*ANGA LA WASHENZI – 19*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
“Ni kweli kabisa!” kisha akauliza: “Na vipi Brokoli? – alichukuliaje hii taarifa?”
Mudy akapandisha mabega juu.
“Sijui! Ila nakumbuka walikaa vikao viwili kama si vitatu mfululizo. Hatukuambiwa wanaongelea nini. Wala hatukupashwa habari kama kuna mabadiliko ama mazingatio yoyote kutokana na vikao hivyo!”
ENDELEA…
Kinoo akaguna kisha akauliza:
“Unajua wapi Brokoli anaishi?”
“Yah! Najua,” Mudy akajibu akitikisa kichwa.
“Na ulishawahi kuiftuatilia hiyo kampuni ya umeme wa jua?”
“Hapana. Sikufanya hilo kwa kutegemea polisi watalivalia njuga.”
“Sawa, na vipi kama hili jambo likabuma tena huko polisi, upo radhi kwenda umbali gani kutafuta haki ya Bite?”
Kidogo Mudy akasita.
“Una maanisha nini?”
“Unajua Mudy, si kila muda mambo yanaenda kama vile tunavyotarajia ama tunavyotaka. Nadhani uliona namna polisi walivyokuangusha ulivyowapelekea hili jambo. Sasa mimi nataka kujua unaweza kwenda kilomita ngapi kutafuta haki ya Bite?”
“Kadiri ya uwezo wangu.”
“Ahsante sana, hicho ndicho nilikuwa nataka. Njia hii inaweza ikawa ngumu na ndefu, inabidi tujiandae. Aidha kupita njia kuu ama nyinginezo ilimradi haki ipatikane.”
Kinoo akasafisha kwanza koo, akaendelea:
“Kikubwa ninachohitaji toka kwao ni taarifa tu, hayo mengine mimi nitayasimamia. Nitahitaji taarifa mbalimbali toka ofisini mwenu kama hutojali, yote kwa ajili ya Bite.”
“Nitajitahidi kadiri ninavyoweza.”
Wakapeana mikono. Kinoo akaaga.
“Ina maana mgeni unaondoka pasipo kupata chochote kitu?”
“Nashukuru sana, usijali. Leo si mwisho wa dunia. Anyway, unaishi mwenyewe?”
“Yah! Nipo mwenyewe.”
“Nyumba yote hii?”
Mudy akatabasamu. “Ndio, nipo mwenyewe.”
“Aisee!” Kinoo akatahamaki akiangaza huku na huko. Akapandisha mabega yake na kupinda mdomo.
“Haya mzee. Ningependa unipatie hizi nyaraka zako nikajaribu kufuatilia baadhi ya mambo. Pengine naweza nikaibuka na jambo.”
Mudy akamkabidhi.
“Kuwa makini, bado zinahitajika na ni muhimu ofisini.”
Kinoo akaitikia kabla hajaenda zake. Cha kwanza alichokifanya ni kumtafuta na kukutana na Miranda. Alikuwa yupo nyumbani kwake akijipatia kinywaji laini na kutazama televisheni. Alikuwa amevalia bukta ya timberland na blauzi nyeusi.
Akamweleza yale yote aliyoyapata huko kwa Mudy.
“Umefanya kazi nzuri!” Miranda akampongeza akipitisha pitisha macho yake kwenye nyaraka alizokuja nazo Kinoo.
“Lakini … Kinoo, kama vile naijua hii kampuni.”
“Serious?”
“Yah! Serious.”
“Ipo wapi?”
“Kama sijakosea, nilishawahi kuiona ikitangazwa kwenye TV. Tena si zamani, jana tu! … ngoja!” Miranda akanyaka rimoti na kubadili alichokuwa anakitazama toka kwenye movie mpaka chaneli ya kawaida.
“Bila shaka niliona hilo tangazo hapa.”
Alipoweka hiyo chaneli, wakaendelea na maongezi mengine. Wakagusia swala la picha ya Bite iliyopo kwa Jona.
“Nimeona ni vema nikaonana naye binafsi,” alisema Bite akikuna kichwa. “Nadhani nikimwelezea vizuri anaweza akanielewa. Hata kama asiponipa hiyo picha basi anipe wasaa mdogo wa kuitazama.”
