Naomba mwenye details atuweke sawa. Nimejaribu kutafuta gazeti la Mwananchi sijalipata mtandaoni na hapa nilipo siwezi kupata nakala. Kwani Masha kasema kuwa haoni utata kwa hiyo Bashe ni raia au haoni utata wowote katika kauli za CCM kwa hiyo Bashe siyo raia?:confused2::confused2:
Waziri: Uraia wa Bashe hauna utata Send to a friend Thursday, 19 August 2010 08:47 0diggsdigg
Waziri wa mambo ya nje Laurence masha(katikati),akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar-es-salaam jana walipotaka maelezoya sakata la uraia wa Hussein Bashe
CCM YASEMA DK KIGWANGALA RAIA Boniface Meena na Ramadhan Semtawa RAIS Jakaya Kikwete anasubiriwa kutatua kitendawili cha uraia wa Hussein Bashe baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, kueleza kuwa uraia wa kada huyo wa CCM, hauna utata wowote.
Hata hivyo, pamoja na Masha kusema kuwa hakuna utata katika uraia wa Bashe alipoulizwa na gazeti hili nje ya jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani jana, alishindwa kueleza bayaba kana ni raia au si raia.
Alipoulizwa zaidi kuhusu suala hilo, alisema litaisha baada ya rais Kikwete kuzinduza kampeni za uchaguzi. Masha ambaye awali alisema kuwa yeye ndiye mtu wa mwisho kuzungumzia suala hilo, alisisitiza kuwa uraia wa Bashe hauna utata.
Mahojiano kati ya Mwananchi na Waziri Masha nje ya ofisi za wizara hiyo jijini Dar es Salaam yalikuwa kama ifuatavyo; Mwananchi: Mheshimiwa sulala la Bashe unalizungumziaje? Masha: Hakuna utata kwenye uraia wa Bashe. Naweza kusema hivyo.
Mwananchi: Kama hakuna utata je, Bashe ni raia au si raia (wa Tanzania)? Masha: Nasema hakuna utata kwenye uraia wa Bashe na siwezi kuzungumzia suala hilo zaidi. Sikilizeni, hili suala halina umuhimu kama mnavyolizungumzia.
Mwananchi: Wewe ndiye unayethibitisha kuwa mtu ni raia au si raia. Sasa kwa nini usitueleze kuhusu hilo? Barua zilizochapishwa kwenye vyombo vya habari unazizungumziaje? Masha: Kumbe unajua kuwa mimi ndiye wa mwisho kuzungumzia hilo.
Sasa nasema hii 'issue' sio kama mnavyoizungumzia, nasisitiza hakuna utata. Nimekuja kuwaona msije mkasema kuwa waziri kagoma kutuona. Kuhusu barua zilizochapishwa, tunafuatilia tujue zimepatikana wapi. Mwananchi: Tunajua kiongozi wa juu ndiye aliyelizungumzia hilo na wewe uko chini yake, hilo unasemaje? Masha: Kumbe unajua. Mimi si msemaji wa Ikulu na hivyo tusubiri kampeni zianze tuendelee na michakato mingine. Mwananchi: Vipi kuhusu uraia wa Kigwangala ambaye tumesikia ni Mrundi? Masha: Nimeagiza watu wangu walifuatilie ili waweze kunipa taarifa.
Waziri Masha pamoja na viongozi wa Idara ya Uhamiaji na vyombo vya dola, juzi waliitwa ili wajadili kuhusu uraia wa Hussein Bashe, ambaye CCM kimedai kuwa si raia wa Tanzania na kumuengua kwenye kinyang'anyiro cha ubunge.
Masha, ambaye alikuwa jimboni kwake Nyamagana mkoani Mwanza akisaka wadhamini kwa ajili ya kutetea ubunge, aliwasili jijini Dar es Salaam kwa ndege ili kuhudhuria kikao hicho ambacho kilifanyika kuanzia saa 7:00 mchana pamoja na baadhi ya viongozi wa vyombo vya dola.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo gazeti hili ilizipata kutoka wizarani, viongozi hao walifanya kikao hicho kwenye ofisi za makao makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani. "Waziri alikuwa Mwanza, aliitwa kwa ajili ya kusimamia kikao kinachoendelea hadi hivi sasa," alieleza mpashaji wetu wa habari. Kabla ya kupatikana kwa taarifa hizo Mwananchi lilifika wizarani hapo kuonana na Waziri Masha, lakini lilielezwa kuwa yuko safarini Mwanza na kwamba, naibu wake alikuwa safarini.
