*ANGA LA WASHENZI II ---- 77*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Alipomaliza kusema hayo, wakahisi boti inapepesuka. Wakatazamana pasipo kusema jambo. Pengine wakahisi ni pepo ama maji ya bahari. Ila hapana, boti ikapepesuka zaidi na zaidi! Mmoja akalazimika kwenda kutazama.
Ila alipoenda hakurejea ndani ya muda. Mwenzake, yule aliyekuwa karibu na usukani, akapata shaka. Kabla hajaenda kutazama huko nje, Wales akamsimamisha na kumwambia, “Be careful.”
ENDELEA
Mwanaume yule hakujali sana, akaenda zake huko nje na kumfanya Wales akae tenge kuskiza nini kitakachotokea. Alitamani kwenda lakini majeraha aliyonayo yasingemruhusu kufanya hivyo. Alitega sikio pasi na kusikia jambo. Ikapita dakika moja, akaamua kuita.
Kimya.
Hapa akapata sababu ya kuwa na shaka. Akajikongoja kusimama aende huko nje. Mkononi alikuwa na bunduki ya kumlinda dhidi ya shambulizi. Kufika huko nje hakuona mtu! Akastaajabu. Kugeuka akajikuta amekitwa nyuma ya shingo, akadondoka chini kuzirai! Hakupata hata wasaa wa kumwona aliyemshambulia.
Alikuwa ni Miranda.
“Mpo sawa?” mwanamke huyo akawauliza wale makomandoo waliokuwako ndani wakiwa wamefungwa. Akawafungulia toka kwenye kamba kuwaweka huru.
“Wewe ni nani?” komandoo mmoja akauliza.
“Msijali, mtanijua. Siko mwenyewe.”
Baada ya muda mfupi, Lee naye akiwa ametokea upande wa pili wa boti, akajiri akiwa amelowana chepechepe kama ilivyokuwa kwa Miranda. Watu hawa ndiyo walikuwa wakiwavutia wale watu kwenye maji na kuwamaliza. Naye akajitambulisha kwa jina tu.
“Nanyi mlikuwapo kwenye ndege?” akauliza Komandoo.
“Ndio, tulikuwamo pamoja kwenye ndege kabla ya kuanguka,” akajibu Miranda.
“Vipi kuhusu mheshimiwa? Yupo wapi?” akauliza Komandoo.
Miranda akanywesha sura yake akisema, “Bahati mbaya alifariki safarini.”
“Vipi mwili wake? - upo wapi?”
“Msijali, upo. Utakuja hapa muda si mrefu bila shaka.”
Makomandoo wakatazamana na mmoja kuuliza, “Utakujaje na umesema amefariki?”
“Kuna mtu atauleta,” akajibu Miranda na kuongezea, “Kuna mwenzetu yupo huko nje. Yeye atakuja nao.”
“Anafanya nini huko?” Komandoo akaulizia.
“Anamalizia kazi kabla hatujandoka,” akasema Lee.
Lakini ilikuwa inaleta mantiki kwa Jona kuwapo huko nje? Pengine waweza kuona hii ilikuwa ni fursa adhimu kwake kujiondokea pamoja na wenzake baada ya kushikilia boti hii, ila kinyume na hapo yupo kule kisiwani! Msituni!
Atapambana na wanaume wale sita wenye silaha na ujuzi wa hali ya juu yeye mwenyewe?
Dakika nane nyuma …
“Nendeni,” alisema Jona baada ya kuchomoza nyuso zao toka kwenye maji, yeye pamoja na wenzake. Macho yao yaliyokuwa mekundu kwasababu ya kula chumvi ya bahari yalikuwa yanawashuhudia wanaume wale watano wakiwa wanazama msituni kisiwani kwenda kuwatafuta.
“Twende wapi?” akauliza Lee wakimtazama Jona.
“Nendeni kwenye boti,” Jona akasema. “Mimi nitarudi kule kisiwani kukabiliana nao.”
“Mwenyewe?” Miranda akadakia.
