Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

*JOANA ANAONA KITU USIKU -- 06*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA …
Wote wakamuunga mkono na kumwacha Jona mpweke.

“Kama angelikuwa mlozi usingelikuwa hai hata leo, angekwishakumaliza zamani za kale!” kaka mkubwa akajazia.

Pasipo kujua maongezi hayo yote yalikuwa yanamfikia mama aliyekuwa chumbani amejilaza kitandani.

Mama akaapa kummaliza Moa kabla hakujakucha.

ENDELEA…

Katikati ya usiku wa manane, ndani ya chumba chenye giza totoro, Moa anakurupuka baada ya kuhisi kuna mtu ndani.

Anaangaza kushoto, kulia, juu na chini hamna kitu! Akashusha pumzi ndefu na kuurejesha mwili wake juu ya kitanda.

Hakulala tena kwa muda, akakurupushwa kwa sautiya vishindo vya miguu! Akatoa macho yake kuangaza, hola!

Mwili ulikuwa unamsisimka vinyweleo vikimsimama. Macho yalimtoka. Moyo ukipiga kwa nguvu.

Alihisi kabisa kuna mtu, ila hakujua yupo wapi! Akapiga moyo konde kufuata soketi awashe taa. Akiweka nadhiri kulala na mwanga huo mpaka asubuhi.

Aliifikia soketi, ila aliponyoosha mkono aibinye, kufumba na kufumbua akatokea mtu! Na ghafla akakamata mkono wake.

"Ni muda wako wa kufa!" Akasema mtu huyo. Sauti ilikuwa ya kike. Sauti ilikuwa ya mama yake!

Moa akahisi amepitishwa kwenye dimbwi la barafu. Aliusikia mwili wake umekuwa wa baridi. Tumbo linafukuta na jointi zimekwisha nguvu.

Kabla hajafanya kitu, akakabwa shingo na kunyanyuliwa juu kama mtoto. Akahaha kusaka pumzi. Macho yakamtoka miguu ikitapatapa.

Alipambana kujiokoa kwa mikono yake miwili lakini hakufua dafu. Mkono uliomkaba ulikuwa una nguvu ajabu. Na ulikuwa umepambwa na bangili lukuki.

Japo ni giza kiasi cha kutoziona, bangili hizo zilikuwa zinasikika zikigonganagongana wakati mnyongaji akihangaika na mhanga wake.

Sasa hapa nakufa! Moa akakiri. Katika harakati za kupapatika, bahati akarusha teke, likamkita mnyongaji na kumwangusha chini.

Moa akashangaa kwanini hakuwaza kufanya hivyo mapema. Alikohoa na kuhema kwanguvu kana kwamba kuna mashindano.

Akapaza sauti kuita kaka na baba yake waje kumsaidia, anauawa. Loh! Hakukuwa na wa kumsaidia.

Watu hawa ni kama walilala usingizi wa kifo. Moa alipaza na kupiga yowe lakini hamna hata aliyegeuka wala kuguna!

Moa akastaajabu.

Akadhani nyumba nzima imedhamiria kumuua. Mnyongaji aliangua kicheko kikali akinyanyuka toka chini, akamwambia:

"Hamna wa kukuokoa, Moa. Tupo mimi na wewe tu katika ulimwengu wetu tofauti."

Moa akakimbilia mlango. Akahangaika aufungue atoke ndani, ila hakufanikiwa. Mlango ulikuwa umelokiwa.

Kama lini? Akatahamaki. Hajawahi kuufunga mlango usiku akiwa analala!

Mnyongaji akaangua tena kicheko. Akacheka na kucheka kweli. Kicheko ambacho huwezi bashiri ni cha furaha ama hasira.

Moa akazidi kuhofia. Akatazama huku na huko. Ni dirisha tu ndilo akaona linaweza kumuokoa. Haraka akalikimbilia na kujitupia dirishani.

Hakujali kama ataumia wala kuchanwa na vioo. Kitu kilichokuwepo kichwani ni kumtoroka mnyongaji tu. Kumkimbia mama yake kwa usalama wa uhai wake.

Akavunja vioo na kudondokea nje. Alipata majeraha ya kuchanwa chanwa ila hakuyasikia. Aliamka upesi akakimbia.

Huku nyuma mnyongaji akapiga kelele kali. Sasa hivi hazikuwa za kucheka, bali hasira. Ilieleweka amekasirika.

Moa alikimbilia mbali na nyumbani, huko mtaani. Hakuchoka kukimbia. Alikimbia zaidi na zaidi mpaka alipojikuta ufukweni mwa bahari.

Ulikuwa ni usiku wa manane. Mitaa ilikuwa kimya, wala hakuna watu nje.

Aliinama akishika magoti, akihema kwanguvu. Jasho lilikuwa linamtiririka haswa. Mwili umechemka.

Alipovuta pumzi ya kutosha akaanza kujongea kwenda zake mbele kwa mategemeo kwamba ataona watu. Jiji zima halilali kwa wakati mmoja.

Hakutembea umbali mrefu, mara akapoteza uwezo wa kuona. Alijikuta yupo gizani kana kwamba umeme umakatika. Alihofia mno. Kufumba na kufumbua, akajikuta ndani ya maji ya bahari.

