Kanunue bond Bot ndio suluhisho kuu.. Inalipa zaidi.
[
https://tiob]
RIBA YA HATI FUNGANI ZA SERIKALI NA MAENDELEO SEKTA YA KIBENKI
Na: Jackson Rwekaza
Published: 13/March/2018, Mtanzania Newspaper
Hati fungani za serikali ni fursa nzuri ya uwekezaji hasa kwa wale wanaohitaji kuwekeza fedha na kupata faida bila kutumia nguvu nyingi au kuwekeza bila kupata hasara.
Mabenki ni miongoni mwa taasisi zinazowekeza mara kwa mara kwenye hati fungani za Serikali.
Taasisi nyingine zinazowekeza kwenye hati fungani za Serikali ni mashirika ya bima, mifuko ya pensheni, mifuko ya uwekezaji wa pamoja na makampuni makubwa.
Wananchi pia huwekeza katika hati fungani za Serikali lakini hii fursa hutumiwa na watu wachache sana kutokana na watu wengi kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa kutumia chanzo hiki cha utajiri.
Riba ya hati fungani za Serikali ni gharama kwa serikali, hivyo kushuka kwake ni habari njema kwa mtoaji. Lakini kwa wawekezaji kushuka kwa bei za hati fungani za Serikali kunapunguza faida.
Kwa mabenki, hati fungani za Serikali hasa za muda mfupi ni dhamana zenye ukwasi mkubwa na dhamana hii inatumika kiuwekezaji, yaani kama chanzo cha mapato lakini wakati mwingine inaweza kutumika kwa matumizi mengine kama vile kuweka rehani kwa ajili ya kukopea na pia ikatumika kama dhamana ya dharura wakati wa uhitaji mkubwa wa fedha tasilimu.
Hati fungani za Serikali huuzwa kupitia minada ambapo kila muwekezaji huwasilisha zabuni inayoonesha riba ambayo yuko tayari kulipa kulingana na mahitaji na uwezo wake. Maombi ya wawekezaji, hushindanishwa kufuatana na kiasi ambacho serikali imepanga kukopa kwa mnada husika. Wawekezaji wakiwa wengi na wakija wanahitaji kiasi kikubwa cha fedha kulingana na mahitaji ya kukopa ya Serikali riba za hati fungani za Serikali zitashuka na wakija wanunuzi wachache ushindani utakuwa mdogo na hatimaye Serikali itauza dhamana zake kwa riba kubwa.
Mabenki yakiwa na ukwasi wa kutosha baada ya kukopesha hupendelea kuwekeza katika hati fungani za Serikali za muda mfupi tofauti na taasisi nyingine kama vile mifuko ya pensheni ambayo hupendelea zaidi hati fungani za muda mrefu. Hii ni kwasababu mabenki yanatakiwa yawe na ukwasi ili kuwezesha watu walioweka amana zao wazipate kwa wakati wanapokuja kuzitoa kwa mhitaji yao. Mifuko ya pensheni hupendelea kuwekeza kwenye dhamana za muda mrefu kwasababu wateja wao huweka pesa wakitarajia kuzitoa baada ya kustaafu.
Mabenki yakiwekeza zaidi kwenye hati fungani za Serikali yanaweza kusababisha kushuka kwa riba. Kushuka kwa riba kunasababisha kushuka kwa mapato ya benki yatokanayo na riba hivyo faida za mabenki kupungua. Kushuka kwa riba kutasababisha mabenki kuamua kuwekeza kwenye fursa nyingine. Benki inaweza kutumia fursa ya kuwekeza kwa kukopesha benki nyingine kupitia masoko ya fedha baina ya mabenki.
Mabenki mengi kushiriki kwenye soko la dhamana za muda mfupi kwa lengo la kuwekeza kunaashiria ukwasi baina ya mabenki. Ukwasi kwa mabenki ni jambo jema kiuchumi ili mabenki yaweze kuwekeza kwa kukopesha kwenye miradi mbalimbali inayochochea maendeleo.
Pamoja na kwamba ushiriki wa mabenki kununua hati fungani za Serikali za muda mfupi kwa kiwango kikubwa kunaashiria ukwasi wa kutosha, pia kunaweza kuashiria kukosekana sehemu nyingine za kuwekeza mathalani mikopo. Kwa mfano, ikiwa mikopo mingi hailipiki, na kwa kawaida mikopo ni chanzo kikuu cha mapato ya mabenki, ili kuepuka hasara mabenki yatachagua kwenda kuwekeza kwenye dhamana za Serikali ili kuepuka hasara, hivyo kuchangia ushukaji wa riba.
