34.
kuhisi uso wake mchangamfu ukimtazama kwa tabasamu. Hayo, kama hirizi ya usalama wake ama taji la ushujaa wake, yakamfanya aanze kumfuata adui huyo kwa moyo wenye ari na matumaini.
Hakukubali kumpoteza. Wala hakuwa tayari adui huyo afahamu kuwa anafuatwa. Alimnyemelea, akajitahidi kadiri ya uwezo wake kuepuka kukanyaga vijiti, visiki na kutumbukia katika korongo. Akaushukuru ujuzi na mazoea yake ya kutembea porini. Zaidi ya yote alilishukuru giza. Zamani alipokuwa mdogo alilichukia na kuliogopa, sasa alilitegemea na kuliona rafiki mkuwa.
Baada ya mwendo wa kutosha waliwasili katika kambi yao. Ingawa giza halikumruhusu kuona lakini kadri alivyozoea, hakushindwa kugundua vibanda vyao vilivyojengwa huku na huko. Kisha, aliweza kuona vichwa vya watu waliokuwa wamesimama hatua kadhaa mbele yake. Walikuwa wakizungumza kwa kunong’ona, asingeweza kusogea tena pasi ya kuonekana. Hivyo, alijifutika katika kichaka huku akimtazama kiongozi wao ambaye aliingia katika kundi hilo. Alihisi wakimlaki kwa shangwe. Akawasikia wakinong’onezana maneno kadhaa. Alihuzunika kwa kule kuwa mbali kiasi cha kutoweza kusikia walichokuwa wakizungumza. Kitu kimoja alikuwa na hakika nacho, kwamba maongezi yao yote yalikusudia kuwaangamiza wao. Laiti angeisikia mipango yao! Akasaga meno kwa uchungu.
Halafu alifahamu kinachotokea. Hujuma hiyo ilikuwa ikipangwa kufanyika muda huohuo! Aliyagundua hayo baada ya kuona vikosi vikitayarishwa na kupangwa tayari. Asingeruhusu hilo litokee, kuacha kikosi chao, ama kijiji chao, kivamiwe ghafla. Ni hilo alilofuata kulikomesha. Hivyo, bila ya kufikiri kwa mara ya pili aliinua bunduki yake na kupiga risasi juu kwa namna ya kuwatahadharisha askari wenzake waliobaki kambini. Mlipuko wa bunduki yake uliwafanya adui wote waduwae na kubaki kimya kwa muda. Lakini mlipuko huohuo uliyafichua maficho yake. Hivyo, wakati adui hao wameduwaa yeye aliinuka na kuanza kukimbia. Hakupiga hatua tatu kabla ya adui mmoja hajafahamu kilichokuwa kikitokea na kuanza kumfuata mbio. Alikuwa adui mwenye mbio nyingi, labda kwa ajili ya kuwa mwenyeji katika msitu huo, kila hatua yake moja alizidi kumkaribia Sikamona. Ndipo Sikamona alipoona kukimbia kusingemfikisha popote. Akasimama na kumgeukia. Adui alipomkaribia , alimpiga risasi na kuanza kukimbia. Lakini sasa alikuwa akifuatwa na kundi zima. Alijua asingefika mbali. Hivyo, aligeuka kuwakabili, hakuwa na muda wa kulala chini. Hakuwa na nafasi ya kufanya hivyo. Wima, kama kisiki, akaiwasha bunduki yake na kuwamiminia adui risasi bila hata ya kulenga shabaha. Wengi walianguka na kufa, wengi wakageuka na kukimbia, lakini ni wengi pia ambao walizidi kumjia kwa uchu kama kundi la mbwa mwitu lililomfumania mwanakondoo. Hatimaye, risasi zikamwishia. Alifahamu
kukimbia kusingemsaidia. Hivyo, alijitosa katika genge la maadui na kuanza kuwapiga kwa sime. Haikumchukua muda kabla hajajikuta angani akipigwa kwa kitako cha bunduki hii na kudakwa kwa singe ile.
