Wanaofanya mambo na kunena kwa unafiki watakupinga lakini walio wakweli wa nafsi zao, watakiri kwa uwazi kuwa uliyoyanena ni ukweli mtupu 100%.
Kuwa mzalendo wa kweli kwa Taifa, ni kutenda yale ambayo unatakiwa kutenda na Taifa, na kuyaacha mapenzi yako binafsi. Hii ndiyo sababu ya kumuapisha kiongpzi na kumtaka atamke chini ya kiapo kuwa atafuata katiba na sheria, na siyo matakwa yake.
Tujiulize - katika utendaji wake wote wa kazi, Rais wetu amekuwa anafuata na kulinda katiba, sheria na kanuni?
Rais na kiongozi mwingine yeyote, na hata sisi raia, tunayotakiwa kuyatenda, tunaelekezwa na katiba, sheria na kanuni. Unapotenda ambayo katiba, sheria na kanuni zinakuzuia, wewe kamwe huwezi kuwa mzalendo wa kweli bali unakuwa adui wa Taifa hata kama kila mahali neno uzalendo utalitamka.
Ni bahati sana kwake Rais ameongoza nyakati hizi, Taifa hili na aina ya watu kama sisi. Nchi nyingine, au hata watu wa kizazi kingine, isingewezekana. Ni kosa lisilo na msamaha kwa kiongozi kukiuka sheria na katiba kwa uwazi, tena katiba uliyoapa kuilinda, halafu ukaendelea kuwa kiongozi wa Taifa.
Kuwa kiongozi hakubadilishi ubinadamu wako, na wala hakukufanyi uwe binadamu kuwazidi wengine. Wewe ni binadamu yule yule, uliyepewa majukumu fulani kwa wakati fulani kwa kuzingatia maelekezo ya katiba. Wala kuwa kiongozi, iwe kwa kuchaguliwa au kuteuliwa, hakukuongezei akili wala ujuzi ambao haukuwa nao kabla ya kuwa kiongozi. Uwezo na akili uliyoongezewa ni uwingi wa watu wanaokuzunguka. Wewe kazi yako ni kutengeneza mazingira wezeshi ya watu wote kuweza kutumia ujuzi, uzoefu na akili zao katika kulipeleka Taifa mbele.
Kiongozi unatakiwa utende haki kwa kuzingatia katiba hata kama binafsi hupendi unayoelekezwa na katiba.