*JOANA ANAONA KITU USIKU --- 04*
ILIPOISHIA …
Baadae majira ya usiku, saa tano, Mama akaenda kumgongea mlango Moa. Akaketi pembeni ya kitanda na kumueleza:
“Rudisha bangili hiyo kwa Joana. Umenielewa?”
“Mama ame…”
“Sitaki maneno, Moa. Nimekwambia rudisha hiyo bangili, sawa?” Mama alisema akitumbua macho yake meupe nje. Moa akaogopa.
ENDELEA…
Japokuwa mama yake aliondoka, lakini mwanaume huyu hakulala kwa amani. Sauti ya mama yake ilikuwa inajirudiarudia masikioni mwake na kumgutua. Akafikiria pia kuhusu Joana basi ndiyo akazidi kukosa usingizi.
Akaamua kutoka kitandani na kwenda nje kibarazani. Huko akaegemea kingo ya kibaraza akiangaza mbali, mwili wake ukipulizwa na upepo wa bahari wenye fujo.
Akaendelea kuwaza hapo akitegemea upepo wa bahari unyakue angalau mawazo kidogo na kupumzisha kichwa chake.
Lakini twende mbele turudi na nyuma, mwanaume huyu alikuwa na jambo fulani la kutuweka wazi.
Pasi na shaka.
Ni yeye ndiye alimpokonya bangili Joana baada ya kusimuliwa yale yanayomtukia mwanamke huyo. Je kwanini alimpokonya? Ina maana anajua jambo kuhusu bangili hiyo?
Anadhani pengine ndiyo sababu ya mauzauza ya Joana? Japokuwa hakuwa na uhakika, aliamini bangili hiyo ndiyo adui haswa.
Simulizi za kale alizokuwa anazisikia, tangu akiwa utotoni, kumhusu mama yake kuhusishwa na ulozi zilikuwa zinaingilia sikio moja na kutokea lingine. Hakuwahi kuziamini kamwe.
Alibashiri ni kwasababu ya macho ya mama yake, na kovu kubwa usoni mwake ndivyo vilikuwa sababu ya shutuma hizo. Alikuwa anampenda mama yake, na mama yake alikuwa anampenda vilevile.
Kuna siku moja, akiwa mvulana mdogo wa miaka kumi na miwili, alirudi shule akiwa amechoka mno na mwenye njaa. Alikuwa anaburuza miguu na begi lake la mgongoni akilining’iniza mkononi.
Nyumba siku hiyo ilikuwa pweke asiwepo mtu hata mmoja.
Alimuita mamaye, lakini hakupata majibu. Kabla hata ya kwenda jikoni kutazama chakula kukidhi haja yake ya tumbo, akaenda kwanza chumbani mwa mama yake kutafuta.
Hakuzoea kujipakulia chakula mwenyewe, na hii ni kwasababu ya kudekezwa na wazazi wake tangu yeye ni mtoto wa mwisho.
Aligonga mlango pasipo majibu, akausukuma na kuzama ndani. Akaangaza angaza, hakuona mtu, lakini juu ya meza iliyokuwa imesimama pembeni ya kitanda akaona kisanduku kidogo cha chuma.
Kilikuwa rangi ya bluu iliyokoza. Na kalikuwa wazi.
Akapata hamu ya kutaka kujua kilichomo ndani. Akakisogelea na kutazama, ndaniye akaona bangili nyingi za shepu mbalimbali, na mikufu michache.
Bangili moja ikamvutia kwa kung’aa kwake, michoro na hata umbo lake mithili ya mawimbi ya maji. Basi akainyakua na kwenda nayo sebuleni. Akaichezea na kuijaribishia mkononi.
Ilikuwa inawakawaka!
Kwa muda kidogo bangili hiyo ikamsahaulisha uchovu na njaa aliyokuwa nayo. Alihisi ni ya gharama kubwa sana, na basi pengine kila mtu angependa kuwa nayo. Akaiweka kwenye mkoba wake kwa ajili ya kwenda kuwaonyesha na kuwaringishia marafiki zake shuleni kesho yake.
Baadae mama yake aliporejea, akamkuta akiwa tayari ameshakula na kujilaza na sare zake za shule. Hakugundua kama Moa amechukua moja ya bangili yake, akalaumu tu kwa kukuta kisanduku ki wazi.
“Huyu mzee anapenda kupekua vitu vyangu, kuna siku vitamtokea puani!” Moa alikumbuka namna mama yale alivyolalama. Ingawa alikuwa kwenye usingizi alisikia vema.
Alisikia pia na sauti ya kisanduku cha bangili na mkufu kikifungwa kwanguvu. Muda mfupi kidogo, mama yake akaja kumwamsha na kumtaka akaoge na kubadili nguo.
Kesho yake, asubuhi na mapema ya majira ya saa kumi na mbili kasoro, Moa akaamka kwa ajili ya kujiandaa kwenda shule. Hakuamshwa siku hiyo tofauti na ilivyo kawaida yake mpaka mamaye ampokonye blanketi, tena kwa mbinde.
Ni hamu tu ndiyo ilimkata usingizi na kumgutua – hamu ya kutaka kuringishia bangili kwa marafiki.
