ANGA LA WASHENZI --- 06
*Simulizi za series inc.*
Mwanamke akatazama nyuma, akaona pikipiki. Alijitahidi kuing'amua sura ya Jona lakini akashindwa, kofia ilimkinga.
Alisonya kisha akauliza; "Ni nani huyu?" Hakukuwa na mwenye majibu. Ila walijua tu hawapo salama, na ni lazima jambo lifanyike.
Dereva akadaka njia zingine za kuchepukia, ndani ya muda mfupi wakatokea baharini, wakasimamisha gari.
Jona naye akasimamisha pikipiki na kuwatazama. Mpaka hapo alikuwa amehisi huenda akawa ameshtukiwa.
Alijifanya anatazama maji ya bahari kwa muda kidogo kisha akakwea tena pikipiki na kupotea.
Pande lile la mtu na mwanamke aliyeongozana naye wakamtazama mpaka alipoyoyoma. Walishindwa kujua nini haswa lengo la huyo mtu, ambaye ni Jona sasa.
Walikaa hapo eneo la bahari kwa muda wa dakika kumi kusoma mambo. Walipojihisi wapo salama, wakaondoka zao, lakini wakiwa waangalifu sana.
Walisogeza chombo mpaka kwenye nyumba namba 89. Nyumba kubwa yenye uzio mrefu. Wakazama ndani na geti kufungwa nyuma yao.
Walijua sasa wapo salama. Waliketi sebuleni wakajadili kuhusu pikipiki ile iliyokuwa inawafuata. "Kuna haja ya kumfikishia taarifa, mkuu?" Akauliza pande la mtu ambaye ndani ya maongezi haya jina lake lilijiweka wazi, Kinoo.
Na la mwanamke lilikuwa Miranda. "Hapana, ni mapema sana," alijibu Miranda akiliza mifupa ya vidole vyake. Macho yake yalionyesha yupo mbali kifikra.
"Tunahitaji kujua kwanza ni nani anayetufuatilia na anahitaji nini," akaendelea kueleza Miranda. "Endapo tukimwambia mkuu kwa taarifa hizi robo robo, hatatuelewa, atatuona wazembe." Kukawa kimya kidogo. "Shida ni kwamba tuna maadui wengi, ni ngumu kubashiri," alisema Miranda. "Ni kweli," akaitikia Kinoo. "Ila tuna jukumu la kujua ni adui gani ameanza kunyoosha mkono tusije tukawaamsha wengine usingizini." Miranda akaitikia kwa kutikisa kichwa. Alinyanyuka akaendea chupa ya kinywaji, wiski, akaiweka mezani pamoja na glasi mbili. "Sasa yule mshenzi ameshaenda, nini sasa kinafuata?" Akauliza Kinoo akijinyoosha kuiteka glas ajipatie kinywaji. "Hali inakuwa ngumu zaidi," akajibu Miranda. Alimimina kinywaji akanywa kwanza fundo moja kupoza koo. "Nani kammaliza Bite? Unajua hilo swali linanitatiza sana," alisema Miranda akimtazama Kinoo. "Na kamuua kwasababu gani? Amekufa kabla hajatusaidia kupata ile picha na kutufafanulia." "Picha si ipo kwa yule mchoraji?!" Akasema Kinoo. "Umeipata?" "Hapana, ila angalau tuna uhakika ipo." Miranda akanywa fundo mbili. "Hata nguvu za kuitafuta hiyo picha zinaniisha," akasema akitikisa kichwa. "Hapana!" Kinoo akawaka. "Mimi naamini yule mchoraji atakuwa anajua jambo. Sema wewe ndiyo unazingua?" "Mimi?" "Ndio!" "Kivipi nazingua?" "Unamremba sana yule boya, tunajikuta watakatifu sana yani."
"Kwani wewe ulikuwa unatakaje, Kinoo? Tutengeneze kesi zingine? ... Si kila kitu chaendeshwa na mdomo wa risasi!" "Sasa kwa hiyo system tutapatia wapi hiyo picha? Tumekagua nyumba nzima hamna kitu! Ukimwomba akupe, hata kwa fedha, hataki! Sasa?" Miranda akashusha pumzi ndefu. Akanywa tena mafundo mawili. "Tujaribu tena," akashauri. "Unajua nini Kinoo, tatizo ni kwamba nataka kuepuka vyombo vya habari kabisa.
Nataka tufanye mambo haya kwa siri, tumalize kwa siri. Unajua mwenyewe namna gani hii ishu ilivyo ngumu." "Una maanisha nini?" "Endapo hili jambo la huyu mchoraji likivuma, basi wale wabaya wetu watalifahamu, watajua kuna jambo na watalifuatilia.