Maumivu aliyoyasikia hayakuwa na kifani. Hata hivyo, aliyasikia kwa muda mfupi tu kwani dakika chache baadaye, badala ya kuelekea hewani, alijisikia akididimia polepole katika shimo refu lenye kiza kinene.
alipozinduka alijikuta kalala juu ya kitanda katika chumba chenye harufu tofauti na ile aliyoizoea, harufu ya mchanganyiko wa madawa. Uso wake
mzima ulikuwa umefunikwa na bandeji nzito ambazo zilimzingira hadi mikononi na kifuani. Alipojaribu kujigeuza alalie ubavu alipambana na maumivu makali, maumivu ambayo yalimfanya akikumbuke kile kipigo alichokipata toka kwa adui. “Niko wapi?” aliuliza.
“Kampala. Hospitali,” sauti ilimjibu.
Alipogeuka kuangalia macho yake yaligongana na yale ya Brigedia wake, Chunga. Akagutuka kidogo kwani hakutegemea. Akajaribu kuinua mkono ampigie saluti lakini hakufanikiwa.
“Usisumbuke Sikamona,” Brigedia alimjibu akitabasamu. “Unahitaji kupumzika kwa muda,”
akasita. Kisha, alianza tena, “Umekuwa hapa hospitali bila fahamu kwa siku tatu. Kwa kweli, tulianza kukata tamaa. Sasa hatuna shaka kuwa utapona.” Akasita tena. Kisha akaendelea, “Kitendo chako kamwe hakitasahaulika. Licha ya kuokoa maisha yetu ilituwezesha kuwaangamiza adui ambao walikuwa wakitusumbua sana. Hata hivyo, bado hatujafahamu uliwezaje kufahamu kambi ziliko na kwa nini ulianza kupambana nao peke yako.”
Sikamona angependa kueleza yote, tangu alivyomwona adui, alivyomfuata na hata alipofyatua bunduki ya kuwataadharisha. Hata hivyo, kwa ajili ya maumivu makali aliishia kuongea machache tu. Brigedia alisikiliza kila kitu kwa furaha, huku kasahau tabasamu usoni kwake. Baada ya kusikia yote alitikisa kichwa na kusema. “Ushujaa wako hautasahauliwa. Laiti kila kijana wa kitanzania angekuwa na roho yenye uamuzi na nia kama yako! Nasikitika tulichelewa kidogo kufika hapo ambapo ulikuwa umewadhibiti adui. Hata hivyo, tulifanikiwa kuwateka wote wale ambao walikuwa wamekuzingira na kukukanyagakanyaga kama vifaru wenye vichaa. Nadhani watajuta milele kwa ujinga wao wa kusahau yote waliyostahili kuyakumbuka na badala yake kukuvamia wewe.
Sikamona hakuyasikia yote. Uchungu mkali ulimrudia tena. Vitu kama nyundo vilimpiga kichwani. Ghafla akajiona akididimia tena katika lile shimo refu lenye kiza cha kutisha.
***
Sasa alikuwa hajambo kiasi. Aliweza kukiacha kitanda chake na kujikongoja hatua chache nje ya jengo la hospitali. Aliweza hata kula mwenyewe, ingawa alipata matatizo katika kulenga mdomoni na kutafuna. Alidhani hayo yalisababishwa na plasta zilizomzingira usoni, hivyo yangetoweka mara tu zitakapoondolewa.
