*ANGA LA WASHENZI -- 16*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA...
Alisogelea dirisha la sebule, akachungulia ndani. Hakumuona Jona, ila akamuona mwanaume aliyeketishwa kwenye kiti na kufungwa kamba. Hakumtambua mwanaume huyo kwani alikuwa amezibwa na kinyago usoni.
Lakini kinyago hicho kikamgutua. Kilikuwa ni cheusi chenye umbo la fuvu la binadamu. Alikumbuka Miranda aliwahi kumwambia kukihusu. Ya kwamba mwanaume yule aliyemvamia kuchukua kamera, alikuwa amekivaa.
Ina maana ndo’ huyu? Akajiuliza. Anafanya nini hapa akiwa amefungwa kamba?
ENDELEA...
Sasa kidogo Kinoo akaanza kuelewa kwanini Miranda alimwambia 'mchoraji' yule, ambaye ni Jona, hakuwa mchoraji tu, ni mtu mwenye ngebe za mafunzo na ujuzi.
Hakutaka kuingia ndani haraka bali ausome kwanza mchezo, Jona yupo wapi? Na anamfanya nini huyu mtu aliyeonekana dhahiri kuwa mateka?
Akatulia kungoja. Kwa dakika kama nne pasipo kuona wala kusikia jambo la kulituhumu.
Alikuja kushtuka aliposikia chuma cha baridi kisogoni mwake, na sauti ya Jona ikamuamuru:
"Tulia hivyo hivyo! - mikono juu!"
Akatii amri. Kwa uzoefu wake alishajua ni mdomo wa bunduki ndiyo ambao upo kisogoni. Ila alikuwa mkaidi kuwa mpole kirahisi.
Akaanza kufikiri ni njia gani inaweza kumuokoa akaushika mchezo.
Ila kama vile alishtukiwa, akaonywa:
"Ukijitia mjanja, nakutoboa kichwa!"
Akatulia tuli, macho yake yakiangaza angaza kana kwamba mtu mwenye haraka atafutaye ufunguo wa gari.
"Haya ongoza ndani!" Jona akaamuru. Pasipo kubisha, Kinoo akaanza kuchukua hatua kusogelea mlangoni.
Kichwani mwake alitafakari ilikuwaje akadakwa kirahisi hivyo? Alijiona mjinga na mzembe pia.
Endapo asipofanikisha hili, Miranda ataenda kumlaumu sana. Kumtusi na kumshusha vyeo.
Hivyo lazima apate namna.
Alipokaribia mlangoni, upesi akakisogeza kichwa chake kukwepa mdomo wa bunduki kabla Jona hajafanya lolote.
Kisha akautwaa mkono wa Jona na kujaribu kuupoka silaha.
Wakavutana huku na huko nguvu zikitumika. Kinoo akamzidi nguvu Jona, akaiteka silaha akimsukumizia kando mpinzani wake.
Ila kabla hajafanya kitu na bunduki hiyo, Jona akautuma mguu wake, haraka sana, kuutengua mkono wa kulia wa Kinoo uliobebelea bunduki.
Bunduki ikaangukia chini!
Wote wakaitazama kwa macho ya ashki ila wasithubutu kuinamisha migongo yao kwa kumhofia mwenziwe.
Kuinama kunamaanisha kumpa fursa adui akutende atakavyo, hilo kosa hakuna aliyetaka kulifanya.
Wakaachana na bunduki wakitazamana kama mafahari ya ng'ombe ndani ya zizi. Walikunja ngumi wakitegeana.
"Niliwapa onyo, naona hamjataka kulisikia!" Alisema Jona akimkazia macho Kinoo.
"Wewe si wa kutupa sisi onyo. Bado huna hadhi hiyo," Kinoo akajibu kwa dharau kabla hajaguna.
Jona akatabasamu asitie neno. Alipanga matendo yake yaongee sasa na si sauti ya mdomoni.
Kimwili alikuwa mdogo ukimlinganisha na Kinoo, na alijua hilo lina faida na hasaraze. Endapo akiingia mikononi mwa Kinoo basi itamuwia vigumu kuchoropoka.
Faidaye, Kinoo atakuwa mzito kufanya mashanbulizi. Miili mikubwa huchukua hatua kubwa kushurutisha viungo.
Basi akajipanga vema kutumia hiyo faida.
Akachokoza pambano kwa kurusha ngumi mbili za haraka, Kinoo akazikwepa kisha akatuma ngumi yake nzito. Jona akayeya! Ikapita.
Akatuma nyingine na nyingine, Jona akazikwepa kama mchezo wa rede.