“Ndio, mwenyewe. Kuna haja gani ya kwenda wote kama kazi inaweza kufanyika na mmoja wetu?” Jona akasema akiwatazama wenzake kwa macho ya uhakika.
“Una uhakika?” akauliza Miranda. Uso wake ulikuwa na mashaka.
“Ndio, nina uhakika. Ikipita dakika arobaini na tano sijafika, basi nyie nendeni.”
“Hatuwezi kwenda tukakuacha, Jona,” aliteta Miranda kisha akamshika Jona mkono na kumwambia, “Please, be safe.”
“I will be safe,” akasema Jona na kabla mtu mwingine hajaongeza neno lingine, mwanaume huyo akazamia kwenye maji asionekane ameelekea upande upi wa dunia. Basi Miranda na Lee wakafanya kama vile walivyoambiwa, wao waende botini. Jona yeye ataenda kukabiliana na wale wanaume walioenda kule msituni mpaka arudi na kitambulisho, gate-pass (kama itakuwapo) na chombo cha mawasiliano alichobebelea yule mkuu wa kikosi kilichokuja kumwokoa Wales.
Walijua mwanaume huyo alikuwa navyo kwani walishawafuatilia watu hao kwa muda fulani huko msituni. Yaani siri ilikuwa sirini. Wakati wanaume hao wakiwa wanajificha na kufanyia siri kwenye mashambulizi yao, na wao sirini walikuwa wanatazamwa ama kufuatwa!
Kifuani mwa mwanaume yule aliyekuwa kamanda mkuu wa wenzake, kulikuwa kunaning’inia karatasi fulani iliyokuwa ‘laminated’. kwenye karatasi hiyo kulikuwa na picha ndogo na pembeni ya picha hiyo taarifa kadhaa.
Ilikuwa ni jambo linaloleta maana masikioni kuona wakina Jona wanawinda namna ya mawasiliano ya mkuu huyu. Walijua watu hawa wametoka kutumwa na hivyo basi mawasiliano yao na makaoni huwa yenye nguvu na tija kuliko yale ya Wales. Walijua watu hawa watakuwa na cha ziada. Cha ziada ambacho kitawasaidia kuangusha ngome mbeleni.
Lakini wote twajua kuwa kupata vitu hivyo haitakuwa nyepesi. Tena ikifanywa na mtu mmoja ambaye silaha yake ni mikono pekee.
**
Alipochomoza toka kwenye maji alipanda haraka ardhini. Alikuwa kwenye ubavu wa magharibi wa kisiwa. Alitazama huku na kule kabla upesi hajakimbia na kuzamia kwenye miti.
Na basi akiwa amebeba tahadhari zote, akatazamia ardhi na kuona alichokuwa anakitaka baada ya hatua kadhaa, nacho si kingine bali alama za watu anaowatafuta. Majani yalikuwa yametawanyika mahali walipopita, na pengine ambapo hapakuwa na majani akaona nyayo za viatu.
Akafuatilia kwa muda wa dakika sita. Akajibana kwenye kwenye mti baada ya kusikia sauti ya wanaume wakiongea. Aliporusha macho yake, akaona watu wawili. Ni wale ambao walipewa kukagua upande wa magharibi.
Akaendelea kunyata kuwajongea. Ilikuwa ni hatari kwake kuwaonyesha alipo mapema maana walikuwa na silaha za moto, wangeweza kuzitumia kummaliza kabla hajatimiza adhma yake.
Basi alipoona sasa amekaribia vya kutosha, akanyanyua tawi moja la mti lililo kavu, lakini kabla hajamaliza kunyanyuka, tawi lile likameguka kuvunjika! Likatoa sauti iliyowashtua wanaume wale na kuangazia upande huo upesi!
Jona akatulia tuli nyuma ya mti akihema taratibu. Wanaume wale wakatazama eneo hilo kwa sekunde kadhaa. Na wasipuuzie jambo, wakatazamana na kupeana ishara ya kwenda kutazama kupata uhakiki. Taratibu wakajongea, ila ghafla wakasikia sauti ya kitu upande wao wa kushoto. Haraka wakageukia huko!
