*ANGA LA WASHENZI --- 05*
*Simulizi za series*
Cha kwanza alichokifanya Jona ni kuulizia taarifa zote za mtandaoni kumhusu mke wa Mheshimiwa. Alitaka kujua majina na akaunti zake.
Asiwe na bahati, Mheshimiwa akawa hajui lolote kuhusu hayo. Cha kufanya Jona akaomba jina kamili kisha akaendelea na mengine ambayo aliona yangeweza kumsaidia kwenye kazi. "Waweza nijuza anapendelea nini? Kwenda wapi? Kufanya nini?" "Anapenda sana kuogelea. Alikuwa anaenda kuogelea kila mwisho wa juma. Pia, ni mtu wa lakshari sana."
"Unaweza ukamuelezea ni mtu wa aina gani kwa ujumla?"
"Yah! Muongeaji, mchangamfu, anayependa starehe na kujishughulisha pia."
"Na vipi kuhusu mavazi?"
"Aaahm ... kwa kifupi anapenda kwenda na wakati."
"Kabila lake?"
"Mnyaturu."
"Naomba unipatie picha yake." Mheshimiwa akaelekea chumbani na kutoka na albamu ya picha, akamkabidhi Jona. Jona akatazama na kuchagua picha tano. "Naweza nikaenda nazo zote hizi?"
"Bila shaka," akajibu Mheshimiwa.
"Ana ndugu yeyote hapa Dar?"
"Ndio. Shangazi yake anaishi Kimara suka, nyumba namba 102. Na pia mama mdogo yake anaishi Kinondoni, kama nakumbuka vema, ni nyumba namba 52. Ghorofa moja rangi nyeupe.
Hao ndiyo ninaowafahamu kwa hapa Dar."
"Kwao ni wapi?"
"Arusha; Mianzini."
"Asante sana," Jona akasimama. "Nadhani nimepata pa kuanzia hii safari." Wakapeana mikono na Mheshimiwa. "Vipi hautahitaji fedha kufanikisha hili?" Mheshimiwa aliuliza.
"Usijali nitakutaarifu punde nitakapokuwa nahitaji msaada," akasema Jona.
Ila kabla hajaondoka, Mheshimiwa akamuita na kumwambia: "Nahitaji kumpata huyo mwanamke, si kingine. Mtafute na umlete hapa. Usihangaike na mengine kumhusu.
Bila shaka tumeelewana." Jona akaitikia kwa kupandisha na kushusha kichwa chini. Ila uso wake ulikuwa na mashaka.
Kauli ya Mheshimiwa ilimpatia maswali kadhaa. Alijiuliza nini kipo nyuma ya angalizo hilo.
Alitoka ndani ya nyumba, akaenda kufuata daladala. Bado hali ya hewa ilikuwa ya manyunyu na baridi pia. Hivyo koti lake lilikuwa na faida.
Alienda kazini akamkuta Jumanne ameketi akifanya kazi fulani kwa mkono. Akamsalimu kisha naye akaketi.
Akatoa simu na kuzama mtandaoni. Akatafuta jina la mke wa Mheshimiwa ndani ya mtandao wa Facebook. "Mariam Jullian," akaandika hivyo na kusaka. Yakaja majibu mengi mno. Watu kutoka maeneo mbalimbali, ndani ya nje ya nchi.
Ikamchukua muda kumpata aliyekuwa anamuhitaji akitumia mfanano wa picha za mtandaoni na zile alizokuwa nazo.
Akapekua taarifa za mlengwa wake huyo lakini pia picha na matukio.
Picha ya mwisho kurushwa mtandaoni humo ilikuwa ni jana yake tu. Hilo jambo likamshangaza Jona. Kumbe mwanamke huyu alikuwa hai, tena mwenye furaha.
Akaipakua picha hiyo aitazame vizuri. Akaikagua mazingira akagundua ni ya hoteli. Alihangaika kujua ni hoteli gani na ipo wapi, ila ndani ya picha ile hakufanikiwa.
Akarudi tena mtandaoni na kupekuwa. Akapakua tena picha mbili nyuma ya ile picha ya mwanzo, zote aliona zinarandana mazingira.
Akaanza kuzikagua kwa undani. Katika hizo picha akafanikiwa kumuona mwanamapokezi wa hotel kwa mbali. Ni wazi zilipigwa malangoni mwa hoteli.
Alikuwa ni mwanaume aliyevalia shati jeupe na tai ya mistari mistari. Alikuwa amezingirwa na meza kubwa inayong'aa.