Askari wengi walimjia kumpa pole na hongera, wengi sana, wadogo kwa wakubwa, rafiki kwa watu baki. Wote walikifurahia kitendo chake na kumwomba awasimulie tena na tena alivyofaulu peke yake kuwakabili maadui wengi kiasi kile. Lakini Sikamona hakuwa tayari kufanya hivyo. Asingekubali kurejea tena katika ndoto hiyo ya kutisha. Badala yake alikuwa akijiuliza vipi alinusurika katika mapambano chungu nzima, makali mno na kuja kuhatarika katika pambano dogo la mwisho kama hili. Miongoni mwa mapambano hayo ambayo kamwe yasingetoweka katika fikra za Amini na vikaragosi wake ni pamoja na kile kipigo cha Kagera. “Kumtoa Nyoka Nyumbani,” kile cha Lukaya “Asiye Sikia la Mkuu,” kile cha Entebbe “Joka Limekamatwa Kiwiliwili” na kile cha Kampala “Kupondaponda Kichwa cha Joka” yote hayo alishiriki kikamilifu na kuokoka isipokuwa hili. Hata hivyo, huku pia si kupona? Alijikumbusha. Kwani kupona ni nini? Haja si kuweka jina katika historia? Yeye ameongeza uzito wa jina lake katika kurasa za historia!
***
Halafu akawa amepona. Bandeji zikaondolewa na akaruhusiwa kuondoka. Akajisikia furaha kuvaa tena magwanda yake badala ya kanzu za hospitali. Akainua mkono wake ili auguse uso wake ambao alikuwa hajaugusa kwa muda mrefu. Alichokigusa kilimtisha. Alihisi kushika kitu zaidi ya uso wake, kitu baki kabisa, kitu kikavu na kinachokwangua kama kisiki. Ni kitu gani? Akagutuka. Hofu ilimshauri kutoka nje upesi. Huko pia alikutana na mwujiza. Watu wote aliofahamiana nao si walimtazama kwa hofu na mshangao tu, bali pamoja na dalili zote za kutomjua. Akaduwaa kwa muda, kisha alirejea ndani upesiupesi. “Kioo” alifoka akiangaza huku na huko. Ndipo alipokumbuka kioo kilichokuwa bafuni. Hima, akaelekea huko. Alipofika akasimama mbele ya kioo kujitazama. Mbele yake alimwona mwanajeshi mwingine kasimama akimtazama. Kilichomshangaza ni uso wa mtu huyo. Hakujua kama ulistahili kuitwa uso au vipi. Ulikuwa kama kinyago ambacho kilichongwa kwa makosa, kinyago chenye kovu zito na jeusi nusu ya uso mzima, jicho moja, hali la pili limetoweka na nafasi yake kuchukuliwa na kovu hilo, pua lilipondwa na nusu iliyosalia kuinamia upande, mdomo wa juu ukiwa umeng’oka, hali wa chini umerudishiwa kwa kushonwa na shavu ambalo lilisinyaa na kukauka kabisa. Kwa mshangao, Sikamona aliinua mkono kukuna kichwa. Akashangaa zaidi alipoona mtu huyo akifanya vivyohivyo. Kisha akaelewa. Alikuwa akijitazama mwenyewe katika kioo. Mtu wa kutisha alikuwa
yeye!
Ndipo alipoangua kicheko na kuondoka.
Alipofika kambini kwake, Gulu, alilakiwa na nyuso zilezile za mshangao. Hakujali. Alicheka na kuingia hemani ambamo alipata silaha na kutoka tena haraka. Aliifuata njia ileile ambayo alimnyemelea yule adui. Akafuata uchochoro uleule. Hatimaye, akawasili katika msitu wenyewe. Aliufahamu kwa kuona miti ilivyoumia kwa ukali wa risasi. Ni hapo ambapo aliupoteza uso wake. Ni hapo pia ambapo alikusudia kuupoteza uhai wake. Vinginevyo angewezaje kuishi katika hali hii? Angewezaje kustahimili mishangao ya watu? Angewezaje kutazamana na watu waliomjua? Ndugu zake, rafiki na zaidi ya wote Rusia! Mpenzi wake.