Baadaye Mwananchi ilipata taarifa kuwa waziri alirejea Dar es salaam kwa ajili ya kikao hicho kwa ajili ya kuweka sawa suala la Bashe. Masha alipopigiwa simu alisema kuwa hajatoa taarifa ya kikao hivyo apewe muda wa kulishughulikia tatizo hilo kisha atatoa taarifa zote. "Sijakaa ofisini nataka nipate muda wa kufuatilia na nitatoa taarifa zote," alisema Masha.
Wakati hayo yakiendelea, Katibu Mkuu wa CCM, Yusufu Makamba amesema mgombea wake Dk Kigwangala, ni raia. "Tunachojua mgombea wetu ni raia," alisema Makamba.
Alisisitiza kwamba, kitendo cha Hussein Bashe kukumbwa na tuhuma za kutokuwa raia, zisijaribu kuwaingiza na watu wengine. Kwa mujibu wa Makamba, Dk Kigwangala ndiye aliyepitishwa na Nec kuwa mgombea ubunge na kwamba matokeo hayo hayawezi kubadilishwa.
Alipoulizwa haoni chama kinaweza kupoteza nafasi kama Dk Kigangwala atakuwa na tatizo hilo la kisheria, Makamba alijibu: "Tatizo la nini wakati nimesema yeye ni raia?" Makamba alifafanua kwamba, Dk Kigwangala ana sifa zote zinazomfanya awe mgombea ndiyo maana Nec ilimpitisha.
Kuhusu kama chama kinaweza kumrudisha Bashe kugombea nafasi hiyo, Makamba alisema: "Chama tayari kimeshamchagua mtu. Siwezi kuitisha uchaguzi halafu Nec, haya mambo yanafanyika kwa utaratibu wake, yaani leo hii niitishe Nec ijadili tena mgombea wa Nzega?"
Vyama vyote vya siasa leo vinapaswa kupelekea orodha ya majina ya wagombea wa nafasi zake mbalimbali za uchaguzi kuanzia udiwani, ubunge na urais.
Suala la Bashe lilizua utata mkubwa baada ya Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), kukataa kumpitisha kuwania ubunge wa Jimbo la Nzega akidaiwa kuwa si raia wa Tanzania kwa vile hakuukana uraia wa baba yake ambaye alikuwa Msomali wakati mwanasiasa huyo kijana akizaliwa.
Baada ya Nec kumuengua, ilibainika kuwa Idara ya Uhamiaji ilishampa Bashe uraia wa Tanzania tangu mwaka 2009 na wakati CCM ikielekea kwenye kikao hicho, (uhamiaji) ilimuandikia barua Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba kumueleza kuwa Bashe ni raia wa Tanzania wa kuzaliwa.
Kwa mujibu wa nyaraka nyingine kuhusu uthibisho wa uraia wa Bashe ambazo Mwananchi imeziona, inaonyesha kuwa baada ya kuomba uraia, Julai 10 ,2008 alipata barua kutoka Idara ya Uhamiaji ambayo ilisainiwa na Mashauri G.S kwa niaba ya Mkurugenzi wa Uhamiaji kueleza kukiri kupokea ombi la Bashe na ilikuwa ikilifanyia kazi. Barua hiyo yenye kumbukumbu Na 109758 ilimtaka Bashe awe na subira wakati ombi lake likishughulikiwa na mara litakapokuwa tayari atajulishwa kwa barua.
Septemba 24, 2008, Bashe alikula kiapo mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo kuthibisha kuwa ni Mnyamwezi kikabila na ni mzaliwa wa Nzega Tabora. Barua ya Agosti 10 mwaka huu iliyotolewa na Idara ya Uhamiaji yenye kumbukumbu Na DN 109758 na kusainiwa na P .O Mgonja kwa niaba ya Kaimu Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, ilikuwa ikimjulisha Bashe kuwa haina barua nyingine zaidi ya aliyopewa yenye namba S/N 312 ya Agosti 10, 2009 iliyomthibitisha kuwa ni raia wa Tanzania kwa kuzaliwa kwa mujibu wa kifungu 5(1) au 7(8) cha sheria ya Uraia Na 6 ya mwaka 1995 ambayo alikabidhiwa.
Tayari wanasheria wa Bashe wameshachukua hatua ya kufuatilia sakata zima la mteja wao kwenye ofisi za Idara ya Uhamiaji. Bashe aliongoza kura za maoni Jimbo la Nzega kwa kupata kura 14, 466, na kufuatiwa na Lucas Selelii aliyepata kura 2,706 wakati Khamis Kigwangala alipata kura 1,566. Kigwangala ndiye aliyepitishwa kupeperusha bendera ya CCM. Taarifa ya ziada ya CCM na Ramadhan Semtawa
Waziri: Uraia wa Bashe hauna utata