“Unadhani atakukubalia?” Kinoo akauliza.
“Hayo yote ni matokeo: kunikubalia ama kunikatalia. Ila angalau nimejaribu. Lakini najua sitashindwa.”
Kinoo akaguna.
“Labda … sijui.”
“Kuna utofauti kati yangu na wewe,” Miranda akasema akimtazama Kinoo. “Tofauti moja kubwa mimi ni mwanamke na wewe ni mwanaume.”
Mara simu ya Miranda ikanguruma na kukatisha maongezi. Miranda akaitazama kujua ni nani kabla hajaiweka sikioni. Alikuwa ni waziri wa michezo; Mheshimiwa Eliakimu Mtaja.
“Tunaweza tukaonana, binti?” sauti ya Eliakimu iliuliza.
“Muda gani mheshimiwa?”
“Kesho majira ya jioni hapa nyumbani kwangu.”
“Sawa.”
Simu ikakata. Lakini ilimkumbusha jambo, kuwasiliana na bwana Boka, waziri wa Afya. Alienda chumbani kwake akarejea na kadi ya biashara aliyopewa na mwanaume huyo, akapiga namba iliyokuwa imeanishwa.
Bahati haikuwa kwake, simu haikupokelewa. Alipiga mara tatu kabla hajaamua kusitisha zoezi hilo.
***
“Kesho atakuja,” alisema bwana Eliakimu akimwambia Nade. Wote walikuwa sebuleni peke yao. Sauti ya televisheni ilikuwa inanguruma kwa mbali ikikosa shabiki wa kuitazama.
Eliakimu alikuwa amevalia suti ya traki ya michezo rangi ya bluu, Nade akiwa amejivalia suruali nyeusi ya kitambaa iliyoendana na koti lake fupi jeusi lenye kola rangi ya pinki.
“Nadhani mipango yetu imeenda kama tulivyotarajia,” alisema bwana Eliakimu. Nade akatikisa kichwa.
“Ndiyo, mkuu. Lakini kuna kajitatizo kadogo kametokea.”
“Wapi huko?”
“Ni kumhusu Maxwell Ndoja. Ameapa kutoshirikiana nasi tena. Amesema inatosha kwa yale yote tuliyoyafanya. Kwa sasa anataka kufungua ukurasa mpya.”
“Ukurasa mpya! Bloody fool!” bwana Eliakimu alifoka. “Anamaanisha nini kusema inatosha?”
Nade akapandisha mabega yake juu.
“Tangu lini pesa ikatosha?” Aliuliza Eliakimu. “Maxwell anataka kunipanda kichwani sasa. inabidi ajue hichi ni kitabu, hakuna ukurasa mpya kama haupo wa zamani, na ukitoa karatasi moja kwenye riwaya basi riwaya nzima inapoteza maana.”
Aliposema hayo akaulaza mgongo wake kwenye kiti akizama fikirani. Kwa dakika kama moja kukawa kimya kabla Nade hajamuuliza:
“Kwahiyo tunafanya nini, mkuu?”
Bwana Eliakimu akanyaka simu yake, akatafuta jina la Max, akaliita. Baada ya muda mchache ikapokelewa.
“Max, tunaweza tukaonana?” bwana Eliakimu aliuliza. Mzee huyu huwa haongei na mtu kwenye simu kuhusu mambo yake. Kuficha taarifa zake huwa anamwomba mtu wake wakutane. Na hupendelea zaidi nyumba yake kama mahali pa makutano.
“Hapana, hatuwezi kukutana,” ikajibu sauti ndani ya simu.
“Kwanini?”
“Kwasababu sina tena sababu ya kukutana na wewe mheshimiwa. Nadhani kibaraka wako ameshakwambia.”
“Max!”
Simu ikakata. Bwana Eliakimu akaitazama kana kwamba haamini.
“Amekata!” akasema akimtazama Nade. “Hivi huyu ananijua ama ananisikia?”
Akashusha pumzi ndefu … akakuna kidevu … akakuna kichwa.
“Hatuwezi tukamwacha huyu mtu hai,” akasema Bwana Eliakimu. “Anajua siri zetu nyingi mno. Hawezi akatoka tu kienyeji namna hii. Tutapataje uhakiki wa taarifa zetu kwake?”