Kwa hiyo kushuka na kupanda kwa bei ya dhamana za Serikali kunaweza kutazamwa kwa namna mbili. Namna ya kwanza ni kuwepo kwa ukwasi wa kutosha kwenye masoko lakini pia kukosekana kwa sehemu nyingine za kuwekeza zenye athari ndogo.
Bei za dhamana za serikali zinakuwa na athari pia kwa wawekezaji wengine. Kwa mfano mifuko ya pensheni inapowekeza kwenye dhamana za serikali inategemea kupata faida kubwa ili iweze kulipa wastaafu. Riba inaposhuka, faida pia hushuka na kuipunguzia taasisi ya aina hii uwezo wa kulipa pensheni nzuri zaidi kwa wanachama wake. Mwanachama anapokaribia kustaafu hujawa na matumaini makubwa ya kupata pensheni itakayomfurahisha, hivyo anapokuja kupewa pensheni ndogo huishia kukata tamaa.
Aidha bei ya dhamana za serikali huathiri bei ya dhamana nyingine. Kama vile bei za hisa na vipande vinavyotolewa na mifuko ya uwekezaji wa pamoja. Kupanda kwa bei ya dhamana za Serikali kutafanya wawekezaji wahamie kwenye dhamana za serikali, hivyo hisa kukosa ushindani. Aidha vipande vinavyotolewa na mifuko ya uwekezaji wa pamoja vinaweza kuwa na faida kubwa hivyo watu waliowekeza kwenye vipande wanapata faida. Pia watu waliowekeza katika mifuko ya pensheni kwa utaratibu wa hiari nao wanaweza kupata gawio kubwa kutokana na faida.
Kwa wakati mwingine bei za dhamana za Serikali zinaathiri riba ambazo mabenki yanatoza katika kukopesha wateja wake. Kwa mfano riba ya hati fungani za Serikali zikiwa chini, mabenki yatakopesha kwa riba ya chini kwa sababu ya ukwasi kwenye soko. Aidha kuna wakopaji wengine ambao hupendelea riba inayobadilika kuendana na riba ya hati fungani za Serikali za muda mfupi zinavyobadilika “floating rate”. Kwa mteja aliyekopa kwa riba inayobadilika, riba ya dhamana za serikali inaposhuka yeye hupata faida ya kushushiwa riba ya mkopo wake wakati wa marejesho.
Katika siku za hivi karibuni riba ya dhamana za Serikali ilishuka. Tunachotegemea kwenye uchumi ni mabenki kuwekeza kwenye kukopesha wateja wao hivyo shughuli za kiuchumi zitaongezeka. Aidha mabenki ambayo yalikuwa na ukosefu wa ukwasi yataweza kupata pesa kwenye masoko ya mabenki ya kukopeshana kwa gharama nafuu hatimaye yataweza kukopesha kwa faida na kutengeneza faida.
Kitu kinachotakiwa kufanyika ni kuendeleza kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili biashara nyingi zipate faida na kuwezesha ulipaji wa madeni kufanyika kwa wakati hatimaye kuwezesha mabenki kukopesha zaidi.
Aidha riba za mikopo zinatarajiwa kushuka hivyo kuwezesha kupungua kwa kiwango cha marejesho. Hii itasaidia kupunguza kiwango cha mikopo chechefu. Hatimaye Tanzania itashuhudia sekta ya mabenki imara na stahimilivu.
Kwa hiyo bei za hati fungani za Serikali ni suala nyeti na inaathari kubwa katika uchumi. Kupanda na kushuka kwake kunaweza kuashiria maendeleo mabaya kwenye uchumi au maendeleo mazuri kwenye uchumi kwa sababu ya ushindani huru katika kuinunua hivyo inaashiria hali halisi ya uchumi.
CONNECT WITH US
[
https://tiob]
[
https://tiob]
Follow
[
https://tiob]
[
https://tiob]
[
https://tiob]
[
https://tiob]
CONTACT US
Faykat Tower, 5th Floor, Plot No. 236,
P.O. Box 8182 Dar es salaam, Tanzania
Ally Hassan Mwinyi Road, Kinondoni,
Next to Airtel Head Office.
Tel: +255 22 2669091 / +255 22 2669092
Email:
info@tiob.or.tz
Website:
www.tiob.or.tz
QUICK LINKS
Join TIOB
E-Learning
E-Library
Examination Results
E-Books
[emoji2398] 2019. Tanzania Institute of Bankers, All Rights Reserved.