Alisugua meno na kuoga, mamaye akamkuta akiwa anavaa sare. Akatabasamu na kumpongeza:
“Umekua sasa, Moa. Ukiendelea hivyo utakuwa mtoto mwenye nidhamu na akili!”
Moa akatabasamu pasipo kutia neno. Alikuwa anakwepa macho ya mama yake mara kwa mara. Alitaka kuondoka haraka kwa kuhisi anaweza kugutukiwa.
Kweli akafanikiwa.
Kitu cha kwanza kukifanya wakati wa mapumziko, ikawa ni kuwakusanya marafiki na kuwaonyesha mali aliyo nayo – bangili. Wote wakatahamaki!
“Umeitoa wapi, Moa? Naweza nikaiona?”
Moa akatamba na kujivuna. Rafiki yake kipenzi aitwaye Filipe akamuazima bangili hiyo aenda nayo na atamrejeshea kesho.
“Nitakupa na zawadi, Moa,” Felipe akaahidi. Moa akasukumwa kumpatia. Kwani si atarejesha? Na zawadi si n’tachukua?
Felipe akaweka bangili mkobani, na wazo lake la kwanza lilikuwa ni kwenda kumpatia dada yake.
Siku iliyofuata, Moa akawahi pia kuamka na kwenda zake shule. Siku hiyo alikuwa anajua anapata zawadi na pia anarejesha bangili nyumbani. Faida maradufu!
Alilenga akishairudisha, basi achukue nyingine na mtindo uwe ule ule kama alioufanya awali. Atatengeneza faida kiasi gani? Aliwaza na kujikuta akijibu kwa tabasamu.
Lakini mbaya alipofika shule, hakumwona Filipe. Hakuwepo darasani wala shule nzima.
Akajihisi vibaya kwa kudhani amedanganywa, na pengine rafiki yake, Filipe, amemzulumu.
“Twende, mi napajua kwao!” Rafiki mmoja akamsahuri Moa. Basi wakakubaliana waende punde tu watakapotoka shule.
Ila kabla muda wa kutoka haujawadia, mwalimu wao wa darasa akaingia darasani na kuwataka watulie maana ana tangazo anataka kuwapatia. Wote wakatii agizo.
“Mwenzetu Filipe amefiwa na dada yake usiku wa kuamkia leo. Amefia huko baharini alipozama na kuokotwa.”
Moa akashikwa na huruma, pamoja pia na marafiki zake, kumbe sasa akajua nini hakikumleta Filipe shuleni, sasa hapo wakaongezeka idadi ya watakaoenda kwa kina Filipe, lengo likiwa kumpa pole.
Wakaongozana pia na mwalimu wa darasa kama mwakilishi wa shule.
Siku hiyo nzima Moa akaipotezea huko. Alimuuliza Filipe kuhusu ile bangili aliyompatia, Filipe akamwambia alimkabidhi dada yake, na hata alivyoenda huko baharini nyakati za usiku, alienda nayo.
Kwahiyo bangili ilikuwa imepotea.
Lakini kwanini dada yake Filipe aende baharini usiku? Yani atoke usiku na kwenda bahari tena pasipo kumwambia wala kumuaga yeyote? Japo Moa alikuwa mdogo, akili yake ilishangazwa sana na haya.
Kwasababu alichelewa mno kurudi nyumbani siku hiyo, mama yake akafungasha safari kwenda shule kumuulizia. Akapewa taarifa za msiba wa Filipe, rafiki yake Moa, akaona heri kwenda huko kumkuta mwanaye.
“Kwanini haukuja nyumbani kun’taarifu kuwa unaenda msibani?” Mama aliuliza kwa hasira.
Aliunyakua mkono wa Moa akaenda naye baada ya Moa kumuaga rafiki yake, Filipe.
Baadae wakiwa nyumbani wanakula, basi Moa akamuuliza mama yake kuhusu yale yaliyokuwa yanamtatiza kumhusu dada yake Filipe.
Namna alivyokufa maji kwa kutoka na kwenda baharini usiku wa saa sita bila kumuaga yeyote, wala kushirikiana na yeyote.
Mama yake akamkazia macho na kumuuliza:
“Kuna yeyote aliyemuona wakati anaenda huko baharini?”
“Ndio,” Moa akajibu. “Filipe alimuona. Akamuita mara tatu lakini hakugeuka wala kujali.”
Mama akanyamaza asiseme lolote lingine. Wakala na baadae wakati wa kulala, mama akaja chumbani kwa Moa.
Usoni alikuwa na ndita za mashaka. Mkono wake wa kushoto alikuwa ameukunja ngumi ukitetemeka.
“Moa,” akaita kabla hajaketi kitako kitandani.
Moa akaamka na kumtazama mama yake.
Uso wa mama ulikuwa na kielelezo kilichompa walakini, kuna jambo halikuwa sawa.
“Moa, umechukua bangili kule kwenye kisanduku chumbani?” Mama aliuliza.
Moa akajikuta anaishiwa nguvu kabla hata hajanena.
***
Sent from my SM-J110F using
JamiiForums mobile app