Abdul Nondo: Bilioni 28 za Matumizi mengine za Wizara inajumuisha posho, mafuta ya gari, chai na vitumbua n.k

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
5,352
Reaction score
15,876
Your browser is not able to display this video.

​
Utangulizi
Ngome ya vijana ACT-Wazalendo kwa niaba ya vijana, tumefuatilia hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri Joel Arthur Nanauka aliyoitoa jana tarehe 20 Aprili, 2026 kuhusu Mpango na Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Vijana kwa Mwaka 2026/2027.

Katika ufuatiliaji wetu, tumeainisha maeneo yenye kasoro na changamoto yanayoongeza ugumu katika utekelezaji wa bajeti hii kufikia malengo ya kusaidia na kustawisha maendeleo ya vijana kiuchumi. Hotuba ya Mh. Waziri Nanauka haijakidhi kiwango cha utatuzi wa changamoto zinazowakabili vijana nchini hasa ukosefu wa ajira, uwezeshaji wa vijana kiuchumi (mikopo), ujuzi na mazingira wezeshi ya kujiajiri. Hotuba ya Waziri haijajibu utatuzi wa changamoto za mifumo ya kitaasisi, kiuwajibikaji, kisheria, kimiongozo na kiuratibu ili kusaidia ustawi wa kundi la vijana.

Kwa ujumla, ukisoma hotuba ya bajeti ya Waziri na ukisikia hoja katika randama ya Mpango na Bajeti kwa 2026/2027, unagundua kabisa ya kwamba bado wizara haipo ‘serious’ katika utatuzi wa changamoto za vijana na uwezeshaji vijana kiuchumi. Tuna hoja zifuatazo;-
​

Uwiano Usiokidhi kwenye Bajeti ya Wizara Kati ya Fedha za Matumizi ya Kawaida na Fedha za Miradi ya Maendeleo​

Wizara ya Maendeleo ya Vijana kupitia Waziri Joel Nanauka imeomba kuidhinishiwa Bajeti ya Tsh. 35,957,298,000 (Bilioni 35) kwa mwaka 2026/2027 kwa mchanganuo ufuatao;

  • Tsh. 30,104,264,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambayo hujumuisha mishahara (PE -Personal Emoluments) na matumizi mengine (OC-Other Charges). Ambapo kati ya hizo Tsh.30,104,264,000, mishahara ni Tsh. 1,227,961,000 (Bilion 1 na million 227) na matumizi mengine(OC yaani Other Charges) imetengwa Tsh. 28,876,303,000 (Bilion 28 na milioni 876) kwa ajili ya nauli, posho, kununua samani, kununua vitendea kazi, karatasi, kulipia umeme wa ofisi, mafuta ya magari, chai na vitafunwa, sare za sherehe za kitaifa, posho na kujikimu kwa watumishi, safari za ndani na nje ya nchi, matengenezo ya magari na vifaa kama viyoyozi vya ofisi, ununuzi wa magari, likizo, mikutano na warsha sawa na 83% ya bajeti yote.
  • Wakati fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya vijana ni Tsh. 5,853,034,000 ambapo Milion 853 ni kwa ajili ya program ya kukuza kazi za staha nchini na Tsh. 5,000,000,000 (Bilioni 5) tuu ndio fedha za uwezeshaji vijana kiuchumi kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana sawa na 17% ya bajeti yote, ambapo kati ya hiyo bilioni 5, Tsh. 4,700,000,000 (bilioni 4 na milioni 700 ni fedha ya mikopo kwa vijana kwa makundi 100 tuu hadi kufikia Juni 2027 na milioni 300 ni kwa ajili ya mafunzo ya ujuzi na ujasiriliamali kwa makundi 100 hadi kufikia Juni 2027. Fedha hizi chache, ndogo hazikidhi idadi ya vijana wenye uhitaji na inaonesha namna gani bado hatuna dhamira ya dhati.
Mapendekezo Yetu Katika Hoja Hii;
Tunaungana na hoja ya Mbunge na Katibu Mkuu wetu Ndg. Ado Shaibu Ado aliyoongea Bungeni kwa kuitaka Serikali iongeze fedha katika mfuko wa maendeleo ya vijana kwa kurejesha fedha zote za vijana kati ya bilioni 200 zilizopelekwa wizara za kisekta ili kuvimbisha mfuko wa maendeleo ya vijana. Lakini pia, Ngome ya Vijana tunaitaka serikali ipunguze fedha za matumizi mengine (OC) Tsh. 28,876,303,000 ili kuongezea kwenye miradi ya maendeleo kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana kwa kuongeza uwezeshaji wa vijana kulingana na idadi kubwa na uhitaji wa mikopo kwa vijana.