Kwa nusu dakika, akausoma mchezo, akapata alichokuwa anakitaka.
Kinoo hakuwa mzuri kwenye kujilinda, alikuwa mzito kukwepa, na alikuwa akiziacha mbavu zake wazi mara kwa mara.
Bila shaka alikuwa anategemea zaidi kushambulia kuliko kujilinda.
Jona akaanza kucheza na mbavu za mwanaume huyo, akilenga kumtepetesha na kumminya uwezo wa kuhema.
Kinoo akarusha ngumi zake kwa mfululizo, Jona akawa anakwepa kisha anakita mbavu za Kinoo kwa ngumi za upesi.
Kila alipopata mwanya, basi akafyatua ngumi tatu ama nne!
Ikafikia mahala Kinoo akachoka kwani alikuwa anatumia nguvu nyingi kurusha ngumi zilizokuwa zinaenda patupu. Ukijumlisha na ngumi alizokuwa antekenywa mbavuni, akashindwa kufua dafu.
Alikuwa hoi bin taaban.
Alikuwa anatamani kuhema kwanguvu, lakini mbavu haizikuruhusu. Ni kama vile alipewa pumu.
Ni wazi alikuwa ameshindwa, ila hakutaka kuingia kwenye mikono ya adui, hivyo basi akatoroka kwa kukimbia.
Aliruka ukuta akazama ndani ya gari lake na kuhepa kwa kasi!
Jona alihofia kufyatua risasi kutoshtua majirani. Hakutaka kuwapa hofu wala makisio na mahisio yoyote juu yake na mambo yake.
Basi akamwacha Kinoo aende. Huko akafikishe habari aliyokumbana nayo.
Yeye akarudi zake ndani na kumtazama Bigo. Akampuuzia na kuendelea na mambo yake. Akaoga na kisha akajipeleka chumbani alipojilaza akiendelea kunywa.
Bigo aliachwa palepale kwenye kiti.
***
Kadiri usiku ulivyokuwa unasonga ndivyo na tafrija ilivyokuwa inanoga.
Sasa ilikuwa ni saa tano inayoelekea saa sita usiku na muziki laini ulikuwa unaburuza eneo wageni wakiserebuka.
Ndani ya eneo hili lililokuwa limesheheni taa kali zilizogeuza usiku kuwa mchana, kulikuwa kuna walinzi kedekede wakiwalinda wanaume na wanawake waliokuwa humo tafrijani.
Watu hawa walikuwa ni 'vibopa', watu wazito wenye nyadhfa zao serikalini ama mahala pengine nyeti kiuchumi.
Karibia wanaume wote walikuwa wamevalia suti, zikipishana tu rangi. Wanawake 'wakila' magauni ya kupendeza na michuchumio ya haja.
Nyuso za wanawake hawa zilikuwa zimerembwa kwa 'make-up' zilizofiti usoni. Waling'aa kama malaika, ila hawagusa kwa mwanamke Miranda.
Alikuwa amependeza haswa. Pia na kujiamini kwake pamoja na kujua kwenda na muda, kulimfanya avutie zaidi.
Kila muziki ulipowekwa alijua kwenda na mapigo. Alifanya watu wamtazame na pia kumwongelea wasijue mwanamke huyu alikuwapo kazini, na lengo lake lilikuwa kumtia kimyani mheshimiwa fulani.
Muziki ulikata, wakarejea kwenye viti vyao. Miranda alikuwa ameketi na BC meza moja. Meza iliyokuwa imechafuliwa kwa vinywaji.
Meza yao ilikuwa inatazamana, kwa umbali kidogo, na meza aliyokuwa ameketi mheshimiwa Boka, waziri wa Afya. Mwanaume mnene mweusi mwenye kitambi kama kiroba cha mihogo.
Alikuwa amevalia suti na tai ya bluu. Mezani alikuwa pamoja na mwanamke fulani mnene, pasi shaka mkewe, pia na kijana mmoja wa kiume mwenye kadirio la miaka ishirini na saba - nane - tisa.
"You did great!" (Umefanya vizuri!) BC alisema akitazama meza ya mheshimiwa Boka. "He was really impressed, now we've to figure the way out to reach him." (Aliguswa sana, sasa tunatakiwa tutafute njia ya kumpata.)
"The problem is his wife," (shida ni mkewe,) alisema Miranda akikunja shingo kutazama penye lengo. "She's very close to him as if she knows our intention. But I will get the way out!" (Amemganda sana kana kwamba anajua lengo letu. Lakini nitapata namna!)
Miranda aliposema tu hivyo, akanyanyuka akijifanya anatengenezea nguo yake vizuri. Mheshimiwa akamtazama, naye akamtazama kukutanisha macho.
