Tulia ugangwe ,
Tumeona kwa uchache dini ya Kikristo iliyoletwa na Paulo miaka michache baada ya Nabii Isa au Yesu (a.s.) kuondoka, jinsi inavyohusiana kimsingi na dini hiyo ya wapagani katika imani ya mungu-mtu na ibada potofu wanazoifanyia miungu hiyo. Endelea...
Uhusiano kati ya mungu wa Ukristo na miungu ya upagani
Sambamba na imani hiyo ya watu wa mataifa au wapagani, ya kuamini miungu-watu (akina Zeu na Herme) wanayoiamini kuwa na desturi ya kujigeuza kuwa mfano wa wanadamu (kama tulivyoona katika makala iliyopita katika gazeti hili), maandiko ya Biblia tukufu yanafundisha pia kuwa, muasisi wa dini ya Kikristo, Bwana Paulo naye baadae aliihubiri miungu hiyo ya wapagani lakini kwa jina lingine. Uthibitisho wa hilo tunaupata kwenye mafundisho yake mwenyewe (Paulo) yafuatayo:
"Nakuandikia hayo nikitaraji kuja kwako hivi karibuni. Lakini nikikawia upate kujua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, iliyo Kanisa la Mungu aliye hai, nguzo na msingi wa kweli. Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaamniwa katika ulimwengu, akachukuliwa juu katika utukufu". (1 Timotheo 3:14-16)
"Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa Yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu, kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu." (Wafilipi 2:5-7)
Cha msingi anachofundisha Bwana Paulo hapo juu ni kwamba, hapo mwanzo Yesu (a.s.) alikuwa hana tofauti yoyote na Mungu, kwa maana kwamba alikuwa ni Mungu kamili! Baadae akaona kuna umuhimu pia awe mtumwa; kwa hiyo akaamua kuuvua Uungu wake na kuuvaa mwili akawa mwanadamu kamili japokuwa roho yake iliendelea kubaki kuwa Mungu!
Aidha, kwa lugha ya jumla anachotueleza Bwana Paulo hapo juu ni kwamba, kipindi fulani Yesu (s.a.) alikuwa Mungu kamili na kipindi kingine alijibadilisha akawa mwanadamu kamili japokuwa Uungu wake ukabaki nao rohoni! Kwa uchache, hivi ndivyo Bwana Paulo (muasisi wa Ukristo) afundishavyo kuhusu Mungu.
Hata hivyo, mafundisho hayo ya Bwana Paulo kwamba Yesu ni Mungu japokuwa ni mwanadamu kamili, yanapingwa vikali na mafundisho sahihi ya Bwana Yesu mwenyewe (a.s.) kama ifuatavyo:
"Na mmojawapo wa waandishi akafika, akawasikia wakisemezana naye, akatambua ya kuwa amewajibu vema, akamwuliza, katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza? Yesu akamjibu, Ya kwanza ndio hii, sikia Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndio hii. Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi. Yule mwandishi akamwambia, Hakika, Mwalimu umesema vema ya kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ile Yeye, na kumpenda yeye kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima za kuteketezwa na dhabihu zote pia. Naye Yesu, alipoona kwamba amejibu kwa busara, alimwambia, Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu. Wala hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea hapo". (Marko 12:28-34)
"Yesu akamwambia. Usinishike, kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu". (Yohana 20:17)
Hapa Bwana Yesu (a.s.) anawafundisha wanadamu wafahamu kwamba Mungu wake na wao ni mmoja tu na daima hakuna mwingine.
Sambamba na ukweli wa mafundisho yake hayo, ni jambo lilowazi kabisa pia kwamba, hakuna mahali popote ndani ya maandiko matakatifu ambamo Bwana Yesu (a.s.) katika maisha yake yote alimowahi kukaririwa akidai Uungu japo kwa kutania. Kinyume chake tunaona mara nyingi alikaririwa akifundisha wazi wazi kuwa Yeye ni mtu (tazama Yohana 8:40) na kusisitiza mara kwa mara kwamba yeye daima ni mwanadamu kamili (tazama Mathayo 11:19)
Aidha, kwa kuzingatia ukweli kwamba yeye (Yesu a.s.) ni mtu na ni mwanadamu kamili kama mwenyewe alivyofundisha hapo juu, itakumbukwa katika makala iliyopita katika gazeti hili tuliona jinsi Mungu (Yehova au Allah s.w.t.) anavyokataa kata-kata kwamba Yeye kamwe si mtu na wala si mwanadamu kwa kila hali (rejea Hesabu 23:19)
Kwa shuhuda hizo basi ni wazi kuwa Mungu aliyekuwa akimhubiri Bwana Paulo hapo ni ile ile miungu ya wapagani (akina Zeu na Herme). Kwa kutumia jina la "Yesu", hasa kwa kuzingatia desturi aliyomsifia kuwa nayo mungu wake huyo ya kujigeuza kuwa mfano wa wanadamu i sawa na imani ile ya watu wa mataifa au wapagani katika miungu yao hiyo (Zeu na Herme). Mafundisho kama hayo ya Bwana Paulo yamepelekea leo kuwababaisha wanadamu wamdhani Yesu kuwa ni Mungu wakati si kweli.