Wizara hii ni mpya, haiwezi kuwa na fedha ya matumizi ya kawaida mara 5 ya fedha za miradi ya maendeleo. Haiwezekani kati ya fedha yote ya bajeti TSh. 35,957,298,000 (Bilioni 35), TSh. Tsh. 4,700,000,000 tu ndiyo iwe fedha ya mikopo kwa vijana kwa makundi 100 tu kwa mwaka 2026/2027.

Wizara yenyewe imekiri kwenye hotuba yake ukurasa wa 22 kifungu cha 35 kwamba wizara inakabiliwa na changamoto ya ongezeko la uhitaji wa mikopo ukilinganisha na kiasi kinachotengwa alafu bajeti yake inaleta mambo haya, hii haiwezekani maboresho yafanyike.

Hoja ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi Kupitia Bilioni 200 za Mikopo kwa Vijana.​

Kwenye ukurasa wa 13 wa kitabu cha Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Vijana, Mh. Waziri Joel Arthur Nanauka anasema hadi kufikia Aprili 3, 2026 takribani vijana 30,384 walikuwa wameomba fedha kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Ngome ya Vijana ACT-Wazalendo tunasema idadi hii sio ishara njema wala sio mafanikio ya kujivunia kwani ni idadi ndogo sana ukilinganisha na idadi ya vijana wenye uhitaji wa uwezeshwaji na mikopo kama mitaji. Idadi hii ndogo imechangiwa na wizara kwa sababu zifuatazo;

Ukosefu wa taarifa za kina, uratibu na taratibu za kueleweka za namna ya kuomba fedha hizo.​

Taarifa zimekuwa hazieleweki na wizara ya maendeleo ya vijana kama wizara mama yenye wajibu wa kuratibu na kutoa taarifa imekuwa haifanyi hivyo kwa kiwango kinachokidhi na kuridhisha. Akaunti binafsi ya mitandao ya kijamii ya Waziri na wizara ndiyo imekuwa njia kuu ya kutoa taarifa na kukwepa kutumia vyombo vya habari, mahojiano na mijadala kwa ufafanuzi ili kufikia vijana wengi zaidi.

Vigezo na masharti ya kibaguzi kwa vijana kuomba mkopo.​

Vijana wengi walishindwa kuomba sababu wengi walibaguliwa na vigezo kama vile kuwa na kitambulisho cha NIDA vijana wengi hawana NIDA hasa wale wa maeneo ya mipakani kama Kigoma. Vigezo vingine kwamba kijana awe kwenye eneo linalotambuliwa na mamlaka kwa ajili ya kufanyia biashara mfano soko (physical business address/existing business), kijana awe na leseni ya biashara, awe na TIN ya biashara ni masharti magumu kwa vijana wengi. Kijana hawezi kupata leseni ya biashara katika mfumo wa TAUSI halmashauri au TIN ya biashara TRA kama hana mkataba wa pango. Kijana awe na barua ya utambulisho wa eneo la

biashara kutoka kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa/kijiji. Vijana wengi wameshindwa kupewa barua ya utambulisho serikali ya mitaa baada ya kushindwa kuonesha wapi na eneo gani biashara zao zipo. Vijana wetu baadhi na mimi pia nilishiriki kuomba ili kushuhudia changamoto hizi. Mimi pia niliulizwa eneo la biashara yangu ilipo nilipowaonesha ndipo wakanipa barua ya utambulisho nikaomba ila kwa vijana ambao walishindwa kuonesha eneo la biashara sababu ndiyo wanaanza walinyimwa barua ya utambulisho hivyo hawakuweza kuomba huo mkopo. Inaonekana fika vigezo hivi vya wizara ya maendeleo ya vijana ni kwa ajili ya wenye biashara tu ila vijana wasio na biashara au wanaotaka kuanza ambao ndio wengi zaidi wanabaguliwa na vigezo hivi.