Akatabasamu na kutazama kiaibu. Mheshimiwa naye akatabasamu kujibu.
Miranda akaketi. Sasa akajua dhahiri mheshimiwa Boka atakuwa anatazama tazama mezani kwake baada ya hilo tukio.
Basi hakujiweka mbali. Akawa anampa mheshimiwa macho na kajitabasamu.
"The bird's fallen into the trap!" (Ndege ameangukia mtegoni!) Akasema Miranda kwa tabasamu.
"Now take it!" (Sasa mchukue!) BC akashadadia.
Punde Miranda akanyanyuka, akamtazama mheshimiwa, kisha akayaelekezea macho yake upande wa maliwatoni.
Alafu akaelekea huko akitembea kwa madaha ya walimbwende jukwaani. Mheshimiwa akamsindikiza kwa macho ya ukware.
Naye, isichukue muda, akanyanyuka aende huko huko maliwatoni. Basi wakakutana na Miranda kwenye korido.
Mwanamke huyo alikuwa anahangaika na zipu ya gauni huko mgongoni, akijinasibu anahangaika kuifunga.
"Naweza nikakusaidia?" Mheshimiwa Boka akapaza sauti akitabasamu.
'Naona umejileta mwenyewe boya wewe!' Miranda akasema kifuani. Aligeuza uso wake kutazama, akakutana uso kwa uso na waziri. Akaigiza aibu.
"Hapana, ahsante mheshimiwa," akajibu akitabasamu.
"Aaaah bwana mrembo kwanini upate shida hivyo na mie nipo?"
Miranda hakusema kitu. Alitabasamu tu akaendelea kuhangaika na zipu yake. Basi mheshimiwa akaamua kujisogeza, alichukulia ukimya kama 'ndio', akadaka zipu ya Miranda na kuipandisha juu pasi na tabu.
"Ahsante sana, mheshimiwa, na samahani kwa usumbufu!"
"Usijali, mrembo. Unaitwa nani wewe?"
"Flaviana," Miranda akajibu akitazama chini.
"Oooh jina zuri kweli!"
"Ahsante."
Mheshimiwa akatazama mazingira, akajiona wapo wenyewe. Ila alijua fika hawatadumu kwa muda mrefu hapo. Aidha mkewe aje, ama watu wengine waliobanwa na haja, basi akaamua afanye mambo upesi.
"Sasa mrembo nataka tupate nafasi ya kuongea vizuri na wewe. Vipi sasa nitakupataje? - una simu?"
"Ndio ninayo."
"Sawa sawa!" Mheshimiwa akajipekua mfukoni, akatoa kadi ya biashara na kumkabidhi Miranda.
"Utan'chek basi, sawa?"
Miranda akatikisa kichwa. "Sawa, mheshimiwa, n'tajitahidi."
Mheshimiwa akatabasamu na kujilamba lips, akatoka maeneo ya maliwato na kurudi kwenye meza yake.
Baadae kidogo napo Miranda akarudi zake kukutana na BC. Akamwonyeshea kadi aliyopewa na mheshimiwa.
"That's a very big step!" (Hiyo ni hatua kubwa sana!) BC akasema akimpongeza Miranda kwa kumpa mkono. "We have already put him in our store." (Tayari tumeshamtia kwenye ghala.)
Sasa wakanywa kwa furaha wakiendelea kupanga na kusuka mipango yao.
Walikuwa na matumaini makubwa ya kumtia mikononi mheshimiwa Boka, na lengo lao kuu ni kumtumia kiongozi huyo wa kitengo cha Afya kusafirisha mizigo yao kwa kutumia kibali chake.
Huyu kwake alikuwa na faida kubwa kuliko mheshimiwa Eliakimu kwani yeye anahusika moja kwa moja na mambo ya madawa.
Lakini pia gharama yake itakuwa ndogo ama hamna kabisa kwasababu ya kumtumia Miranda kama chambo.
Wakiwa wanelekea ukingoni wa tafrija na sasa wakiwa wanajiandaa kuondoka zao,kwa amani kabisa maana hawajaupoteza usiku, mara kwa mbele yao wanamuona mke wa Mheshimiwa Boka akija.
Kabla hawajafanya kitu, mwanamke huyo alikuwa mbele yao akishikilia kiuno.
*MKE WA MHESHIMIWA ANATAKA NINI?*
*MIRANDA ATAFANIKIWA KUMRUBUNI MHESHIMIWA?*
*VIPI KUHUSU KINOO NA BIGO?*
USIKOSE SEHEMU IJAYO.
*Simulizi za series*