Adhabu ya viboko, kwa maoni yangu HAIFAI, HAIFAI, HAIFAI KABISA si kwa watoto majumbani wala kwa wanafunzi mashuleni kote HAIFAI. Adhabu ya viboko inavyoendelea sasa ni kielelezo cha jinsi wanadamu walivyo na tabia za kinyama na kishenzi, wenye udumavu wa akili na wasiotaka kubadilika. Kwa lugha nyepesi ni kwamba UMEKOSA MUDA WA KUTULIA NA KUFIKIRI kupata namna bora ya kumuadhibu mtoto/mwanafunzi na kilichobaki ni kumdhuru mwili wake. Umekosa maarifa mbadala. Unatumia nguvu kuliko akili yako, kama wewe unatumia nguvu zaidi kuliko akili, wewe una tofauti gani na mnyama?
Wengi wanaoamini katika adhabu ya viboko wanasumbuliwa na imani kwamba mtoto au mwanafunzi ndiye mwenye tatizo, lakini kiuhalisia mwenye tatizo ni mchapa viboko au anayeamini katika viboko na si mtoto au mwanafunzi. Ndiyo, iko hivi, kama wewe hivi sasa una tabia ya kuchapa au kupiga watoto wako au wanafunzi wako viboko, basi tambua mwenye tatizo hapo ni wewe na si watoto au wanafunzi.
Jifanyie uchunguzi mdogo wewe mwenyewe (Mchapaji viboko) hasa pale wakati unapoinua mkono au fimbo kuchapa (hapo hapo!) jiulize swali: Hali yangu ya utulivu wa akili hapa ikoje? (What is my state of mind?) Utagundua akili yako haiko sawa, unagundua una hasira, una msongo fulani wa mawazo, una haraka, au umechoka, na mara nyingi kuchoka kwako kumesababbishwa na kitu kingine, labda kazi, ugumu wa maisha, mahusiano na kero zingine mbalimbali.
Hivyo kumchapa mtoto/mwanafunzi ni njia ya mkato ya kumaliza tatizo au ukorofi wa mtoto, hii si fikra sahihi, lakini hivyo ndivyo wachapaji wanavyoamini.
Adhabu mbadala za kuwapa watoto na wanafunzi wetu ziko tele tu, lakini inabidi ujifunze polepole na lazima uwe na nia ya dhati ya kujifunza misingi yake ni nini. Kujifunza ni mchakato hivyo, lazima ujipe muda wa kutuliza akili yako, ili mtoto akienda kinyume ujiulize msingi wa yeye kwenda kinyume ni nini, na hata ukiamua kumpa adhabu unampa bila wewe kuwa na hasira, kumbuka lengo si kumuumiza au kumkomoa, lengo la adhabu ni kufunza, atambue kipi ni sahihi na kipi si sahihi, akue, na awe mtu mwema kadiri anavyokuwa, kwa njia ya kistaarabu na si kwa njia za kinyama.
Changamoto waliyonayo wazazi/walimu wachapaji wengi ni kwamba hawana muda wa kutuliza akili zao, wana hasira zinazosababishwa na mengi, wana msongo, wa haraka, hawana muda kutafakari athari za muda mrefu na pia hawana maarifa mbadala ya adhabu.
Tunawachapa watoto na wanafunzi kwa kuwa 'wamekosea' si ndio? kwani sisi watu wazima, wazazi na walimu hatukosei? Je nasi tuchapwe pia? Si tunakosea kila siku?
Dunia imebadilika sana, hivyo nasi tubadilike, tutumie akili zetu zaidi kuliko nguvu zetu.