Miaka mitatu iliyopita Novemba 2009, gazeti la ----------- lilichapisha habari hii kwenye ukurasa wake wa kwanza kuhusu Zitto Kabwe.
Gazeti lilikuwa limefanya mahojiano na Mama Mzazi wa Zitto, Shida Salum. Katika mahojiano hayo, Mama Mzazi wa ZItto alikiri mwanawe kutumiwa na watu wasiokitakia mema chama.
Leo ni miaka mine tangu Mama Zitto kueleza hayo. Sasa wakati tukitafakari yanayompata Zitto ndani ya Chadema, tuyaangalia yale ambayo Mama Zitto alieleza wakati huo.
SHIDA Salum, mama mzazi wa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA), Zitto Kabwe, ameibuka na kusema mwanaye anatumiwa kukivuruga chama chake.
Akizungumzia taarifa zinazoandikwa na baadhi ya magazeti kuhusu kinachoitwa mgogoro wa uongozi katika CHADEMA, kati ya Zitto na viongozi wenzake, Shida alisema, hakuna mgogoro pale, kuna kikundi cha watu wanaotaka kumtumia mwanangu kufanikisha mambo yao.
Akizungumza na gazeti hili juzi jijini Dar es Salaam, alidai kuna watu walio nje ya CHADEMA wanakula njama za kumgombanisha mwanawe na viongozi wenzake.
Alisisitiza, kuna baadhi ya wanasiasa ndani ya CHADEMA wanaotumiwa na walio nje kugombanisha viongozi.
Akaongeza, Mambo ya uchaguzi yalikwisha kitambo na Zitto kwa moyo mmoja alikubali kumaliza tofauti zake na Mbowe (Freeman Mbowe) ndiyo maana akamuacha Mbowe kuwa mgombee pekee wa uenyekiti.
Shida aliwatuhumu watu walio nje ya CHADEMA akisema ndio wanaopandikiza mbegu za chuki kwa lengo la kuwavuruga. Hata hivyo, hakuwataja.
Alisema kila mwenye akili timamu anajua kinachotafutwa, na nani mkweli na yupi anasingiziwa.
Angalia wanaoandika haya. Kweli Zitto anaweza kutetewa na magazeti ya Habari Corporation yanayomilikiwa na Rostam Aziz halafu ukaamini kile kinachoandikwa? alihoji.
Aliongeza, Rostam yupi? Ni huyu tunayemjua au mwingine? Kwa wema upi alionao kwa chama chetu.
Wiki iliyopita magazeti ya Rai na Mtanzania yalinukuu taarifa zikidai kuwa zimetolewa na Shida, kwamba anataka mwanawe aondoke kwenye chama hicho kwa kile ilichoeleza kuwa kumwepuesha na yaliyomkuta Chacha Wangwe.
Katika kujibu hilo, Shida anasema, Mimi na Zitto tunajua katiba ya chama chetu. Tunafahamu taratibu za kuendesha chama. Yeye ni naibu katibu mkuu, mimi ni mjumbe wa Kamati Kuu. Tunajua nini maana ya uongozi, hivyo hatuwezi kukurupuka barabarani.
Kwamba kama kuna malalamiko au tuhuma mathalani juu ya uteuzi wa wabunge wa viti maalum, basi sote ni sehemu ya hicho kinacholalamikiwa. Kutokana na hali hiyo, hatuwezi kujifanya hatuhusiki na tukatuhumu kupitia vyombo vya habari, tena magazeti yanayomilikiwa na mwanachama wa CCM.
Shida alisema anajua kwa mapana chanzo cha yote yanayoandikwa na jitihada za kutaka kumgombanisha Zitto na viongozi wenzake, hasa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.
Yote haya tunafahamu chazo chake. Si uchaguzi wa ndani ya chama. Uchaguzi ulishakwisha na Zitto kwa moyo mmoja alikubali kumuachia Mbowe uenyekiti ili kulinda maslahi ya chama, alisema.
Alisema kuwa yeye kama mlezi, hawezi kuruhusu hali hiyo, hivyo atatumia nafasi yake ya mjumbe wa CC kuhakikisha kwamba tabia hiyo ya kugombanisha viongozi inakoma.
Nikiwa mzazi, mlezi na mjumbe wa kamati kuu ya CHADEMA, siwezi kuruhusu Zitto kutumika kuingiza chama katika mgogoro. Nitasimama imara kuhakikisha kwamba CHADEMA inakuwa salama, alisema.
Wiki iliyopita, Dk. Slaa aliwaondoa katika nafasi za utendaji David Kafulila aliyekuwa Afisa Habari na Danda Juju aliyekuwa Afisa anayeshughulika na Halmashauri na Bunge kwa kile kinachoelezwa kuwa utovu wa nidhamu kwa chama na viongozi wake.
Kafulila alinukuliwa na baadhi ya magazeti kuwa alibeza kikao cha viongozi wa juu wa chama hicho kilichofanyika Dodoma ambapo Mbowe na Dk. Slaa walikutana katika kikao cha kawaida na wabunge wa chama hicho na baadhi ya wakurugenzi.
Kafulila alisema mkutano huo wa viongozi haukuwa na maana; na alifika mbali zaidi kwa kuufananisha na vikao vya geto. Ni matamshi hayo na mengine yaliyomfanya Dk. Slaa kutumia mamlaka yake ya kikatiba kumuondoa Kafulila katika wadhifa huo.
Taarifa zinasema hoja ya kumuondoa Kafulila katika kikao ilitolewa na Msafiri Mtemelwa, mmoja wa viongozi wake na ambaye alikuwa meneja wa kampeni za Zitto wakati wa kuwania uenyekiti wa CHADEMA