Muda mfupi wa kuomba.​

Wizara ilifungua dirisha la maombi ya mkopo huu wa mfuko wa maendeleo ya vijana tarehe 19 Machi hadi tarehe 3 Aprili 2026 takribani siku 12 ambazo hazikuweza kutosha sababu ya uhaba wa taarifa za kutosha na pia ni muda mfupi sana kwa vijana wasio na leseni. Kuomba leseni ya biashara na kupata ndani ya muda huu ni vigumu. Katika hotuba yake Mh. Waziri Joel Nanauka ukurasa wa 10 kifungu cha 14 anaonesha changamoto zilizotajwa na vijana kwenye ziara yake ni pamoja na vijana kutokidhi vigezo vya mkopo kwenye taasisi za kifedha. Ngome ya vijana tulitarajia angekuja na majawabu badala yake na yeye amekuja na vigezo na masharti yanayowazuia vijana wengi kuomba mkopo huu na ndiyo maana idadi imekuwa ndogo.

Mapendekezo Yetu Katika Hoja Hii;​

  • Wizara ya Maendeleo ya Vijana ipitie upya masharti na vigezo vyake na kuondoa vigezo vya kuwa na leseni ya biashara isiwe lazima kwa ambao hawana leseni, kigezo cha barua ya utambulisho serikali za mitaa eneo la biashara kiondolewe badala yake iwe barua ya utambulisho wa makazi kumtambulisha kijana anapoishi, kigezo cha NIDA kiondolewe isiwe lazima kwa ambao hawana NIDA kwani vijana wengi hawana NIDA.

  • Awamu ya pili ya dirisha la kuomba mkopo lifunguliwe mara moja ili vijana ambao hawakupata fursa kuomba awamu ya kwanza wapate kuomba sasa. Tarehe ya lini dirisha la pili litafunguliwe itangazwe mapema zaidi ili vijana wapate kujiandaa. Muda uwe wa kutosha kuwezesha vijana kuomba.

  • Uratibu wa taarifa, hamasa na miongozo ya wazi itolewe kupitia vyombo vya habari, radio, magazeti, mijadala na mahojiano ili kurahisha taarifa kufikia vijana kwa wepesi, haraka na kwa uthabiti.

  • Waziri wa Maendeleo ya Vijana Mh. Joel Nanauka ametoa taarifa za vijana 30,384 tu walioomba mkopo kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana. Wizara hii ndiyo yenye jukumu la kuratibu kwa kushirikiana na wizara zingine za kisekta katika masuala yote ya vijana. Lakini hakuna taarifa yoyote kuhusu mikopo mingine ya vijana inayotolewa kwenye wizara zingine za kisekta kama kilimo, mifugo na uvuvi, viwanda na biashara, madini, elimu, sayansi na teknolojia, wanawake na makundi maalum. Ndiyo maana tunazidi kusisitiza ya kwamba fedha zote zinazohusu vijana zipitishwe kwenye mfuko mmoja wa maendeleo ya vijana ili ziratibiwe, kusimamiwa vizuri sehemu moja ili kuongeza uwajibikaji kuliko kuzitawanya katika wizara tofauti za kisekta. Sambamba na kutengeneza sheria ya Bunge ya kuendesha mfuko wa maendeleo ya vijana.

Hoja ya Kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Vijana.​

Katika hotuba hii ya Waziri Joel Nanauka ukurasa wa 29, kifungu cha 45 anasema wizara itaangalia ili kuanzisha Benki ya Vijana kwa ajili ya kurahisisha uwezeshwaji vijana katika kupata mikopo na mitaji.

