*ANGA LA WASHENZI II --- 79*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
“Jona,” na kisha akasema kwa uhakika, “nadhani kuna mtu tunamhitaji kuturahisishia kazi yetu.”
“Nani huyo?” Jona akauliza.
“Mwanamke mmoja aitwa Glady,” Lee akajibu akimtazama Jona machoni.
“Glady? Ni nani huyo na atatufaa vipi?”
ENDELEA
Lee akachukua zamu kueleza ni kwa namna gani Glady anaweza kuitenda kazi kwa kutumia kaliba yake ya kujiuza na kujua kushawishi, Jona akavutiwa na maelezo hayo, ila kwa namna gani Glady atakuja kuwakuta na pesa hata ya kumsafirisha hawana?
“Usijali,” akasema Lee. “Nitamwelekeza Marwa aliyekuwepo nyumbani nini afanye na pesa atazipata. Zipo nyingi sana chini ya akaunti yangu na hata ya Sheng mwenyewe.”
Wakakubaliana na Lee akafanya mpango wa kuwasiliana na Glady kwenye mtandao wa whatsapp. Kheri alikuwa anakumbuka namba ya mwanamke huyo. Alimpata ndani ya muda mfupi na akamweleza haja ya moyo wake. Jambo hilo likamshangaza na kumtisha Glady, ila akapata uthubutu baada ya kuambiwa kauli hii na Lee:
“Nitakupa pesa unayotaka.”
Akajichekesha na kuridhia dili hilo ambalo mbele ya macho yake lilionekana ni nono haswa. Uzuri alikuwa ana passport na kuhusu visa Lee akamwambia afike ubalozini, kuna mtu wake pale atakayempanga kufanikisha hilo ndani ya muda mfupi.
Wakaelewana kila kitu na ikawa ndani ya mipango kuwa Glady atafika Uingereza keshokutwa kama mambo yakienda vile yanavyotakiwa.
Basi baada ya hapo, Jona na wenzake wakaona ni vema wakienda kutembelea jiji la London na hata basi watakapopata fursa waende na kuyaona na yale maeneo ambayo wale mateka wao wamewaeleza.
Ndani ya muda mfupi wakawa wamejiandaa. Wakawafungia wale mateka wao ndani ya chumba na kisha wakaondoka kwenda kubarizi jiji. Wakafanya vivyo ndani ya masaa matatu, walipomaliza kutalii huko wakaanza kupitia eneo moja baada ya lingine ya yale waliyopewa taarifa nazo. Uzuri Lee alikuwa msanifu mzuri kwenye uchoraji, akachora kila linalotakiwa, haswa muonekano wa majengo, njia na hata vituo.
Kwahiyo kwenye majira ya jioni ndipo walirejea kwenye makazi yao, ya wale wakazi waliowateka, wakiwa wamefanya kila linalotakiwa. Ila walipofika walikuta mazingira tofauti, na jambo hili kidogo likawazusha shaka.
Mosi, walikuta mlango u wazi. Pia walipotazama eneo walipowahifadhi wale mateka wao, hawakuwakuta! Zilibakia kamba tupu pasipo cha kufungia. Swala hili likawafanya damu zao zianze kuchemka!
Kulikuwa na nyayo kadhaa za viatu kwenye zulia. Kwa harakaharaka nyayo hizo zilikuwa za watu watatu. Ina maana ndiyo hao waliokuja kuwakomboa mateka!
Hawajakaa vema risasi zikaanza kurushwa kupasua vioo vya dirisha! Haraka Jona na wenzake wakalala chini. Risasi zikaendelea kutupwa kuchafua na kuharibu kabisa jengo. Zilikuwa ni risasi za mfululizo na nyingi!
Watu waliokuwa wanashambulia walikuwa watano. Wanaume watatu na wanawake wawili. Wanaume walikuwa wamevalia makoti marefu rangi ya kaki, pengine ni sababu ya mvua za hapa na pale na baridi. Wanawake walikuwa wamevalia makoti ya ngozi yaliyobana miili yao na kufanya waendane na fasheni na kwa wakati huohuo kujiweka salama dhidi ya baridi.
Nyusoni walikuwa wamevalia miwani meusi, ilikuwa ajabu ukitazama na muda huu wa giza. Labda, tuseme labda, miwani hizi hazikuwa za jua kama tujuavyo tuonapo kila miwani meusi.
Basi mashambulizi yakaendelea kwa fujo. Ilikuwa ni kitu cha kushangaza maana Jona na wenzake hawakuwa wamkitarajia hili kwa ghafla hivi. Hawakudhani pengine vita ingeanza mapema kiasi hiki.
Sasa maadui watakuwa wanajua kuhusu ujio wao, si ndiyo hivyo? Na pengine pia washajua kuwa wale makamanda wao waliowatuma tayari wameshauawa.
Ndio, hilo lilikuwa bayana. Kumbe muda mfupi baada ya wao kuondoka, watu hawa wa kazi walifika kwenye makazi ya hawa madereva kwa ajili ya kukusanya taarifa toka kwao baada ya ukimya wa ajabu tangu watumwe. Ukimya pia kwa wale makamanda ambao hawakuwa wanapatikana hewani kwa ajili ya mawasiliano.
Walichokikuta ni madereva hao wakiwa kambani na wakiwa tayari wametoa taarifa nyeti. Haraka wakapasha habari kule makao makuu na agizo likatolewa kwamba watu hao wamalizwe haraka kabla haijaleta kizazaa ndani ya nchi.
