"Kuna watu ni wanafiki Katiba siyo Msaafu, muda wowote inabadilishwa na siyo Rais wa kwanza kuongezewa muda, atake asitake alazimishwe haiwezekani kumuachia nafasi, naulizwa kila siku baada ya Magufuli nani anafuata mimi nasema anaongezewa muda"- Ally Kessy (CCM).
Spika Ndugai ajibu hivi
“Mheshimiwa Keissy ngoja twende uchaguzi mkuu, turudi, na mimi naamini sote tunarudi. Hilo ulishikie uwe nalo moyoni, tutarudi hapa [bungeni] salama, azimio hilo utakuja kulileta wewe Mzee Kessy na litapita kwa kishindo, atake asitake [Rais Magufuli] tutaongeza muda,” Job Ndugai
Return...
Haya ya Mh. Kessy ni upeo wa fikra zake kushindwa kutafakari hatari na uzito wa jambo kama hilo atakalo lipitishwe na Bunge.
Katiba ipo sasa litafanyika hilo kwa vigezo vipi?
Kuna rejea wakati Salmin Amour alipotaka kufanya kama hili naamini viongozi wetu wanajua CCM ilichukua hatua gani.
Katiba ya nchi si kitu cha kuchezewa na matukio ya nyakati kwani viongozi wanapita lakini taifa ni lenye kudumu na kuishi nje ya nyakati na misimu.
Kwa upande mwingine unaweza kusema haya ya kuingia ndani ya katiba na kukata kipande kikawekwa kingine ni matatizo ya Afrika kwa uchanga wake. Haya yote yanaingia katika mifano mingi ambayo Afrika imeshuhudia.
Afrika chaguzi zake zina shutuma nyingi za wizi wa kura, hila na udanganyifu.
Haya ni sehemu ya chaguzi zake achilia mbali matumizi ya vyombo vya dola kuiba kura na kuzuia baadhi ya wananchi wasipige kura kwa hofu ya kushindwa.
Afrika sanduku la kura limegeuka kuwa jinamizi la kutisha viongozi waliopo madarakani.
Sasa serikali inayoingia madarakani kwa mtindo huu itakuwa na uhalali upi?
Serikali za namna hii ni nyingi sana Afrika.
Ikiwa hii ndiyo hali iliyoko Afrika si tabu kuelewa fikra za wabunge wake zitakuwaje iwe hapa kwetu nchi jirani au mbali na sisi.
Katika mazingira kama haya haiwezi kuwa kitu cha ajabu kwa wabunge kuja na hoja ya kujiimarisha zaidi madarakani kwa kupitia njia zilizo kinyume na kitu kinachoitwa "common good," yaani kufanya yale yenye manufaa kwa wote.
Lakini ukiangalia historia ya dunia utakuta kuwa nchi nyingi zimepitia hali kama hii.
Imani ya wataalamu wa siasa ni kuwa hiki kipindi kitapita na iko siku Afrika haitakuwa kichekesho cha dunia.