Kama kuna kitu cha kushangaza au kusikitisha ni jinsi gani ajali hii inavyoonyesha mawazo ya Watanzania yalivyo.
Nilitarajia kurasa hizi 27 zingezungumzia ulazima wa kuboresha barabara, kuimarisha hospitali zetu, kuhakikisha kuwa mafunzo ya usalama wa barabara na udereva yanafanyiwa umakini, lakini gumzo kubwa ni mambo ya kafara na hujuma kisa ni Mwakyembe!
Je wiki kadhaa zilizopita wakati washabiki wa Simba na karibu wachezaji wa Simba wapate ajali mbaya pale Morogoro, tungesema ni Yanga waliochimba mahandaki barabarani au kulegeza nati za gurudumu?
NI Ndugu zetu wangapi; Baba, Mama, Mjomba, Shangazi, Kaka, Dada, Shemeji, Wifi, Babu na Bibi, Rafiki hata Majirani ambao wamepoteza maisha kutokana na ajali za barabarani ambazo chimbuko kubwa ni 1. Ubovu wa Barabara, 2. Ujuvi wa madereva, 3. Magari mabovu, 4, Ufinyu wa huduma za Uokoaji, Tiba na Dharura na zaidi kuwa ni za viwango vya chini?
Tangu Salome Mbatia mpaka leo hii ya Mwakyembe, ni Watanzania wangapi ambao wamepoteza maisha kutokana na ajali za barabarani?
Je kama Taifa tumechukua hatua gani kulifanyia utatuzi tatizo hili sugu?
Siku mashabiki wa Simba walipopata ajali kule Morogoro, Mwenyekiti wa Simba Hassani Dalali alitoa wito kuitaka Serikali na Tanroads kufanya utafiti wa kina wa kinachosababisha ajali za barabarani Nanukuu kutoka Habari Leo
HabariLeo | Dalali ataka barabara ya Dodoma ichunguzwe
Dalali ataka barabara ya Dodoma ichunguzwe
Mwenyekiti wa Simba Hassan Dalali ameiomba Wizara ya Miundombinu kuifanyia ukaguzi barabara kuu ya Dodoma - Morogoro inayopitia katika Kijiji cha Chamale, Kata ya Magubike, wilayani Kilosa, kwa ajili ya kuweza kubaini vyanzo halisi vya ajali za mara kwa mara.
Dalali alitoa ushauri huo alipowatembelea majeruhi ambao ni mashabiki wa timu yake waliopata ajali usiku wa Aprili 26 katika kijiji hicho walipokuwa wakitoka kuishuhudia Simba ilipocheza na Polisi Dodoma.
"Ipo haja kwa serikali kuingilia kati ili kujua kwa nini eneo hilo linatokea ajali za mara kwa mara ili kunusuru maisha ya watu …huenda eneo hilo lina matatizo au vijana ndiyo wanaomwaga mafuta ya dizeli, " alisema Dalali.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa Simba, iwapo serikali kupitia wizara inayohusika kulikagua eneo hilo la barabara huenda ikatoa majibu sahihi ya kubaini iwapo lami iliyotumika ina kasoro ama kuna tatizo lingine litakalopaswa kuchukuliwa hatua za haraka.
Mashabiki kadhaa wa timu hiyo walinusurika kifo baada ya basi dogo walilokuwa wakisafiria kutoka Dodoma kuelekea Dar es Salaam, kuacha njia na kupinduka eneo la Chamale, Kijiji cha Magubike, wilayani Kilosa mkoani Morogoro.
Ajali hiyo ilitokea saa 5: 45 usiku katika eneo hilo baada ya siku mbili kupita wakati ilipotokea ajali mbaya ya basi mali ya Kampuni ya RS Investiment iliyosababisha kifo cha Mbunge wa zamani wa Jimbo la Biharamulo Magharibi (TLP), marehemu Phares Kabuye na watu wengine wawili na kujeruhi abiria 54.
Mchana wa siku hiyo, viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro akiwamo Mwenyekiti na Katibu wake walipata ajali katika eneo hilo na usiku wake ndipo mashabiki hao wa Simba walipatwa na mkasa huo. Mashabiki 12 walijeruhiwa katika ajali hiyo na kukimbizwa Hospitali ya Misheni ya Berega iliyopo wilayani humo.
Badala ya kuchukua fursa hii ya ajali iliyomkumba mtu maarufu kama Mwakyembe kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya ajali za Barabarani, tunabakia kubishana na hekaya za nani mchawi!
Inachosha!