Kumbuka taasisi hii ni ya siri. Hata waingereza wenyewe hawakuwa wanafahamu juu ya uwepo wake isipokuwa kwa watu kadhaa nyeti, tena wachache. Na ilitakiwa kuwa hivyo milele na milele, aamin.
“Fuata silaha!” akapaza Jona. Kulikuwa kuna kelele sana. Risasi zilizokuwa zinapasuapasua madirisha zilifanya usikizani uwe hafifu. Ilibidi umtazame mtu anayeongea mdomoni ujue anasema nini au basi mpeane ishara.
Taratibu wakasonga kwenda vyumbani. Kila mmoja na alipoweka silaha yake akachukua na kuziweka vema kwa ajili ya kujikomboa. Sasa wakaanza kupekua huku na kule kuangazia maadui zao wapo pande gani.
“Wawili wapo upande wa mashariki …” akasema Komandoo mmoja, Blanko kwa jina la vitani. Mwingine naye, Chombo, akasema kuna wawili upande wake wa magharibi. Jona akamalizia kwa kusema kuna mmoja upande wa kaskazini.
Basi baada ya jitihada hizo za kufahamu walipo maadui zao kufanikiwa, japo ilikuwa ni tabu wakipunyuliwa na ncha za risasi madirishani, wakagawana majukumu ya kuwashuhulikia. Makomandoo wawili, Chombo na Tito, wakapewa shavu la upande wa magharibi. Blanko na Miranda wakapewa upande wa mashariki na Lee akapewa upande wa Kaskazini.
Jona yeye akabaki kuwa ‘free roller’ kazi yake ikiwa ni kuangazia na hata itakapobidi kwenda nje kuangalia kama kuna wengine na kupambana nao!
Basi mashambulizi ya kutupiana risasi yakadumu kwa muda wa dakika sita. Wakafanikiwa kuwaangusha maadui watatu na kuwabakiza wanaume wawili tu. Ila hao wawili wakiwa wamefahamu kuwa wamezidiwa na mipango ya kimashambulizi, wakajificha, na basi wakawa wanatupa risasi zao kwa kutegea.
Wakitupa mbili tatu, wanajiziba ama kuinama kusikizia majibu yaliyokuwa yanakuja kwa mkupuo.
“We need backup!” alisema mmoja. Walikuwa wameweka migongo yao nyuma ya kuta wakihema kana kwamba wametoka mbio.
“We are outnumbered! We need damn backup!” akafoka. Mwenzake akamtazama na kumwambia, “we need to go, not backup! Police are going to be here soon!”
Hawajakaa vema, wakasikia king’ora cha polisi. Sasa wakaanza kutazamia nafasi watoroke kabla hawajatiwa nguvuni. Haikutakiwa kujulikana kama ni wao ndiyo walihusika na hilo tukio. Na hata kama wakikamatwa basi watajieleza kuwa wao ni majambazi na si wahusika wa taasisi yao ya siri.
Walipotazama na kuona mazingira ni sawia, mmoja akachoropoka upesi akimwacha mwenzake nyuma. Mwenzake naye akatazamia usalama, mara naye akachopoka, ila alipokata kona akifuata upande ule alipokimbilia mwenzake, akastaajabu kumkuta mwenziwe chini!
Hajakaa, mara akajihisi hana nguvu! Akajihisi analegea. Akadondoka chini asielewe kitu. Alikuwa gizani. Sauti ya king’ora cha polisi ilififia masikioni mwake na hatimaye ikakoma kabisa.
Punde Jona akamsachi na haraka akatokomea hapo.
**
Saa tatu usiku …
“We failed!” alifikisha taarifa mwanamke mwenye kibandiko cha upanga, yaani Sword., kifuani Alikuwa amesimama kwa ukakamavu akimtazama mkuu wao aliyekuwa amekaa vema kwenye kiti chake akiwa ameziba mdomo wake kwa kiganja chake kipana.
“You failed,” mkuu akarejea kusema kauli hiyo kisha akatabasamu. “They’ve killed all our commanders. Kidnapped our drivers and got almost all information … Moreover, they are on our playground, at our home! … and you come here to tell me about failure!”
Mkuu akabamiza ngumi mezani. Akasimama na kumkwida mwanamama aliyemletea taarifa, akamsogeza karibu na uso wake uliokuwa umegeuka kuwa mwekundu.
“Don’t tell me that shit, okay? I am not used to failure, my dear. And don’t make me be, my dear. Got me?”
“Yes, sir!”
Mkuu akamsukumiza mwanadada huyo kando na kumfokea akimyooshea kidole.
“I want them within reasonable time! Nobody can hide in this country as far as I know it like the palm of my hand! … And when you get them, bring them here to face me.”
“Yes, sir!”
Mwanamama akageuza mgongo wake kuufuata mlango. Mkuu akatoa agizo la mwisho. “Don’t return here with empty hands as I shall kill you with my bare hands, my dear.”
Mwanamama akalipokea agizo na kwenda zake. Akakusanya kikosi cha wapambanaji kumi na wawili, na kabla hajatoka makaoni wakaingilia mifumo yote ya kamera zilizo mitaani na za utambulisho wa watu mahotelini. Hivyo punde watakapoona nyuso za walengwa wao zifanyiwe kazi haraka iwezekanavyo.
Jambo hilo halikuwawia ugumu kwani nyuso za Jona na wenzake zilikusanywa upesi baada ya kufanya utaalamu wao wakizitoa kwenye kamera zilizokuwa zimefungwa kwenye nyumba za wale madereva waliotekwa.
**