Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Ndugu zangu,Shwari na ndugu zangu wengine,
Niruhusini nikupeni historia ya wazalendo watatu katika siasa za vyama vya wafanyakazi mwishoni miaka ya 1940s kuelekea 1950s mjini Dar es Salaam.
Wazalendo hawa ni Erika Fiah, Kleist Sykes na mwanae Abdulwahid Kleist Sykes.
Nafanya hivi kwa kuwa Erika Fiah katajwa mara kadhaa hapa jamvini ningependa nikuhadithieni historia yake ili mpate kumfahamu vizuri.
Kwa kuwa ni historia ndefu nitatanguliza link ambayo ni kisa kizima na baadae In Shaa Allah nitaiweka historia hii kwa ufupi:
DAR ES SALAAM DOCKWORKERS’ UNION (CHAMA CHA MAKULI WA DAR ES SALAM) 1947 – 1950
DAR ES SALAAM DOCKWORKERS’ UNION (CHAMA CHA MAKULI WA DAR ES SALAM) 1947 – 1950 Utangulizi Historia ya Dar es Salaam Dockworker...mohamedsaidsalum.blogspot.com
''...tunakutana na Abdulwahid Sykes na African Association na hii ikiwa mwaka wa 1947 miaka miwili imepita baada ya yeye na mdogo wake Ally kurudi kutoka Burma walipokwenda kupigana katika Vita Kuu ya Pili.
Dhiki ilitawala mji mzima hasa kwa kuwa ndiyo kwanza Tanganyika ilikuwa inatoka katika kishindo na mkiki mkiki wa vita.
Hali hii ndiyo iliyomsukuma Abdul Sykes katika siasa na ikamfanya aelewe maana ya harakati za wananchi dhidi ya utawala wa kigeni akiwa bado kijana mdogo sana.
Kidogo kidogo baba yake alianza kumkabidhi Abdul kazi za African Association na mara akawa msaidizi wa baba yake katika siasa za Dar es Salaam.
Ilikuwa katika kutimiza haya ndipo Abdulwahid akajikuta anahusika na ule mgogoro wa makuli ulioibuka bandarini Dar es Salaam ambao ulikuwa ukichemka pole pole chini kwa chini kwa muda mrefu tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili.
Hatimaye, Abdul Sykes alihusika na harakati za siri za wafanyakazi bandarini ambao, wakiwa wamechoshwa na sheria za kazi za ukandamizaji na wakiwa wamechoka kunyonywa na makampuni ya meli, walikuwa wanapanga kuitisha mgomo.
Kleist mwenyewe alikuwa hakuwa mbali na siasa za wafanyakazi yeye akiwa mwajiriwa wa Tanganyika Railways alijaribu kuwakusanya wafanyakazi wa Railway kuasisi chama chao.
Kamati ndogo ya siri iliundwa na Abdulwahid akatiwa ndani ya kamati hiyo ili kuongoza mgomo uliokusudiwa.
Kazi ya kamati hiyo ilikuwa kupanga na kuratibu mikakati ya kuitisha mgomo ambao ungelisaidia katika kuondoa ile dhulma iliyokuwepo. Makuli waliitisha mkutano pembeni kidogo mwa mji, mahali palipokuwa pakijulikana kama ‘’Shamba kwa Mohamed Abeid,’’ katika bonde la Msimbazi.
Mohamed Abeid mwenye shamba hili alikuwa Muarabu mwenye asili ya Yemen na shamba lake lilianzia Msimbazi kuelekea Mchikichini.
Sehemu hii ilichaguliwa makhususi mbali na macho ya watu ili ipatikane faragha waweze kufanya shughuli yao waliyokusudia kwa utulivu.
Makuli walikula kiapo na kusoma Ahlal Badr ilii kujikinga na unafiki, usaliti pamoja na shari ya vizabizabina wangeokataa kugoma.
Siri ya mgomo huu ilihifadhika hakuna nje yao aliyejua nini kitatokea.
Mapema asubuhi moja kile kilichoanza kama mipango ya siri dhidi ya makampuni ya Wazungu bandarini, kililipuka na kuwa mapambano ya dhahiri.
Watu katika mitaa jirani ya Mtaa wa Aggrey, alipoishi Abdul na baba yake walikuwa hawajatoka vitandani mwao alifajiri moja wakasikia vishindo na makelele vimetanda mtaani.
Makuli, baadhi yao wakiwa vidari wazi, walikuwa wameizingira nyumba ya Kleist, wakipiga makelele wakimtaka Abdulwahid atoke nje.
