*JOANA ANAONA KITU USIKU -- 16*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Alikuwa ana usingizi mzito ila alikuwa na hofu huenda akakabwa tena.
Kwa upande wa Joana yeye alikuwa amekabwa na maswali. Akili yake ilikuwa inawaza huyo mkabaji ni nani? Na je anahusiana na yule mhanga wa ukabwaji kwenye hoteli ya kwanza?
Vipi kama Rosie asingempiga teke? Alikuwa anakufa?
Mawazo ambayo alikuwa ameanza kuyasahau, sasa yanaanza kumrejea.
ENDELEA
Alikosa raha kabisa. Mpaka usiku unaisha hakulala kabisa. Walienda kunywa chai asubuhi na mapema lakini bado akiendelea kuwaza.
Walikula na kurejea mapumziko, baadae majira ya jioni wakatoka kwenda mazoezini kupasha viungo.
Ilikuwa imebakia siku mbili tu ili mashindano yaanze rasmi. Mkufunzi wao aliwapa maelekezo ya kuzingatia na kuwataka waanze kujenga picha ya shindano vichwani mwao.
"Hatujaja hapa kushiriki bali kupambana. Kumbukeni lengo letu ni kufika robo fainali."
Pengine lengo hilo waweza liona ni la chini, ila kwa hiyo klabu lilikuwa ni lengo mujarab tu ukilinganisha na uchanga wao.
Pale kwenye mashindao watakutana na klabu kubwa, zoefu na zenye ujuzi mkudufu. Hivyo kuchomoza na kufika hatua ya robo fainali, kwao itakuwa hatua kubwa mno.
Wakapeana motisha wakiamini kila kitu kinawezekana pakiwa na nia.
"Tule vizuri. Tupumzike na tuzingatie," mkufunzi alisisitiza.
Ila kabla watu hawajatawanyika kwenda kujiandaa ili warudi kambini, huko hotelini, mkufunzi akamwomba Joana waonane.
"Nina maongezi nawe."
Wakawa wanatembea wakiteta. Mkufunzi alikuwa anata kuulizia hali ya Joana kwani hakuonekana kama yupo sawa mazoezini.
"Ulikuwa unamis sana mipira. Hata energy na passion ilikuwa chini. Kuna tatizo?"
Joana akamwomgopea Mkufunzi kwamba alikuwa sawa, pengine ni siku tu haikuwa njema kwake.
Alihofia kama angesema ukweli kuwa hakulala basi mkufunzi angeng'aka kumgombeza.
Kwa shingo upande, mkufunzi akakubali ila akamtaka azingatie kazi kubwa iliyopo mbeleni.
"Tunakutegemea kwa kiasi kikubwa. Usije ukatuangusha."
Basi wakarudi hotelini. Baadae majira ya usiku, Joana akiwa amejitenga mwenyewe akachukua picha zake na kurudia kuzitazama.
Alizitazama kwa umakini sana. Alitazama kile kivuli alichokuwa anakiona na hakutaka hata kujiuliza maswali.
Alipapasa papasa na vidole vyake kabla hajafunga hizo picha na kubakia akiwanda wanda.
Hakutaka kulala. Aliogopa kulala japokuwa kwa muda ni kama vile hakuwa anajua kwanini anaogopa kufanya hivyo.
Alimtazama Rosie akamwona tayari ameshalala. Amejifunika shuka akikoroma kabisa. Akatamani angelikuwa yeye.
Basi kwasababu hakuwa na usingizi na usiku ni mrefu, akaamua kutafuta jambo litakalomsogezea muda. Asingeliweza kukaa macho muda wote vile.
Akili yake ikampatia wazo. Ila wazo hatarishi. La kwenda mojawapo ya klabu ndani ya jiji la Paris akaukatie usiku huko.
Swala la pesa halikuwa na shida kwani alikuwa ana kiasi cha maana tu alichopewa na mamaye.
Ila akasita ... akawaza ... akaamua kukata shauri kwenda. Abaki pale hotelini kufanya nini na wakati amekuwa bundi?
Akavaa na kutoka, akachukua taksi iliyompeleka moja kwa moja mpaka kwenye klabu moja ya usiku inayoitwa ROGUE. Humo akazama ndani na kushawishika kunywa vileo.
Akaagiza whisky moja kali ya kumsahaulisha mawazo. Taratibu akawa anapiga tarumbeta akitazama watu wakicheza muziki kwenye mwanga hafifu unaong'arishwa na vijitaa vya rangi rangi.
