Abdallahking
JF-Expert Member
- Mar 19, 2018
- 3,985
- 10,840
Simulizi : ZAWADI YA USHINDI
Mwandishi : BEN R. MTOBWA
Imeletwa kwenu na: BURE SERIES
Sehemu ya 1
SHANGWE na vigelegele ambavyo viliutoka umati huu mkubwa vilipaa hewani na kujaza anga lote. Sauti za kila aina zilitamkwa kwa kila rangi kiasi
kwamba zilitoa kelele, si kelele za shangwe tena bali mngurumo ambao uliitetemesha ardhi. Naam, ilikuwa siku ya furaha, siku ambayo haitasahaulika, siku ambayo wazee waliusahau uzee wao na kujitoma uwanjani kifua mbele, wakikoroma mikoromo ambayo ilizaa ngurumo ya furaha, siku ambayo vijana waliikumbuka afya yao na kuihadharisha uwanjani kwa kurukaruka huku na huko huku, midomo yao ikiimba nyimbo za ushindi, siku ambayo hata watoto waliukana utoto wao na kujikuta katikati ya wazazi wao wakipiga vigelegele na kucheka.
Naam, siku ya siku! Nani ambaye asingefurahi leo? Siku ambayo mashujaa walikuwa wakirejea
toka katika ile safari yao ndefu ya kumwangamiza nduli, fashisti, dikteta Iddi Amini ambaye alikuwa ameivamia nchi na kuyahatarisha maisha ya mamia ya wananchi wasio na hatia.
Ngoma ziliendela kupigwa ingawa mlio wake ulitawaliwa na vifijo na vigelegele hata visisikike kabisa. Wachezaji waliendelea kucheza na kuimba ingawa macho ya wachezaji yalikuwa juu, kila mmoja akiwatazama wanajeshi ambao walikuwa wakiteremka toka katika magari yao yaliyokuwa yakiendelea kuwasili. Wanajeshi hao walipowasili walijiunga na wenzao katika magoma na vigelegele.
Kila mara mtu mmoja au wawili walionekana wakiiacha ngoma ghafla na kumkimbilia mwanajeshi ambaye ndio kwanza anateremka toka garini. Walimkumbatia na kuviringishana kwa furaha huku machozi ya faraja yakiwaponyoka na kuteleza mashavuni. Pengine alitokea mzee akajikongoja kumkimbilia mtu, alipomfikia alisita ghafla moyoni akinong’ona “siye.”
Hali hiyo iliendelea kwa muda mrefu, lakini hatimaye ngoma zikatelekezwa na nyimbo kusahauliwa, kila mmoja akawa ama kamkumbatia huyu au kaduwaa akimtazama yule.
Waliolia kwa furaha walilia, waliocheka kwa faraja, walicheka. Baadhi walitulia wakitetemeka kwa hofu, mioyo yao ikiwa na imani yenye shaka: Atafika kweli? Atarudi salama? Mungu atajua…
***
Huyu aliteremka polepole, mzigo wake ukining’inia mgongoni. Kama wengine wote alikuwa amevaa mavazi rasmi ya kijeshi, mavazi ambayo yalimfanya aonekane si kama kichaka kinachotisha tu bali kadhalika kama chui anayeranda baada ya kuliangamiza windo lake. Alikuwa akitabasamu. Au tuseme alifahamu mwenyewe kuwa anatabasamu kwani haikuwa rahisi kwa mtu baki kufahamu. Hakuwa mgeni katika mji huu wa Dodoma. Ingawa si mzaliwa wa hapa lakini miaka minne aliyoishi hapa kama haikufaulu kumweka katika orodha ya wenyeji basi ilimfuta katika ile ya wageni. Hivyo, hakuwa na shaka ya kupokewa na watu aliowafahamu. Akatazama huko na huko kwa shahuku. Naam, haukupita muda kabla hajamwona mtu anayemfahamu. Mzee philipo Matayo, mfanyakazi mwenzake, alikuwa akimjia. Akajiandaa kumpokea kwa kuongeza ukubwa wa lile tabasamu lake huku akipanua mikono amkumbatie. Lakini ah! Mzee alimpita bila dalili yoyote ya kumfahamu. Alijaribu kumwita lakini sauti haikufua dafu miongoni mwa kelele nyingi zilizokuwepo. Pengine hakumwona! Aliwaza.