Kutazama wakaona ni kipande cha tawi la mti. Kilikuwa ni kipande ambacho Jona amekirusha. Kabla hawajarejewa na akili, Jona akawa ameshawafikia. Kurejesha nyuso zao kule walipokuwa wanaelekea, bunduki zikakamatwa na kuviringitwa duara kamili, mikono yao ikachina, sasa haraka silaha hizo zikavutwa pasipo kipingamizi.
Hawajakaa vema, silaha zao zikatumika kuwabondea vichwa na kuwaangusha chini wakiwa hawana fahamu. Jona akachojoa vyombo vyao vya mawasiliano na kuzihifadhi silaha zao kwa ajili ya matumizi ya baadae.
“ … thirteen … fourteen … Fifteen!” alisema Jona kisha akapiga ngumi kiganjani mwake. Mpaka muda huo alikuwa ametumia robo saa. Hivyo ana nusu saa tu kutimia dakika arobaini na tano za kumaliza kazi yake. Muda ambao amewaambia wenzake kuwa ukifika na bado hajarudi, basi wawashe boti kwenda zao.
**
“Sure? … ok, we’re coming!” alisema yule kamanda mkuu wa kikosi kisha akamtazama mwenzake aliyekuwa anashirikiana naye kwenye ukaguzi wa kisiwa eneo la katikati. “They’ve got them in the West!” akamwambia kisha akawasiliana na wale wengine wa upande wa Mashariki kuwa hawana haja ya kuendelea kusaka kwani watu wao wamepatikana.
Basi wakaanza funga safari kuelekea kule upande wa magharibi. Walikuwa wanatembea kasi wakiwasiliana. Baada ya dakika kama kumi na moja, wakawa wamefika upande huo wa magharibi wakiwa wote wanne.
“Hey, where exactly are you?” akauliza kamanda mkuu. Punde akajibiwa, akawatazama wenzake na kuwapa ishara ya kichwa kuwataka wasonge mbele zaidi. Wakasonga kwa dakika mbili. Ila ghafla kamanda akawataka wasimame kwani alihisi kitu! Wote wakasimama!
Kwa utulivu mkubwa akaskiza. Macho yake yalienda kushoto na kulia. Juu na chini. Hamaki! Akatokea Jona mbele yao toka nyuma ya mti mkubwa uliopo hatua nane tangu walipo.
Mwanaume huyo alikuwa amebebelea bunduki kwenye mikono yake yote miwili na tayari tunduze ameshawaelekezea maadui. Basi kamanda kuona vivyo, kabla Jona hajabinya vitufe vya bunduki, upesi mno akamkamata mmoja wa wenzake na kumweka mbele yake kujikinga.
Basi risasi zikanyesha haswa!! Ilikuwa ni ti!-ti!-ti!-ti!-ti!-ti!-ti!-ti! Wanaume wale wakizungu wote wakala za kutosha isipokuwa yule kamanda mkuu ambaye akiwa amejikinga, akawa anasonga kumfuata Jona.
Aliposonga karibu kidogo, akamrushia Jona mtu yule aliyekuwa anamkingia. Jona kumkwepa mtu huyo na kukaa vema, kamanda akawa ameshamfikia akatengulia bunduki zake kando. Akachomoa bunduki yake ndogo, ila Jona naye akawahi mkono wake na kuutengua, bunduki ikadondokea chini. Sasa wote wakawa hawana bunduki mikononi.
Wakatupiana mikono, ila wote wakafanya ustadi kujilinda. Wakakaa tenge kutazamana kana kwamba majogoo. Kamanda akauliza, “So you are the dangerous one?”
Jona hakujibu akamvamia. Alikuwa hana muda. Alikuwa anakimbizana na muda na mpaka muda huo alikuwa amebakiza dakika kumi na mbili tu.
**