Alipokuwa amekaa palikuwa ni kochi kubwa gizani. Mwanga ulikuwa unamulika mara moja moja na Joana alitokea kupenda hayo mazingira.
Akatulia hapo akinywa na kunywa. Muda si mwingi akapata kampani ya mwanaume fulani mnene aliyejitambulisha kwa jina la Rabiot.
Mwanaume huyo alikuwa amebebelea glasi ya mvinyo na alikuwa anapata shida kuongea kiingereza kuelewana na Joana.
Ni mtu mwenye asili ya Ufaransa. Kiingereza chake kilikuwa kimemezwa na lafudhi ya kifaransa akiongea maneno utadhani anayameza.
Joana alifurahia kampani hiyo kwani ilimwondolea upweke. Lakini pia ilikuwa imamsogezea muda.
"Unahitaji nyingine?" Akauliza Rabiot baada ya kuona Joana anatikisa chupa ya whisky. Kabla Joana hajajibu, Rabiot akamuita mhudumu na kumpatia chupa ya Joana.
"Leta kama hiyo!" Akasema kwa kifaransa. Mhudumu akaleta nyingine, Joana akaendelea kujimiminia.
Kwenye majira ya saa tisa usiku, Rabiot akatoka na Joana. Joana alikuwa amelewa na maamuzi anayoyafanya yakisukumwa na kileo kichwani.
Aliridhia kwenda kulala na Rabiot nyumbani kwake. Jambo ambalo kama angelikuwa mzima asingelifanya.
Rabiot yeye hakuwa amelewa. Alikuwa mzima na anayejitambua. Na alikuwa anajua kile anachokifanya.
Alimpakia Joana kwenye gari lake, Volkswagen ndogo rangi ya kijivu, wakaelekea mpaka nyumbani kwake.
Ilikuwa ni apartment moja nzuri inayopatikana pembezoni mwa jiji. Ndani yake kulikuwa kumepangiliwa vizuri, na rangi za kupendeza.
Rabiot akampeleka Joana chumbani kumlaza, kisha akaenda kuoga. Aliporudi akamvua nguo Joana na kuanza kumkagua kwa macho ya uchu.
Alitimiza haja yake pasipo shaka kisha akajilaza pembeni hoi. Alijiona mwenye bahati siku hiyo tangu aanze mtindo wake wa kwenda klabu za usiku.
Alipitiwa na usingizi mzito akalala kama mfu. Yalikuwa ni majira ya saa kumi na dakika kadhaa.
Usichukue muda mrefu, Rabiot akajikuta anakabwa na mikono migumu yenye nguvu. Alifurukuta kwa namna zote ila hakufanikiwa kabisa. Alidakwa shingo mpaka akakata moto.
Aliachama mdomo ulimi ukienda kando. Kisha kama hakuna kilichofanyika muda ukasonga kukiwa kimya.
Yalipofika majira ya saa tatu asubuhi, Joana akashtuka. Alijikuta uchi amelala kando mwanaume. Akaangaza huku na huko kabla hajampiga kofi Rabiot na kufoka kwanini kamfanyia tendo lile pasipo ridhaa yake.
Alifoka akiendelea kumpiga Rabiot, akagundua Rabiot hakuwa hai. Hakuwa anahema wala kutikisika.
Nani kamuua? Akajikuta anajiuliza upesi.
Alipomtazama Rabiot shingoni akagundua alikuwa ana michubuko, na mivilio ya damu. Ndani hakukuwa na mtu mwingine yoyote bali wao, sasa nani kamuua?
Ni yeye!
Aligundua ana alama za meno kwenye mkono wake wa kuume. Maana yake nini? Ina maana aling'atwa wakati anamkaba Rabiot?
Mbali na hayo ilibidi kwanza atoke eneo hilo upesi kabla mambo hayajaharibika, ila huko napo anapoenda ataeleza nini? Mpaka muda ule itakuwa tayari imeshajulikana kambini kuwa hayupo!
Alivaa akaangaza usalama nje. Alichukua kila kilicho chake. Akafanikiwa kuchoropoka ila maeneo ya getini ndipo akakutana na mwanamke fulani ambaye hata hakumsalimia, akaenda na zake.
.
.
.
USIKOSE SEHEMU IJAYO.
Sent from my SM-J110F using
JamiiForums mobile app