Ngome ya vijana ACT wazalendo tunamwambia Mh. Waziri ya kwamba changamoto ya uwezeshaji vijana kiuchumi haitokani na kutokuwa na Benki ya Vijana bali inachangiwa kwa kutokuwa na dhamira ya dhati ya serikali katika kupambana na ubadhilifu na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji, utaasisi, uratibu, udhibiti, usimamizi madhubuti, ufuatiliaji, miongozo madhubuti na ukosefu wa dhamira ya pamoja katika taasisi za serikali katika kuandalia vijana mazingira wezeshi ya kujikwamua. Bila kuwa na hizi nguzo ni kazi bure.

Tumekuwa tukiona katika taarifa za CAG kila mwaka namna fedha zinavyoliwa na kupotea, namna mikopo ya vijana 10% ngazi ya Halmashauri inavyotafunwa bila uwajibikaji, vikundi hewa kila mwaka, fedha zinazotengwa kwa ajili ya mikopo ya vijana hazitolewi mfano Tsh. 1,000,000,000 zilizotengwa kwa ajili ya kuwezesha vijana 2025/2026 hadi Februari 2026 fedha hizo hazijatolewa kwa mujibu wa randama ya mpango na bajeti ya wizara ya maendeleo ya vijana kwa mwaka 2026/2027.

Bila nguzo hizi hata hiyo benki ya vijana haitadumu na changamoto zitabakia hivyo hivyo. Tunapaswa tutangulize dhamira na sio kufanya mambo kisiasa. Tuna mifano mingi, mwaka 1999 wanawake wajasiriamali nchini walikuja na wazo la kuanzisha Benki ya Wanawake kwa Rais Mkapa ili kuwezesha wanawake kiuchumi na kukopeshesheka.

Baada ya miaka 8 mwaka 2007 benki ya wanawake ilianzishwa “Tanzania Women’s Bank” (TWB) serikali ikiwa na hisa za 97% na watu binafsi 3% ikaanza kufanya kazi tarehe 28 Julai, 2009. Ndani ya miaka 9 tu Benki hiyo ya wanawake ikafa. Tarehe 03 Agosti, 2018 Benki ya Wanawake ikazikwa rasmi kwa tangazo la Benki ya Tanzania (BOT) la tarehe 02 Agosti 2018 baadaya kuiunganisha na Benki ya TPB (Tanzania Postal Bank) ambapo 2021 ikabadilishwa kuitwa TCB-Tanzania Commercial Bank.

Benki ya wanawake ilikufa kwa sababu ya usimamizi mbovu, matumizi mabaya ya fedha bila uwajibikaji na ukosefu wa mtaji na utayari wa serikali kwani mwisho serikali iliona ni mzigo sababu benki ilianzishwa kisiasa, mifano ni mingi vipi hali ya bank ya serikali TIB- Development Bank ipo taabani, vipi TADB (Bank ya wakulima) ipo taabani alafu wizara inawaza tena kuongeza Bank nyingine ya serikali.

Pendekezo Katika Hoja Hii;​

a) Serikali kupitia wizara ya maendeleo ya vijana iachane na hili wazo la Benki ya Vijana kwani limekaa kisiasa Zaidi. Badala yake serikali ijikite kwanza katika kupambana na ubadhilifu na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji, utaasisi, uratibu, udhibiti, usimamizi madhubuti, ufuatiliaji, miongozo madhubuti na kuwe na dhamira ya pamoja katika taasisi za serikali na viongozi wa serikali katika kusaidia vijana kujikwamua kiuchumi kama kuwapa vijana msamaha wa kodi na tozo katika kipindi fulani biashara inapoanza kukua. Serikali ina mambo mengi ya kuboresha na kufanya kabla ya kufikiria kuanzisha benki ya maendeleo ya vijana. Serikali inatakiwa kuboresha sera, sheria na miongozo yake katika kutengeneza mazingira ya kuwezesha vijana kiuchumi.