“Hilo ndiyo jambo kubwa. Siri ziko mashakani sasa. hatuwezi jua nini kimemsukuma akajitoa kwenye duara.”
“Kwanini hukummaliza?”
“Nisingeweza kummaliza pasipo idhini yako.”
Eliakimu akanyanyuka akiweka mikono yake nyuma ya mgongo.
“Hakikisha kesho unammaliza huyu punguani. Usibakize ushahidi wowote nyuma!” alisema bwana Eliakimu kwa macho ya kumaanisha.
“Sawa, mkuu. Nitajitahidi,” Nade akapokea kauli.
Eliakimu akaenda zake chumbani. Alikuwa amekunja uso akibinua mdomo.
***
“Kwanini ulimuua Fakiri?” Jona alimuuliza Bigo aliyekuwa hapo kitini kwa masaa ya kutosha sasa. Bigo hakuwa amekula wala kunywa chochote. Tangu alipofungiwa kwenye kiti hakuwa amesogea wala kwenda popote.
Kuepusha asije akapiga makelele na kuzua tafrani, Jona huwa anamfunga mdomo pale anapotaka kulala ama kuondoka.
Bigo alitabasamu akimtazama Jona kwa kebehi.
“Sijui nini unaongelea,” akajibu kisha akalaza kichwa chake kutazama chini.
“Bigo, unapenda kuhangaika na kuteseka namna hii?” Jona aliuliza. “Mimi sina shida na wewe, najua wewe ni kibaraka tu unayetumwa. Mimi nina shida na bosi wako. Na shida yangu ni kujua kwanini anataka kuniua. Kwanini mnataka kuniua?”
Bigo akatabasamu.
“Ngoja nikwambie kitu kimoja, msanii. Sisi huwa hatumfuati wala kusumbuka na mtu asiye na faida kwetu, tunamfuata yule aliye na chetu, yule ambaye ana kitu tunachokitaka.”
“Mimi nina kipi chenu?”
Bigo akatikisa kichwa kichovu.
“Sina haja ya kukwambia, utakuja kujua mwenyewe. Kwa sasa mimi ni wa kufa tu, aidha nifie kwako ama kwa mkuu wangu. Najua hataniacha hai. Kwahiyo sina cha kupoteza, fanya upendacho.”
“Sina haja ya kukuua. Nipe taarifa ninazozitaka.”
“Alafu?”
“Nitakuacha uwe huru.”
Bigo akajaribu kucheka, ila zoezi likashindikana. Hakukuwa na ushirikiano toka tumboni.
“Huru? … siwezi kuwa huru kamwe maisha yangu yote.”
“Kwanini unasema hivyo?”
“Kwasababu najua. Njia pekee ya mimi kuwa huru ni kifo, la hasha sipo huru kabisa. Kwahiyo kama unataka kuniweka huru, inabidi uniue.”
“Sina haja ya kukuua, Bigo.”
“Basi mimi mwenyewe nitajiweka huru.”
“Kivipi? – huwezi kujiua hapo.”
Katika hali ya kushangaza, Bigo akaanza kuvuja damu nyingi mdomoni. Jona akashangazwa sana na hilo tukio. Alimkagua Bigo na macho yake lakini hakuona kama ana mushkeli popote pale.
Mbele ya macho yake, Bigo akalegeza kichwa, akakata pumzi.
Muda mfupi mbele, bado Jona akiwa ameduwaa, ulimi ukatoka mdomoni mwa Bigo na kudondokea chini!
Bigo alikuwa ameunyofoa ulimi wake kwa kutumia meno!
MANENO YAKE ALIYOMWAMBIA JONA YALIKUWA YANAMAANISHA NINI?
NADE ATAFANIKIWA KUMMALIZA MAX ALIYEAMUA KUSILIMU? KWANINI MAX KASILIMU?
KAMA MAX ANAFANYWA HIVI NINI KITATUKIA ENDAPO ELIAKIMU AKIGUNDUA BC NA MIRANDA WANA MPANGO WA KANDO?
KINOO NA MIRANDA WATAFANIKIWA?
Usikose sehemu ijayo.
Sent from my SM-J110F using
JamiiForums mobile app