Huoni kama hapo itakuwa nongwa? Wakifuatilia wakajua ni kuhusu picha, basi watatusumbua zaidi. Watataka kujua kilicho kwenye picha.
Kama waliweza kummaliza Bite kuficha siri, vipi wakisikia kuna jambo litakalovujisha neno?" Kukawa kimya. Kinoo alimalizia kinywaji chake glasini kisha akalaza mgongo kitini. "Miranda," akaita. "Mimi bana nakuachia hili jambo mwenyewe. Wewe utakavyoona, sawa. Utantaarifu." "Usijali," alisema Miranda kisha akanyanyuka. "Leo hatuendi?" Aliuliza. "Wapi?" Kinoo akatoa macho. "Nawe acha uoga, unadhani ni wapi?" Akaangua kicheko. "Ni klabu tu hapo!" "Siendi," Kinoo akajibu na kuongezea: "Hivi wewe hujachoka enh? Siku nzima msibani na bado unataka kwenda klabu! We kiboko."
Miranda akatabasamu. Akanyanyua chupa kubwa ya wiski na kumiminia mdomoni. "Tena usinikumbushe huo msiba wa kis*nge. Nimekaa hapo kutwa nzima na wala sijapata chochote. Nimepoteza muda tu!" Kinoo akatabasamu. Akanyanyuka na kujinyoosha. "Maisha ndivyo yalivyo. Si kila mara wapata, la hasha! Kuna muda wakosa na kuna muda wapata. Cha msingi ni kutokata tamaa. Tuendelee kupambana." "Ila roho inaniuma sana, Kinoo," akasema Miranda akipiga kifua chake ngumi. "Kwanini?" "Kila mara tunazidiwa hatua, kwanini? Ina maana sisi ni wajinga na wazembe kiasi gani?" "Hapana, Miranda. Kila mbwa ana siku yake. Kuna siku wataingia kwenye anga letu. Anga la washenzi. Hakika watajuta!" Kinoo aliposema hivyo akapiga mihayo. Miranda alitabasamu na kumtaka aende akapumzike. "Usiku tuna kazi ya kufanya, bila shaka unakumbuka," akasema Miranda. "Tena?" "Ndio, kwani iliisha?" "Poa, mida!" Kinoo akatoka ndani, Miranda akaingia chumbani.
Kinoo akaelekea nyuma ya nyumba ambapo kulikuwa kuna chumba kikubwa kilichojitenga ambacho kilifungwa na mlango wa bati.
Akafungua mlango huo kwa kutumia funguo aliyoitwaa dirishani. Akatoa pikipiki moja matata, Ducati Monster nyekundu modeli ya 2016 aliyotia moto na kuhepa nayo.
Alivalia kofia ngumu na uso wake ukazibwa na kioo cheusi cha kofia hivyo ikawa ngumu kumng'amua uso.
Lakini Jona alimjua mwanaume huyo upesi. Alikuwa amejibanza kwenye jengo moja karibu sana na jengo alimotoka huyo mwanaume, yaani Kinoo.
Lakini pia na nguo alizovaa Kinoo zilimfanya Jona, mwanaume mwenye macho mabovu ndani ya miwani, amkumbuke na kumtambua kwa usahihi.
Alimtazama Kinoo anavyoyoyoma, kisha akaurudisha uso wake getini mwa jengo. Akatazama kwa muda pasipo kuona jambo.
Akaamua kuondoka, ila akiapa kurudi na kufanyia jengo hilo upelelezi zaidi. Alitaka kujua uhusiano wa hao watu na kifo cha Bite,na picha pia.
Ilimradi sasa alishajua makazi yao, kwake hii ni hatua muhimu kuelekea kupata majibu yake. Hivyo hakupoteza muda.
Akajirudisha nyumbani asiende kazini. Alikoga na kula kisha akapumzika kidogo kabla ya kuanza kuchora picha kadhaa kwenyw makaratasi yake marefu.
Leo hii hakuchorea chumbani, bali sebuleni. Alijivika earphone masikioni akisikiza muziki laini huku akitenda.
Macho yalitazama katatasi, mkono wake ukienda kwa ustadi. Alikuwa anarejelea kwenye kumbukumbu zake, na baada ya muda picha ya mtu sasa ikaonekana vizuri.
Alikuwa ni mwanaume mrefu mwenye mwili mpana. Alikuwa amevalia shati lililobana mwili. Kichwa chake hakikuwa na nywele, ila ndevu lukuki. Alikuwa ni Kinoo! Hata mtoto mdogo angekueleza hivyo kwa kutazama tu mara moja.