Mbele yake kulikuwa kuna tarakilishi nyeusi isiyo na chogo.
Kwenye picha moja, mfanyakazi huyo alikuwa amefunikwa nusu ya kifua na tarakilishi, ila ya pili kidogo alikuwa wazi. Hiyo Jona ikamfaa.
Akaivuta kwa ndani akilenga kifua cha mfanyakazi huyo. Alipokipata kwa karibu akapata kujua jina la hoteli.
Lilikuwa limeandikwa juu kidogo ya mfuko pamoja na chapa yake.
Ilimchukua umakini Jona kung'amua hilo kwani kuvuta picha kwa ndani kunaharibu ubora wa picha kimuonekano.
Alimuaga Jumanne akaondoka akiahidi kurejea. Akaenda nyumbani kwake alipobadili nguo na kuchukua vitu kadhaa.
Baada ya muda mfupi akawa ameshafika mbele ya hoteli anayoitaka. Akazama ndani mpaka mapokezi.
Bahati akamkuta mwanampokezi yule aliyemuoma pichani, ila alikuwa njiani akitaka kuondoka baada ya kumuachia mwenzake zamu. "Samahani kidogo," akasema Jona akimsimamisha mlengwa wake. Akachoropoa kitambulisho cha polisi ndani ya koti na kuonyeshea.
Kilikuwa kitambulisho feki, ila kwa macho ya raia wa kawaida asingeweza kugundua abadani.
Hii ilikuwa ni mojawapo tu ya nyaraka feki alizonazo Jona. Ndani ya ghala lake, anazo nyaraka feki lukuki, kwa kazi lukuki kama mwenyewe asemavyo.
Baada ya kutoka jeshini aliona anahitaji nyaraka hizo ili mambo fulani yaende, nyakati fulani. "Naitwa Inspekta Maganga. Kuna taarifa nazihitaji kutoka kwako." Mfanyakazi yule wa hotel akaonyesha hofu. Bila shaka hakuzoea madhila za polisi. Aligeuza shingo akamtazama mwenzake aliyemuachia zamu kwa macho ya maulizo. Alikuwa mwanamke mrembo mweupe ndani ya sare. "Karibu, inspekta," kisha akasema. Wakasogea karibu na kaunta. Wafanyakazi wa hoteli wakajitambulisha.
Inspekta akatoa simu na kumuonyeshea mlengwa wake picha ile ya mke wa Mheshimiwa aliyoipiga karibu na malango. "Nahitaji taarifa za huyu mtu. Alikuja hapa jana majira ya saa nne asubuhi." Haikuwa ngumu kwa mfanyakazi yule wa hoteli kumng'amua mgeni huyo. Picha ilimsaidia kurejesha kumbukumbu haraka.
Akaendeea tarakilishi na kupekua taarifa za wageni ndani ya muda husika. Punde tu akazipata. "Anaitwa Salome Gerald. Alikuwa ameongozana na mwanaume, kwa jina Mushi Gadi," akasema mhojiwa.
"Ina maana wameshaondoka tayari?" Jona akauliza.
"Ndiyo, wameondoka asubuhi na mapema leo hii."
"Wametokea wapi? Na wanaelekea wapi?"
"Wametokea Arusha, wanaelekea Iringa," mhojiwa akasoma taarifa za wageni ndani ya tarakilishi.
"Walikuja na usafiri?"
"Sijajua. Pengine tungetazama videos za cctv." Mchakato huo ukawachukua kama nusu saa, Jona akawa amepata kila anachokitaka. Akaaga na kuondoka.
Akiwa ndani ya daladala akaendelea kupekua mtandaoni juu ya mke wa mheshimiwa.
Miongoni mwa picha, akamuona mwanaume fulani aliyemtilia shaka. Mwanaume huyu alikuwa amefanana na yule aliyemuona kwenye video hotelini akiwa ameongozana na mke wa mheshimiwa.
Akapakua picha hiyo na kuitunza. Akapakua pia na nyingine iliyoonyesha gari aliloliona pia kwenye video ya hotelini.
Japokuwa picha hizi zilikuwa za muda mrefu nyuma, zilikuwa na manufaa. Zilimfanya Jona apate mwanga kidogo wa jambo lake.
Aligundua mke wa mheshimiwa alikuwa ana mahusiano na yule mwanaume kwa muda mrefu. Akagundua pia Arusha ndipo mahali wanapokuwa mara nyingi.
