*ANGA LA WASHENZI (MSIMU WA PILI) -- 03*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
"Tā xiǎng yào duōshǎo?" (Anahitaji kiasi gani?) Sauti ikauliza simuni.
"Bǎ jiàgé fān bèi nàme gàosù nǐ zěnme xiǎng!" (Ongezea mara mbili alafu sema unatakaje!) Mtumishi akajibu.
"Méiguānxì!" (Sawa!) Sauti ikamjibu simuni.
ENDELEA
Baada ya kuteta huko na kukubaliana, mtumishi akawasha chombo chake na kutimka. Sheng akatabasamu akiwa ofisini. Sasa mambo yalienda kama alivyotarajia.
Akajilaza kwenye kiti na kunyanyua simu kumpigia mhasibu, akamwambia amletee tena milioni mia moja. Alipoirudisha simu mezani, akatabasamu tena. Hakika hakutegemea kama siku hiyo ingeisha vizuri.
**
Bado mpaka saa moja usiku ...
"Tuondoke, muda umewadia," akasema Jona akimtazama Marwa. Walikuwa wameketi ndani ya sebule ndogo ya kawaida lakini ikiwa imepambwa kwa usafi wa hali wa juu.
"Hatumngojei baba?" Marwa akauliza.
"Muda umeenda, Tutakuja siku nyingine," Jona akashauri na mara kidogo akatokea mama mtu mzima, makadirio miaka sitini kasoro kidogo. Alikuwa mwembamba mwenye nywele za mvi, lakini akiwa mwenye nguvu na uchangamfu.
Akaketi kitini.
"Naona baba amechelewa sana leo," akasema. "Sijui atakuwa amepitia wapi!"
"Usijali, mama," Marwa akamtoa hofu. "Tutakuja siku nyingine kumwona. Kwa sasa tunaomba tukukimbie."
"Mbona mnawahi hivyo na mmekuja muda si mrefu?" Mama akashangaa. "Kaeni mumngoje kidogo. Nadhani ndani ya muda mchache, atawasili."
"Kuna mahali tunatakiwa kupitia mama," Jona akaeleza. "Tungekaa mpaka usiku mzito."
Mama hakuwa na budi, akawatakia safari njema lakini kabla hawajaondoka akahitaji aongee kidogo na Marwa. Jona akatangulia kwenda nje.
"Vipi? Mbona unaondoka haujatupatia dawa?" Mama aliuliza, na kuongezea. "Unajua imebakia kiasi kidogo sana!"
Akafungua fundo lake la kanga na kutoa kachupa kadogo kumwonyeshea.
"Unaona?"
Ndani ya kachupa hako kulikuwa na kama katone hivi ka maji ambacho kukaona ilihitaji umakini wa hali ya juu.
"Nimeona, mama," Marwa akasema kwa upole. "Nitakuletea tu."
"Kaburini?" Mama akastaajabu. "Unadhani haka katatuweka hai mpaka lini, Marwa?"
Marwa hakuwa na la kusema, akatazama chini.
"Kuna shida gani, Marwa? Naomba uniambie. Dawa imeisha?"
"Hapana."
"Sasa nini shida? Niambie mwanangu."
Marwa akajikuta macho yake yanakuwa mekundu. Sauti ya mama yake ilikuwa inatafuna moyo wake. Alitamani kumwambia hayupo tena kule apatapo dawa lakini alihofia. Angeweza kumuua mamaye kwa presha.
Akamtia tu moyo ampe kitambo kidogo, atakuwa ameshaleta dawa hapo nyumbani.
"Kama kuna shida tuambie," Mama akamwambia akimshika bega. "Sisi ni wazazi wako, hauna mtu mwingine wa kumwaminini."
"Hakuna shida mama," Marwa akakazana. Alikaza uso wake usionyeshe majonzi. Akamkumbatia mama yake na kumuaga. Lakini alipogeuka tu chozi likamshuka haraka. Moyo wake ulikuwa unamuuma. Alikuwa anashuhudia wazazi wake wakifa mbele ya macho yake.
Alienda kukutana na Jona wakaenda zao. Hakusema jambo mpaka wanafika nyumbani.
"Marwa, it's going to be ok!" Jona akamfariji. "Tutapata antidote tu."
Marwa akajikuta anadondosha chozi. Akamtazama Jona na kumwambia shida si kuipata, bali muda. Antidote aliyoiona inawatosha kwa usiku huo wa leo tu. Kesho yake hawatakuwa na cha kutia mdomoni, wataanza kuteseka mno.
"Kwa umri wao ilibidi wawe wamepumzika, si kupitia shida hizi," alisema Marwa kwa uchungu.
Jona akamtazama kwa huruma. Baada ya mafikirio kidogo, akamuuliza:
"Unajua antidote hiyo ilipo?"
"Kivipi?"
"Unafahamu mahali wanapoihifadhi antidote hiyo kule kwa Sheng?"
"Hapana," Marwa akajibu akitikisa kichwa. "Lakini nafahamu ilipo maabara."
"Si mbaya," Jona akateta. "Basi jiandae saa tano tunaenda huko!"
"Wapi?" Marwa akatahamaki kwa woga.
"Ilipo antidote!" Jona akafafanua. Na asingoje maelezo zaidi, akaenda zake chumbani. Marwa akabaki anamtazama kwa mshangao.
**
Baada ya kunyata kidogo,
"Upande huu!" Marwa akaelekeza kwa sauti ya chini. Alikuwa amevalia nguo nyeusi na kinyago usoni. Na Jona pia.
Walikuwa tayari wameshazama kwenye ngome ya Sheng katika majira haya ya saa sita usiku. Lengo lao likiwa moja, kwenda kuinyaka antidote ndani ya maabara.
