Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Zuberi Kabwe kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Kijamii wa Twitter ameandika;
Aprili 2019 nilihoji Bungeni “TAKUKURU ndio taasisi ambayo tumeipa dhamana ya kupambana na rushwa. Bajeti ya 2019/2020 tunawaombea Sh 75 bilioni LAKINI hesabu zake hazijawahi kukaguliwa na mkaguzi yeyote yule.”
“Ni kwanini hawakaguliwi wala hawafungi hesabu?
Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa inataka TAKUKURU kukaguliwa mahesabu yake. Lakini kwa kujificha mgongo wa Ofisi ya Rais ambayo Bajeti ya Taasisi hii hupitishwa, TAKUKURU wanakwepa Ukaguzi. Prof. Assad alipotaka kuikagua alizuiwa na Rais. Kwanini?
Ni kwa sababu TAKUKURU inatumika kisiasa. Kama ilivyo Ofisi ya DPP na kwa kushirikiana, TAKUKURU hutumiwa na Dola kusumbua, kutisha au kubambikia watu Kesi iwapo wanakwenda kinyume na watawala. Wanasiasa wa CCM wanaopingana na utawala wa Magufuli na wa upinzani wakosoaji hulengwa.
Mwezi Machi mwaka 2017 niliitwa na TAKUKURU kuhojiwa kuhusu kilichoitwa kupokea Fedha kutoka Benki ya Standard Chartered Hong Kong ili kuwasaidia katika uchunguzi wa uporaji wa Fedha kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.
Nilipowauliza TAKUKURU nani kawaeleza upuuzi huo wakasema kuwa wameletewa barua na Mbunge mmoja wa zamani (hivi sasa ni RAS). Nikawaambia Mbunge huyo kawadanganya na mlipaswa kujiridhisha kwanza kwani Standard Chartered ni Benki kubwa na haiwezi kujiingiza kwenye upuuzi
Niliomba kumwona Bwana Mlowola Wakati huo akiwa Mkuu wa Taasisi na kumwambia uso kwa uso kuwa taasisi yake inatumika kisiasa. Narudia kumwambia Kaimu Mkurugenzi wa sasa hadharani kuwa taasisi yake inatumika kisiasa na yeye kakubali kutumika
Baada ya kuwaelimisha namna uchunguzi wa Tegeta Escrow ulivyofanywa na kuwaambia wawakamate waliochota Fedha Benki Kuu na kwamba nilifanya kazi yangu pamoja na wajumbe wa PAC kwa weledi wa hali ya juu sana, hawakuniita tena kuhusu hilo.
Mwaka 2018 wakaniita kuhusu tuhuma nilizowapa Watendaji wa Serikali kuhujumu Mradi wa Mchuchuma na Liganga. Nikawapa maelezo yangu ya kutosha. Ulikuwa usumbufu maana hawajachukua hatua yeyote dhidi ya wahujumu ambao ni pamoja na Rais Magufuli
Sasa TAKUKURU wanarudi tena kwenye Tegeta Escrow kwa tuhuma zingine za kubumba zenye lengo la kuniweka ndani muda mrefu ili nisishiriki Uchaguzi Mkuu. Ninawaambia tena, SIOGOPI. TAKUKURU Waache kufanya kazi kama Jumuiya ya Nne ya CCM - Wazazi, Wanawake, Vijana na TAKUKURU
Wala wasidhani kuwa nitaogopa kurudi Tanzania. Nitarudi mchana kweupe. Nitakuwa Mahakamani kusikiliza hukumu ndogo ya Kesi yangu ya uchochezi na pia kesi yangu dhidi ya Rais Magufuli kuvunja katiba ya nchi kwa kumfuta kazi CAG. Zote siku ya Jumanne tarehe 18/2/2020
-
Zitto Kabwe Ruyagwa