Makuli wale walipiga kwata njia nzima kutoka bandarini huku wakitoa maneno ya kupinga ukoloni na wakiimba kupandisha morali zao.
Tukio hili halikuwa na kifani. Ilikuwa ni mara ya kwanza nchini Tanganyika kwa wananchi kushuhudia katika mitaa ya Dar es Salaam uasi wa dhahiri kama huo dhidi ya serikali ya kikoloni.
Abdul Sykes wakati ule kijana mdogo kabisa wa umri wa miaka 23, akichungulia kupitia dirisha la chumba chake alichokuwa amelala, alishangazwa kuona umati mkubwa wa watu nje ya nyumba yao.
Aliweza kuwatambua baadhi ya wenzake katika kamati ile ya siri iliyokuwa inapanga mipango ya mgomo.
Alipotoka nje kuonana nao makuli wenye hasira walimfahamisha kuwa mgomo ulikuwa umeanza na wasingerudi kazini hadi madai yao yote yamekubaliwa.
Mgomo huu ulienea kama moto wa makumbi ulikumba nchi nzima kwa kasi ya ajabu.
Ilikuwa kama vile wafanyakazi wa nchi nzima wametaarifiana.
Wafanyakazi wa Tanganyika Railways huko Tabora wakiongozwa na babu yangu Salum Abdallah waliingia kwenye mgomo tarehe 11 Septemba, siku tano baada ya mgomo wa makuli kuanza Dar es Salam.
Mgomo ule ulisababisha serikali ya kikoloni kupitisha sheria ambayo iliruhusu kuundwa na hatimae kusajiliwa kwa Dar es Salaam Dockworkers’ Union.
View attachment 2068228
Abdul Sykes katika unifom ya KAR
Burma Infantry
Itaendelea...
Miaka zaidi ya 30 sasa imepita toka niliposoma Nyaraka za Sykes.
Hivi sasa katika mambo yanayonisikitisha ni kwa Sykes kuzirejesha hizi nyaraka kwenye ''safe,'' kuzifungia na kutoziweka wazi kwa watafiti kuzisoma.
Watafiti wangepewa fursa ya kuzipitia wangeona kuwa kila mzalendo pamoja na wakoloni Waingereza waliohusika katika siasa za kipindi kile wamo ndani ya nyaraka hizi.
MJ Molohan.
Nimemsoma ndani ya Nyaraka za Sykes.
MJ Molohan Mwingereza huyu alikuwa Kamishina wa Kazi nimemkuta katika Nyaraka za Sykes akipambana na Kleist Sykes miaka ya 1930s hadi 1950 anashughulika na watoto wa Kleist katika siasa za wafanyakazi Waafrika.
Kwanza na Abdul katika Dockworkers' Union kisha na Ally katika TAGSA.
Baada ya mgomo ule wa makuli na sheria ya kuundwa kwa vyama vya wafanyakazi kupita Molohan alianza mchakato wa kutafuta watu ambao wangeweza kushika nafasi ya Katibu Mkuu wa Dockworkers’ Union.
Islam Barakat alikuwa Labour Inspector wa kwanza Mwafrika ingawa alikuwa na damu ya Kiarabu na Kiafrika.
Molohan alimwomba Barakati amsaidie kutafuta mtu wa kusika nafasi ya Secretary General wa Dockworkers' Union.
Barakat alipeleka majina mawili.
Jina la Abdul Sykes na la Erika Fiah.
Abdul Sykes, kijana wa mjini miaka 24, mtoto wa mfanyabiashara na mwanasiasa maarufu Dar es Salaam.
Jina lingine lilikuwa la Erika Fiah miaka 53, mwanasiasa mpevu na mtu wa makamo.
Erika Fiah alikuja Tanganyika pamoja na ma crejeshi ya Waingereza kutoka Uganda wakati wa Vita Kuu vya Kwanza.
Baada ya vita alilowea Tanganyika na kuishi Mission Quarters ambako alihariri gazeti lake, Kwetu.
Fiah alikuwa Mwafrika wa kwanza kuanzisha na kumiliki gazeti lake mwenyewe katika Tanganyika.
Mtu wa pili alikuwa Ramadhani Mashado Plantan mtoto wa Chief Mohosh Shangaan kutoka Mozambique alikuyekuwa Tanganyika na Hermann von Wissman akiongoza jeshi la askari mamluki wa Kizulu.
Tanganyika akajulikana kama Affande Plantan mkuu wa Germany Constabulary.
