Alipoingia madarakani alijitambulisha kama ni mcha Mungu. Alikwenda katika madhehebu mbali mbali kusali na kote huko akiomba aombewe ili aongoze kwa haki kwani alisema "kazi hii ni ngumu" Mara nyingi amesikika akisema "msema kweli ni mpenzi wa Mungu"
Kutokana na wito huo watu wa Mungu tuliingia katika maombi ili kumuombea awe na hekima kama alivyoomba mfalme Suleimani ili atawale na kuongoza kwa hekima kubwa na kwa haki. Katika madhehebu mbali mbali ikiwa ni pamoja na hili ninalosali mimi huwa kuna kipengele cha kuiombea serikali na hasa rais katika kila ibada zetu za Jumapili. Sasa cha ajabu, kadiri tunavyoomba ndiyo mambo yanakwenda sivyo ndivyo. Sasa kila akifungua mdomo badala ya kuhubiri amani, upendo, umoja, uvumilivu, upatanisho yeye anahubiri ubabe, utengano, visasi, kukomoana na kwenda kinyume kabisa na katiba na sheria za vyama vya siasa nchini. Sasa mimi sielewi Mungu anakataa maombi yetu au hatuombi vizuri kiasi kwamba inakuwa kinyume chake? Nafikiri wakati umefika sasa wa yeye kujiombea yeye mwenyewe na kutuombea sisi labda tutaona tofauti. Matamshi yake kwenye ziara hii ya visiwani yametutisha, kutushangaza wengi na kutuacha midomo wazi. Jamani tumekosea wapi ili tujirekebishe? Maana huko tuendako naona kama itakuwa ni zaidi ya kupatwa kwa jua. Mungu tusaidie!
Raha na furaha katika familia ni pale baba anapoonekana na kuongea anawaacha katika amani, matumaini na furaha lakini sio kujawa hofu na mashaka kwamba sijui leo itakuwaje? Je akiongea na kuondoka tutabaki na furaha, amani na matumaini au tutabaki na vilio, manung'uniko, mshangao na hofu?
Kuwa baba ni zaidi ya kuwa mwanaume!