifanya Katiba ya nchi itamke kuwa Raisi wa Zanzibar siyo tena Makamo wa Kwanza wa Rais wa muungano, kama ilivotamkwa 1964. Na ndiyo yaliyo “thibitisha” kuwa nchi ya Zanzibar sasa ni Mkoa kama mkoa wowote Tanzania. Na kubwa zaidi, hayo ndiyo yaliyofanywa kuwaonesha rasmi Wazanzibari kuwa hata ndani ya chama kilichoundwa kwa kuunganisha ASP na TANU, TANU, CCM Bara, ndiyo itakayoamua nani atagombea Uraisi Zanzibar.
Hivi sasa hakuna udhibiti kwa watu kutoka bara kuingia na kuishi Zanzibar. Lengo ni kubadilisha “demographic situation in favor” [hali ya wingi wa watu] ya bara katika miaka michache ijayo. Na hiyo population [idadi ya watu] mpya inaandaliwa kuwa “superior” katika uchumi, ilimu na ushawishi wa kisiasa. Wapemba kuunga mkono chama kinachoongozwa na Maalim Seif Sharifu, Mpemba, university graduate [mhitimu wa Chuo Kikuu] na mzoefu katika serikali na siasa; mtu ambae alikhitalifiana na Mwalimu Nyerere inakaa vizuri katika “grand design” [mkakati mkubwa] ya Mwalimu ya kuwatenga Waunguja. Nyerere alipoenda Zanzibar kueleza kwa nini CCM iliwafukuza Seif na wenzake, alimtaja Seif kama watu “…tuliokuwa tukiwapokea katika chama pasipo kuwachunguza kwa undani ili kujua asili yao na huko watokako…” Mbali ya maneno hayo, Nyerere pia alianzisha propaganda za kwamba watu wenye rangi ya kuchovya kama ya Seif, japo si Waarabu, alitaka watazamwe kama Waarabu. Siasa zao zitakuwa za kutaka kumrudisha Mwarabu Zanzibar.
Nyerere pia alianzisha lugha ya kampeni ya “kuwanasihi” watu wa bara (Tanganyika), kama moja ya propaganda zake za kujenga hoja ya kujitetea pale itakapoonekana kuwa bara inatumia nguvu kulazimisha muungano. Ikawa akisema mara kwa mara kuwa “…hawa wanataka kuuvunja muungano, mkiwaachia, watauana ovyo…sasa wameshaanza kugawanyika na kubaguana, kati ya Wazanzibari na Wazanzibara…Wapemba na Waunguja…” Ingawa hoja hiyo inakusudiwa kuwaomba Watanganyika “kuwanusuru” Wazanzibari ili wasi-jeuana, haikumpitikia Mwalimu wala wengineo kuhoji; kama Wazanzibari wamegawika kiasi hicho, msimamo wa uhalali wa muungano ukoje hivi sasa? Tanganyika hivi sasa imeungana na nani; Wapemba, Waunguja, Wazanzibari au Wazanzibara? Siri ya mapinduzi ya wazee inatowa jawabu lililo safi; Tanganyika iliungana na Waafrika kutoka bara kuwapinduwa Wapemba na Waunguja—Wazanzibari.
Katika mambo ya kudhulumiana nchi, wajanja hufanya kila njia kuepuka masuala ya mfumo. Watakupelekeni kwenye utendaji kazi. Huko mtazungumza na wale waliopewa kazi ya ku “run” government [kuendesha serikali]. Hamtokutana tena na wale wanao “rule” [wanaotawala]. Sioni sahihi kuutegemea Muwafaka badala ya Mkataba wa Muungano na Katiba na sheria za nchi, kutupa muelekeo wa kule tunakostahili kwenda. Hivyo hivyo, siamini kuwa mtu atayewekwa na madhalim katika madaraka ya nchi, ana uwezo wa kujua na kuipeleka nchi hiyo pahali pasipokuwa pale panapo takiwa na madhalim hao.
Kwa vyoyote vile, endapo tutatanabahi, tukatambua kuwa nguvu za wananchi ni muhimu kuliko chochote, na kwamba nguvu hizo hazipatikani ila kwa kuwatoa katika umasikini wa kiza cha ujinga wa ilimu duni; tunakoelekea si kubaya. Kuwatowa wananchi kunako giza la tunakotoka na Zanzibar kujiwakilisha nchi za nje, kuujenga na kuulinda uchumi wake, pamoja na kulindwa na Wazanzibari, ni kuzuri, na huko ndiko kwa kuanzia.