Kama haitoshi, akachora pia na picha ya Bite vilevile kama alivyoichora awali. Alipomaliza akaketi na kuanza kuitazama picha hiyo kwa umakini kama fumbo.
Hakudumu hapo muda mrefu, simu ikamshtua. Akaichomoa mfukoni na kutazama. Ulikuwa ni ujumbe toka kwa Nade.
Kabla hajaujibu ujumbe huo, akajiuliza ni namba ngapi zilizotunzwa ndani ya simu hiyo. Ni mara ya pili sasa amekuwa akiona majina yanatokea katika njia ya kumrahisishia kufahamu.
Ina maana namba hizo zilitunzwa kwa ajili ya matumizi yake? Ndio, akili yake ikamjibu.
Ile simu alikuwa ameandaliwa, na hata watu wa kuwasiliana naye walishaainishwa. Alitumia muda wake kuperuzi majina yaliyotunzwa simuni, akayakuta manne tu.
1. Mh. Eliakimu Mtaja
2. Mama Mdogo (Kinondoni)
3. Nade
4. Shangazi (Kimara)
Ikamshangaza kidogo. Alipewa simu hiyo akiwa hamjui yeyote kati ya hao, labda tu Mheshimiwa.
Ina maana watu hao waliwekwa simuni kabla hata hajaipokea? - Hadi Mama Mdogo na Shangazi wa mke wa mheshimiwa!
Alipuuzia maswali hayo akauendea ujumbe wa Nade na kuufungua. "Habari?" Ujumbe uliuliza. "Njema," Jona akajibu. Hata salio lilikuwa kedekede kwenye simu. "Kuna kitu umepata?" Ujumbe ukaingia. "Ndio," Jona akaandika, ila kabla hajajibu akasita. Akaufuta ujumbe huo na kuuandika mwingine. "Hapana, bado." "Kweli?" "Ndio." Kimya kidogo. "Haya sawa. Naomba unishirikishe utakapopata jambo. Hata kama kidogo. Sawa?" "Sawa." Jona akaweka simu chini. Alistaajabishwa na namna alivyoulizwa kuhusu upelelezi wake ndani ya masaa machache tu.
Alijiuliza ni hofu ama hamu iliyosukuma maswali hayo.
Hakutaka kuumiza kichwa chake zaidi. Alifunga zile picha alizokuwa amechora kisha akazipeleka chumbani.
Baadae kwenye majira ya usiku akiwa yupo kitandani, na tayari amejishindilia kilevi, akazama kwenye mtandao wa Facebook na kuanza kuperuzi akaunti ya mke wa mheshimiwa.
Akafungua akaunti yake upesi akiipa jina la Giovanni Lacatte. Akaweka taarifa bandia akijinadi anaishi Italia na anahusika na mitindo mavazi.
Akarusha picha kadhaa za wanawake wanamitindo. Baada ya hapo akadukua akaunti mifumo na mara punde akawa ana wafuasi wengi waliomfuata.
Wafuasi laki tatu! Wafuasi hawa wote walikuwa feki. Ila usingeweza kutambua mpaka uanze kuwatazama.
Alikuwa ni mtu mmoja tu aliyezidishwa mara elfu!
Jona alipoona kila kitu kipo sawa, akamuomba urafiki Mariam Jullian, mke wa Mheshimiwa.
Haikupita muda mrefu, kabla hajaanza kusinzia, ombi lake likakubaliwa. Akiwa amefungua jicho moja, akamtumia Mariam ujumbe.
Waliwasiliana wakitumia lugha ya kiingereza wakijuliana hali. Jona akamlaghai amempemda na angependa kumtumia kutangazia mavazi yake.
Jambo hilo likamvutia sana Mariam. Akaingia mkenge akitaka kufanya kazi hiyo. Ila alishikwa tahadhari, akauliza kama kutakuwa kuna malipo yoyote anayotakiwa kufanya.
Jona akamtoa shaka. Lakini pia kutengeneza mazingira ya 'kiprofesheno' hakutaka kuzoeana ghafla na 'mteja' wake, akamwambia atamtafuta tena siku za usoni.
Mariam akiwa mwenye furaha, akaridhia na kuaga.
Jona alikuwa sasa anasinzia mno. Akaiweka simu kando na kulala. Dakika tano kupita, akashtuka. Alisikia sauti ya mlango wa geti.
Akakurupuka na kusimamisha masikio.
.
.
.
.
. ***
LAKO JICHO!
***