Hakujua amefikaje. Kuna mtu alikuwa anamvuta, ila hakumuona na hakujua anamvutia wapi. Alipojiona yupo ndani ya maji ndiyo sasa akajua alikuwa anavutiwa huko.

Hakupewa hata muda wa kujitetea. Ni kama vile kimbunga alivyosombwa.

Akajitahidi kuogelea aokoe uhai wake. Lah! Hakufanikiwa. Alikabwa shingo na kuvutiwa kwenye sakafu ya bahari.

Akatapatapa. Akanywa maji akitafuta hewa!

Alichoka kurusha mikono na miguu. Hakufanikiwa kwenda popote pale. Hakusogea hata hatua moja. Taratibu akaona uhai wake unapotea.

Baada ya muda kidogo, mwili wa Moa ukaonekana juu ya maji ukielea. Tayari uhai hamna!

Mnyongaji akapotea.


***


Palikucha kama kawaida. Mama alikuwa wa kwanza kuamka akiwa na akili zake timamu na nguvu maradufu.

Aliandaa chai na kuiweka mezani kisha akatoa beseni kubwa la nguo akilenga kufua. Jua lilikuwa linamulika na hakukuwa na dalili ya mvua, hali ya hewa nzuri kwa ufuaji.

Muda mfupi mbele, baba naye akaamka, akanywa chai na kutoka ndani. Akaaga anaenda zake shamba, kuna mambo anataka kuyaweka sawa. Punde, napo kaka wa kwanza akaaga na kuondoka, anaenda kwenye mihangaiko yake.

Mama akawaaga kwa kuwakumbatia na kuwapa mabusu. Akaendelea na kazi yake ya kufua mpaka hapo alipomaliza na kwenda ndani alipobisha hodi kwenye milango ya watoto wake waliobaki.

“Amkeni mnywe chai. Kumekucha!”

Ajabu, mlango wa chumba cha Moa ukafunguliwa, Moa akatoka.

Alikuwa ni mwenye afya njema, asiye na jeraha wala alama yoyote mwilini. Alijinyoosha mwili kisha akaenda kunawa uso na kuoga akapate kifungua kinywa.

Lakini mtu huyu si amekufa! – Amefia huko baharini baada ya kunyongwa.

Ni nini anafanya hapa?

Kama haitoshi hata huko chumbani, kulikuwa tulivu. Dirisha lilikuwa zima ilhali lilipasuliwa usiku. Kila kitu kilikuwa mahala pake, kilikuwa kimepangwa, na kipo sawa!

Ni nini hiki?

“Tupo mimi na wewe tu katika ulimwengu wetu tofauti.” Maneno ya mama sasa yalianza kuleta maana. Watu hawa walikuwa kwenye ulimwengu wao na si huu tunaoujua.

Walikuwa kwenye ulimwengu mwingine tofauti. Ulimwengu ambao hakuna anayesikia kelele zako, wala anayejali jitihada zako.

Ulimwengu ambao upo wewe na adui tu! Ukimalizwa katika ulimwengu huu, umemalizwa katika ulimwengu wa nyama na roho pia. Tunayekuona ni kivuli tu.

Moa hakuwa Moa tena.

Moa hakuwa …


***


Siku, wiki na mwezi mmoja ukapita.

Notisi ilitoka na taarifa zikasambaa kwenye mitandao ya kwamba chuo kinafunguliwa na wanafunzi wote wanatakiwa kuripoti kwa mujibu wa tarehe iliyokuwa imeainishwa.

Wanafunzi wakapashana habari, wakaanza kujiandaa kwa ajili ya masomo. Wachache walikatisha masomo yao kwa hofu ya yale mauaji. Yani walivyoondoka, hawakurudi tena.

Joana akiwa pamoja na rafiki na meti wake, Lisa Moan, walikutana uwanja wa ndege kwasababu ya mawasiliano. Walikumbatiana na kupeana mabusu kwa hamu ya kutoonana muda mrefu.

Wakiwa ndani ya taksi kuelekea chuo, Lisa akamuuliza Joana kuhusu Moa.

“Sijui anakuja lini. Kwa muda kidogo sijawasiliana naye,” Joana akajibu akipandisha mabega. “Sijui ana shida gani. Niliona niwe mvumilivu pengine nitaonana naye huku chuo.”

“Vipi kama usipomuona?”

“Nitatoroka niende kwao. Labda anaweza akawa amepatwa na matatizo.”

Wakafika chuo na kupanga vitu vyao ndani ya chumba. Baadae usiku, majira ya saa nne, Lisa akiwa amelala na Joana anaangaza tarakilishi yake kutazama tamthilia, hodi ikaita.

“Nani?” Joana akapaza sauti.

“Moa,” sauti ikajibu kwa nje. “Nifungulie haraka kabla sijaonekana na mlinzi.”

Joana akajikuta anatabasamu. Haraka akaweka mashine yake pembeni na kukimbilia mlangoni.

Akafungua na kuangaza, hakuona mtu!


*NI NINI KINATOKEA?*

*MOA HALISI YUPO WAPI?*

*JOANA ATAKUTANA NA MOA? MAUAJI YATAKOMA?*

Usikose sehemu ijayo.

*Simulizi za series*


Sent from my SM-J110F using JamiiForums mobile app
 
Back
Top Bottom