Watoto wake kama walivyokuja kuwa watoto wa Kleist wameacha historia kubwa katika Tanganyika.
Fiah kama wanasiasa wote wa zama zake, alikuwa Mwafrika kwanza na uzalendo ukafuatia.
Vilevile alikuwa mmoja wa wafuasi wa mwanzo wa Karl Marx nchini Tanganyika na gazeti lake Kwetu, lilikuwa maarufu kwa sababu ya ukali na vijembe vyake dhidi ya ukoloni.
Fiah alikuwa mwanasiasa aliyekuwa amepea sana katika wakati wake.
Katika miaka ya 1930 aliwahi kujaribu kuhamasisha tabaka la wafanyakazi na wakulima kuwaunganisha dhidi ya ukoloni, lakini alishindwa kwa kuwa wananchi walikuwa bado hawajaamka kiasi cha kutosha kuweza kuitikia mwito wa kuuhamasisha umma kama tabaka.
Kwa wakati ule Fiah alikuwa na upeo mkubwa wa siasa na alikuwa na uwezo wa kuhamasisha zaidi kuliko kijana mdogo Abdul Sykes.
Vilevile Fiah alikuwa mtu mzima na uzee ni dawa.
Haiwezekani kumlinganisha Fiah na Abdul Sykes aliyekuwa kijana mdogo ambaye Fiah angeweza kuwa mtoto wake.
Kati ya kipindi kile kati ya vita vya kwanza na vya pili ya dunia, Fiah alitumia kalamu yake kudhihirisha bila ya woga matatizo yanayowakabili Waafrika.
Lakini Fiah hakuwa tu adui wa serikali alikuwa pia adui wa Kleist na Waafrika wengine mashuhuri, wengi wa hao wakiwa katika utumishi wa serikali.
Huko nyuma katika mwaka wa 1933 kulikuwako na mgongano baina ya Kleist na Fiah kuhusu uongozi wa African Association.
Kupitia gazeti lake Fiah alimshambulia Kleist akimshutumu kwa kile Fiah alichokiona kuwa tabia yake isiyokuwa ya kizalendo iliyotokana na asili yake ya Kizulu.
Fiah alidai kuwa mambo yanapokuwa mazuri kwa Watanganyika Kleist atajinasibisha na Utanganyika, lakini upepo unapobadilika na kuvuma upande wa Wazulu, mara Kleist anakuwa Mzulu.
Ili kuepuka mgongano Kleist alijiuzulu kama katibu wa African Association na Fiah alichaguliwa kushika nafasi hiyo.
Kalamu ya Fiah ilikuwa haina muhali. Katika rambirambi alizotoa za kijeuri na za dharau juu ya kifo cha Martin Kayamba, Fiah aliomboleza kwa kusema kwamba Waafrika hawakunufaika kwa elimu ya Kayamba wala kwa wadhifa wake kama karani wa kaimu Katibu Mkuu katika serikali ya Waingereza.
Fiah alipingana na Wazungu vilevile.
Mwaka wa 1940 aliandika tahariri iliyowalenga Wazungu waliokuwa wakimpinga kwa kueleza wazi wazi fikra zake na kwa kuchapisha gazetini makala juu ya haki za Waafrika.
Fiah alikuwa mwanaume kweli kweli hata ingawa wakati wa zile harakati za bandarini makuli wakiwa wanakwenda nyumbani kwa Kleist kumfuata mwanae Abdul kwa maandamano na hivyo kumpa hadhi ya uongozi wa harakati zile, kwa hakika Abdul Sykes hakuwa anafikia hadhi wala kiwango cha Fiah ktika siasa za nyakati zile.
Kumfananisha Abdulwahid na Fiah ilikuwa sawa na kufananisha mlima na kichuguu.
Mara kwa mara mawazo ya Erika Fiah kama ilivyotegemewa hayakupokelewa vizuri na serikali katika ya hao waliokuwa serikalini akiwa MJ Molohan.
Ndugu zangu ikiwa kama hamkumjua Fiah huyu ndiye Erika Fiah.
Erika Fiah, Kleist Sykes, Mzee bin Sudi, babu yangu Salum Abdallah kwa kuwataja wachache hawa wote wakifahamika kama ''Wakuja,'' na wenyeji wakiwasema kuwa wanapenda sana kujitia kimbelembele.
Ile ''Wakuja,'' wakiwa na maana kuwa hawana asili ya Tanganyika.
In Shaa Allah darsa litaendelea tutatazama mapambano baina ya Abdul Sykes na Erika Fiah.
Erika Fiah