Mr. Ebbo hatunaye tena duniani! Ni masikitiko makubwa sana kumpoteza mwanaharakati wa muziki kama Mr Ebbo. MuzikI wake ulivutia, kufundisha, kuonya, kudumisha mila na utamaduni. Ni mwakilishi wa wamasai kwenye uwanja wa muziki lakini pia hata Tanzania nzima hasa pale tunapozungumzia muziki nje ya mipaka ya Tanzania. Mr. Ebbo namkumbuka sana kwa ujasiri wake wa kuenzi mila na desturi za kabila lake. Ni wasanii wachache wanaoweza na kuthubutu kudumisha mila na desturi za kabila wanazotoka. Tunashuhudia wasanii wengi wakifanya sanaa ndani ya DSM na kujiinua kuwa wao ndio watoto wa jiji. Huwezi kuwaona wasanii hasa wa muziki wakitukuza na kujivunia desturi za kwao. Hii nadhani ibaki kama kumbukumbu kwa wasanii wote wa muziki Tanzania na hata wale wa sanaa nyingine kuwa na "homage arts".
Ikumbukwe kuwa Mungu alivyotuumba muda wetu wa kuishi duniani hatuna dhamana nao; dhamana hii ipo mikononi mwa Mwenyezi Mungu aliyetuumba. Hivyo hatuna budi kuwa makini na wakati, na kufanya kila kitu na mipango yetu kana kwamba tunakufa kesho. Mr. Ebbo alikuwa sana serious na kazi zake bila haya usiku na mchana.
Mr. Ebbo hatunaye tena, basi tubaki na yale yote mema aliyoyatenda angali hai kwa manufaa yetu na kwa wale watakaobaki baada ya maisha yetu kukoma duniani kama ilivyompata Mr. Ebbo.
Natoa pole sana kwa familia ya mzee Motika, ndugu jamaa na marafiki wa mbali na wa karibu wa familia ya mzee Motika; pia kwa wapenzi wote wa kazi za marehemu Mr. Ebbo. Mwenyezi Mungu atujalie wote mioyo ya subira, uvumilivu na faraja kwa wakati huu wa majonzi mazito sana. Mungu atusaidie sana kuzienzi kazi zote nzuri alizoziacha mwenzetu.
BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA JINA LA BWANA LIHIMIDIWE! AMEN!