Sambamba na mafundisho yake hayo juu ya desturi hiyo ya miungu hiyo ya kipagani katika kutilia mkazo kwamba mungu wa dini yake ya Kikristo kwamba ana desturi ya kujibadilisha badilisha, Bwana Paulo alidiriki kudai kuwa mungu wake huyo aliyemwita "Yesu" pia wakati mwingine huwa anakuwa jabali! Uthibitisho wa dai lake hilo tunaupata katika kauli yake ifuatayo:
"Kwa maana ndugu zangu sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu, wote wakapita kati ya bahari, wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; wote wakala chakula kile kile cha roho; wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo". (1 Wakorintho 10:1-4)
Katika maelezo yake hayo juu, mwamba anaoukusudia hapo Bwana Paulo anaodai eti ulikuwa ni Kristo, yaani Yesu, ni lile jabali lililokuwa katika Horebu ambalo Nabii Musa (a.s.) kama Biblia ifundishavyo alilipiga kwa fimbo yake kisha maji yakatoka na watu wakapata kunywa (tazama Kutoka 17:6).
Kwa maelezo yake hayo, yaonyesha dhahiri Bwana Paulo anakiri kwamba Bwana Yesu (a.s.) aliwahi kutandikwa bakora na Nabii Musa (a.s.)! Ingawa Nabii Musa (a.s.) haonekani kabisa katika zama zake akiwa pamoja na Nabii Yesu (a.s).
Kwa ujumla, mafundisho hayo ya Bwana Paulo yanalenga wazi katika kuonyesha sifa kubwa ya Mungu anayemhubiri kwamba ni pamoja na kujibadilisha-badilisha katika maumbile tofauti! Ambapo desturi hiyo (ya kujibadilisha-badilisha) haipatikani isipokuwa katika imani ya wapagani juu ya miungu yao, ndivyo waiaminivyo kuwa ina sifa hiyo (kama tulivyoona hapo awali).
Na ni katika mafundisho kama hayo ya Paulo ndipo unapopatikana dhahiri shahiri uhusiano halisi wa imani ya mungu-mtu kati ya dini yake ya Kikristo na dini ya kipagani. Kwa mantiki hiyo, ni wazi kuwa asili ya Mungu anayeabudiwa na Wakristo inatokana na imani ya miungu-watu ya kipagani kama ile akina Zeu na Herme.
Paulo kutomtambua Mungu-Yehova
Katika shuhuda za Biblia tukufu zilizotangulia hapo juu, tumeona jinsi Paulo alivyosimama imara na kuihubiri miungu ya kipagani (kama akina Zeu na Herme) kwa jina la "Yesu". Aidha, akitilia mkazo msimamo wake huo (wa kufundisha miungu hiyo ya kipagani peke yake), Bwana Paulo alionyesha wazi kuwa hamtambui kabisa Mungu-Yehova. Uthibitisho wa hilo tunaupata katika kauli zake (Paulo) zifuatayo:
"Maana imani ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa, nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia, tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na mwokozi wetu, ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafisha watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema". (Tito 2:11-14)
"Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe niharimishwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili, ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake, ambao mababu ni wao, katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili. Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu mwenye kuhimidiwa milele. Amina." (Warumi 9:3-5).
Katika kuonyesha kwamba hamtambui kabisa Mungu-Yehova na kwamba amedhamiria kumhubiri peke yake mungu-Zeu na Herme kwa jina la "Yesu", Bwana Paulo hapa anadai kwamba mungu wake huyo aliyemwita "Yesu" ni mungu mkuu na ndiye mungu aliye juu ya mambo yote! Kwa maana kwamba kama kuna Mungu mwingine yoyote basi Mungu wake huyo ndiye zaidi (mkuu)!
Hata hivyo, lakusikitisha, wakati Bwana Paulo anawafundisha wanadamu kwamba mungu wake huyo aliyemwita "Yesu" kuwa ndiye mkuu, tayari Bwana Yesu mwenyewe alikwishafundisha kwamba Mungu-Yehova ndiye Mkuu kuliko yeye (Yesu a.s.) (tazama Yohana 14:28).
Hii yote ni kudhihirisha kuwa Mungu aliyemhubiri Paulo ni mungu yule yule mwenye asili ya miungu ya wapagani (kama akina Zeu na Herme) na kamwe siyo Mungu-Yehova ambaye ndiye Mungu wa Nabii Ibrahimu, Ismaili, Isaka, Yakobo, Yesu, Muhammad na Mitume na Manabii wengine wote (a.s.) aliowatuma duniani.