Alifahamu fika kuwa amekwishampoteza. Huu si uso ambao ulimfanya Rusia ampende. Hivyo, ni uso ambao utamfanya amdharau. Akajaribu kujikumbusha sura yake ilivyokuwa. Hakuweza kuikumbuka. Ilikuwa imekwishamtoka hata akilini. Alichofahamu peke yake ni kwamba alikuwa na sura nzuri, sura inayowavutia wasichana na kuwababaisha akina mama, sura ambayo ilimfanya Rusia ampende tangu walipoonana kwa mara ya kwnanza. Mara ngapi aliwaona wasichana wakimtazama kwa tamaa? Mara ngapi aliwafumania akina mama wakiteta kuwa ana sura nzuri? Ni yupi tena atakayemtazama kwa namna hiyo? Nani atakayewaza kuwa alikuwa na sura nzuri? Amepoteza kila kitu. Ameupoteza
uzuri, ameupoteza ujana na amempoteza mpenzi.
Jioni ile ambayo kamwe uwa haimtoki akilini ikamrudia tena mawazoni.
Alikuwa amejilaza juu ya kitanda chake akisikiliza redio. Kisha, ikamjia ile hamu yake ya sikuzote, hamu ya kumwona Rusia. Alikurupuka toka kitandani hapo na kumfuata nyumbani. Kwa bahati walikutana njiani. Rusia alikuwa akimjia, pengine kwa kiu ya kumwona vilevile. Wakarudi hali wameshikana mikono, maongezi na tabasamu za Rusia ziliifanya safari yao kuwa fupi zaidi. Walipofika ndani Rusia alijitupa kitandani kujipumzisha. Sikamona akamfuata na kujilaza pembeni yake. Kama kawaida tabasamu la Rusia lilimlaki. “Joto,” Sikamona alinong’ona akivua nguo zake. “Vipi ukilivua hilo gauni Rusia?” Rusia akatii. Ngozi yake laini, nyeusi ilimeremeta kwa namna ambayo iliufanya moyo wa Sikamona upoteze baadhi ya mapigo. Uso wake vilevile, ukisaidiwa na tabasamu laini, ulimfanya aonekane si malaika mzuri tu, bali pia ua zuri lililochanua ambalo linaalika nyuki na vipepeo. Yeye alijisikia kama nyuki anayealikwa. Subira ikamtoka. Akajikuta akimsogelea Rusia na kumkumbatia. Joto la mwili na ngozi laini, matiti yake mororo kifuani na tabasamu lake vilimfanya Sikamona ajihisi mwili wake ukitaka kutoka nje ya ngozi yake. Akapiga hatua ya pili. “La, la, la, Sika, tafadhali…” Rusia alisema bila kumsukuma. Sauti yake haikuwa na hasira, lakini tabasamu lilikuwa limeuacha uso wake.
“Tafadhali Rusia,”
“Hapana. Sio leo, Sika.”
“Kwa nini?” sauti yake ilikuwa na uchungu. Rusia alimtumbulia macho yaliyojaa aibu. Kisha akamwuliza kwa sauti ndogo, “Hujui mwenzio bado bikra?” maelezo ambayo yalimfanya Sikamona si azidi kumpenda tu, bali pamoja na kumheshimu kuliko wasichana wote aliowafahamu. Akaairisha chochote alichokusudia kukifanya. Ndipo tabasamu la Rusia liliporejea. Likamfariji. Wakatulia hali wamekumbatiana, wakiisubiri siku halali kwao wote.”
Kumbe haikutokea siku hiyo. Mapenzi yao yalikuwa yamefikia ukingoni. Ilikuwa kama ndoto, ndoto nzuri ya kupendeza, lakini ndoto ambayo ingeendelea kuwa ndoto. Siku hiyo ingesalia kama kumbukumbu tu katika maisha yake, kumbukumbu katika roho yake. Kumbukumbu ambayo itaandamana naye kaburini na kuishi naye huko kuzimu.
Akairekebisha bunduki yake na kuilekeza kichwani kwake. Akajiandaa kuifyatua. “Kwa heri dunia, kwa heri Rusia…”
“Sikamona.”
Sauti hiyo, kali yenye amri, ilimfanya asite kuifyatua bunduki yake na kugeuka. Alikutana na uso wa Brigedia Chungu pamoja na askari watatu nyuma yake.
“Usifanye hivyo Sikamona” Brigedia alisema