Zaidi akapata jina alitumialo mwanaume huyo. Japokuwa halikuwa halisi ila angalau litamsaidia mbali na lile feki alilotumia kujisajilia hotelini.
Mwanaume huyu alikuwa anajiita Black Nyokaa mtandaoni. Alilijua hilo kwa kutazama picha moja ya mke wa mheshimiwa aliyomwalika mwanaume huyo.
Basi Jona akazama tena kwenye profaili ya jamaa huyo apekue. Bahati isiwe kwake, hakukuta jambo la maana.
Hata picha haikuwepo, bali jina tu na akaunti tupu..
Alisonya akazima simu. Akaacha sasa kichwa chake kitafakari mambo aliyotoka kuyaona.
Alitafakari mambo hayo nusura apitilizwe na gari. Alikurupuka akashuka na kukwea gari lingine akayookea moja kwa moja kwenye msiba wa Bite.
Akiwa njiani alinunua kofia aliyoivaa kufunika uso wake usitambulike.
Alifika eneoni akakuta magari na watu wengi, ilikuwa ni siku ya kuaga kabla mwili haujasafirishwa kwenda nyumbani mkoa wa Morogoro.
Makazi ya Bite yalikuwa makubwa na ya kuvutia. Nyumba yenye uzio mzito mpana. Geti refu jeusi likiwa wazi kukaribisha waombolezaji.
Jona alitafuta eneo akaketi kwanza asome namna mambo yanavyoenda.
Lengo lake hapo lilikuwa ni kutafuta lolote jambo litakalomsaidia kwenye ung'amuzi wake juu ya kinachoendelea kumhusu Bite.
Alijua hatoweza kutoka hapo msibani mtupu, anaweza kupata mwanga angalau akajua nini chanzo cha mauaji ya Bite na kama kina mahusiano na ule mzigo wake alionao.
Penye wengi hapakosi jambo, walisema waswahili. Jona aliamini hilo na ndiyo maana yupo hapa.
Alitazamatazama huku na kule, na hatimaye akapata eneo lililokuwa kijiwe cha stori. Walikuwa wamejikusanya wanaume kadhaa hapo wakiteta.
Akajisogeza taratibu mpaka hapo. Akaketi akitega vema sikio.
Kwa muda mfupi aliokuwa hapo akagundua Bite alikuwa anamiliki kampuni ya magari. Kampuni hii haikuwa na muda mrefu tangu ianzishwe, na mtu aliyeshirikiana naye kuianzisha alishakufa.
Akiwa hapo bado anaendelea kuskiza, akamuona mwanamke fulani ndani ya hijabu. Alimtazama vema mwanamke huyu akamgundua ni yule anayemfuatilia - mwanamke aliyekuwa anataka mzigo wa Bite.
Haraka Jona akanyanyuka na kuhakikisha macho yake hayabanduki toka kwa mwanamke huyo, kila alipoenda ma kuongea na watu akawa anamtazama.
Haikuchukua muda mrefu akamuona huyo mwanamke akiwa anaongea na mwanaume fulani aliyekuwa amempa mgongo.
Mwanaume huyo alikuwa mrefu mwenye mwili wa kujengeka. Kichwa chake hakikuwa na nywele ila mwingi wa ndevu.
Jona alimtazama kwa umakini huyo mwanaume, kichwa chake kikamwambia mwanaume huyo ndiye yule aliyemuona siku ile nje ya nyumba yake wakiwa na Range Rover Sport nyeusi.
Alipata hamu ya kujua hawa watu zaidi, malengo yao haswa ni nini na ni wakina nani. Alihakikisha hawatoi kwenye mboni ya macho yake.
Aliwaweka kwenye uangalizi mpaka mwisho gari lililobebelea jeneza likiondoka. Watu hao wakajipaki kwenye gari lalo, Range Rover na kuhepa.
Jona akakodi pikipiki na kuanza kulifuatilia gari hilo kwa nyuma akilipa umbali kidogo.
Alilifuatilia mpaka maeneo fulani hivi ya Kawe gari hilo lilipoacha njia kuu ya lami na kushika ya vumbi.
Likatembea kwa dakika nane. Hapo sasa dereva kwa urahisi akajua anafuatiliwa. Alikuwa ni yule mwanaume pande la mtu akishikilia usukani.
Akamtazama mwenzake, mwanamke aliyeketi kushoto kwake, akamwambia: "Tumepata mkia."
.
.
.
.
.
. ***
LAKO JICHO!
***
Sent from my SM-J110F using
JamiiForums mobile app