Wizara Kuandaa Muongozo wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi​

Katika hotuba ya bajeti ukurasa wa 13 kifungu cha 18, Waziri Mheshimiwa Joel Arthur Nanauka anasema punde tu baada ya kukabidhiwa jukumu la uratibu wa uwezeshaji vijana kiuchumi kwa kutoa mikopo kwa vijana, wizara iliandaa muongozo wa utekelezaji wa program ya uwezeshaji vijana kiuchumi uliojikita kuweka viwango vya ufanisi, uwazi, uwajibikaji, taratibu za utoaji, usimamizi na urejeshaji wa mikopo, sifa za wakopaji na

mifumo ya ufuatiliaji na tathmini. Katika hili aidha Waziri Joel Nanauka aliamua kulidangaya Bunge kwamba kuna muongozo ikiwa haupo au muongozo huo anao yeye binafsi tu. Ngome ya Vijana ACT wazalendo tulikuwa wa kwanza kutaka wizara itengeneze muongozo utakaoratibu utolewaji wa fedha, marejesho, sifa, uwajibikaji na utaratibu wa ufuatiliaji na tathmini kabla ya kuanza mchakato wa utolewaji mikopo. Hadi vijana wanaambiwa waombe fedha kupitia wizara za kisekta na wizara ya maendeleo ya vijana hakukuwa na muongozo wowote uliowekwa wazi kuongoza utolewaji wa fedha, marejesho, sifa, uwajibukaji, ufuatiiaji na tathmini isipokuwa kumekuwepo na vipeperushi tu vya wizara mbalimbali za kisekta.

Pendekezo Letu Katika Hoja Hii;​

a) Kama muongozo hakuna ni muda sasa wizara ya maendeleo ya vijana kutengeneza muongozo wa jumla wenye taarifa mahususi juu ya utaratibu wa ukopaji, sifa, marejesho, usimamizi, ufuatiliaji na tathmini. Kama muongozo huo anao Waziri mwenyewe ni muda sasa muongozo huo kusambazwa ili vijana na wadau mbalimbali wapate kuusoma.

Wizara ya Vijana Imeshindwa Kueleza Bunge na Watanzania Namna Itakavyoboresha Muundo wake wa Utendaji kwa Mwaka 2026/2027​

Wizara hii ni mpya tulitarajia kusikia mipango ya wizara ya maendeleo ya vijana katika kuboresha muundo wake katika kuratibu, kusimamia na kufikia vijana hadi ngazi za chini. Wizara kuendelea kutumia maafisa maendeleo ya jamii ambao wapo chini ya Mkurugenzi wa Halmshauri (TAMISEMI) au kuendelea kuacha mafisa maendeleo wa vijana chini ya TAMISEMI ngazi ya Halmashauri na Mkoa ni kuendelea kuifanya wizara hii kutokuwa na nguvu ya uwajibishaji (Answerability and Accountability), pia ni kuendelea kuifanya wizara ya maendeleo ya vijana kuelea juu juu bila miguu ya kufika chini walipo vijana.

Pendekezo Letu Katika Hoja Hii;​

a) Ngome ya Vijana ACT-Wazalendo bado tunapendekeza kiundwe chombo maalumu kwa sheria ya Bunge chini ya Wizara ya Maendeleo ya Vijana kitakachoitwa “Wakala wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi Tanzania” yaani Tanzania Youth Economic Empowerment Agency (TYEA). Chombo hiki jukumu lake kuu liwe ni kuratibu utolewaji na urejeshaji wa mikopo kwa vijana, kufuatilia, kuhamasisha, kushauri na kulea vijana kimaarifa, kutoa ushauri wa kitaalamu kwa vijana kuhusu miradi na shughuli za kiuchumi, kusimamia marejesho ya mikopo na kuwaunganisha vijana na fursa mbalimbali za kiuchumi, kuratibu na kukusanya taarifa za fursa kwa vijana kutoka idara zingine za serikali ili kunufaisha vijana. Chombo hiki kishuke hadi ngazi za chini, ngazi ya Mkoa na Wilaya. Kifanye kazi kwa kushirikiana na viongozi wa Halmashauri na viongozi wa serikali za mitaa.


Abdul Omary Nondo.
Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa-ACT Wazalendo. 21 Aprili, 2026.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…