Wakatembea tena kwa utaratibu wakichukua kila tahadhari, walipokaribia maabara, wakamwona mwanaume mmoja aliyebebelea bunduki kubwa ndefu mkononi. Jona akaitambua ni SMG.
Mwanaume huyo alikuwa ni mlinzi. Alikuwa ameketi kwenye kibaraza cha jengo la maabara akichokonoa meno yake kwa kijiti.
Jona akampanga Marwa.
"Utatoka na kunyata kuelekea upande huu," akamwonyeshea upande wa kushoto. "Lazima atakutazama na aidha anaweza kukuita. Lakini kabla hajafanya kitu, atakuwa tayari yupo mikononi mwangu."
Marwa hakupewa muda wa kufikiri, Jona akaanza kutekeleza mpango. Haraka akanyanyuka na kutembea upesi kuelekea upande wa kulia, lakini akifanya hayo miguu yake haikutoa sauti hata kidogo.
Basi muda mchache, mlinzi akamwona Marwa akikatiza, haraka akanyanyuka na kuishikilia vema silaha yake. Akapaza sauti:
"Wewe nani?"
Marwa akasimama na kumtazama.
"Mimi? Mimi naitwa Marwa!"
"Marwa?" Mlinzi akatahamaki. Hakuwa analijua jina hilo katika orodha ya walinzi. Akamtaka Marwa anyooshe mikono juu na kupiga magoti.
"Sina tatizo na wewe," Marwa akasema akishuka chini. "Mwenye tatizo ni huyo aliyepo nyuma yako."
Haraka mlinzi akageuza shingo kutazama. Mara shingo hiyo ikadakwa na kuendelezewa safari. Akadondoka chini kama mbuyu.
Wakamficha, kisha chap wakaufuata mlango mzito wa maabara. Ulikuwa ni mlango wa chuma wenye kitasa kipana. Wakajaribu kuufungua pasipo mafanikio.
"Jona, inabidi tukachukue funguo!"
"Wapi?"
"Stoo. Kule wanapozihifadhi."
"Hatuna muda huo Marwa. Mlinzi mwingine anaweza kutokea akagundua uwepo wetu. Na endapo akirusha risasi moja tu, atakuwa keshatibua mambo."
"Sasa tunafanyaje?"
Jona akavua mkanda wake na kuchomoa kichuma cha kushikilia vitundu mkandani. Akakipinda kichuma hicho kwa mdomo, akitumia sekunde kadhaa kama ishirini, alafu akakidumbukiza hicho kichuma ndani ya kitasa.
Akapeleka mkono kushoto na kulia, mara mlango ukalia - kat! Wakajaribu kuufungua. Hola! Mlango haukufunguka.
"Shit!" Jona akalaani.
Akakirepea tena kile kichuma kwa kukibadili muundo wake, alafu akajaribu tena. Mlango ukalia tena - kat! usifunguke.
"Jona, tunapoteza muda. Twende kule," Marwa akashauri.
"Hapana, Marwa," Jona akatikisa kichwa. "Mlango huu umelokiwa mara tatu, utafunguka tu ... ngoja uone ..."
Jona akachokonoa tena kitasa, mlango ukalia tena - kat! Na mara hii walipougusa ukatii amri! Wakazama ndani.
Maabara ilikuwa kubwa. Wakitumia kurunzi kuangaza, wakaanza kupekua upesi upesi. Wakachukua dakika nyingi humo. Baadae ndipo wakaona chumba kidogo ndani ya maabara kikiwa kimeandikwa antidote mlangoni.
Jona akafanya ufundi kufungua kitasa kisha wakazama humo ndani, baada ya muda kidogo wakatoka Jona akiwa amebebelea flask - chupa ya kioo yenye mdomo mwembamba chini ikiwa imejitanua mithili ya pembe tatu. Ndani ya chupa hiyo kulikuwa na kimiminika mithili ya maji.
Kwa haraka wakajongea kuufuata mlango wa maabara, lakini kabla hawajaufikia, Marwa akajikwaa. Mguu wake ulidumbukia ndani ya vifereji vidogo vya kutolea uchafu, akajikuta yu chini kwa kukosa namna ya kujiokoa!
Kabla hawajafanya jambo, ndani ya muda mfupi, wakasikia chupa kadhaa nazo zikidondoka na kusababisha kelele!
Mara huko nje, sauti nzito ikauliza:
"Nani huyo?"
Alikuwa ni mjibaba wa miraba minne, mkononi akiwa ameshikilia bunduki ndogo.
Mwili wake mpana kama gogo ulikuwa umesitiriwa na nguo nyeusi. Chini ana buti kubwa rangi ya kaki. Kichwa chake kinameremeta kwa kukosa nywele. Na mdomo wake ukiwa umefunikwa na mustachi mzito wenye afya tele.
Jibaba hilo likalalama.
"Yani hawa panya sasa naona wananipanda kichwani!"
Likapiga hatua nzito kuufuata mlango lakini kabla hajaugusa, akauliza:
"Isak yupo wapi?" Akitazama huku na kule kisha akalalama;
"Hawa panya watamaliza vitu vyote humu ndani. Experiment gani hizo za kila siku kutumia panya!"
Akasonya.
"Hakuna mnyama namchukia ka --"
Akashtuka kuona mlango una upenyo. Asiamini macho yake akausukuma kwa kidole, mara ukafunguka na kuachama. Akapata wasiwasi. Akashikilia vema bunduki yake na kuzamisha mkono ndani, akabofya switch, taa zikawaka!
Akaangaza akinyooshea bunduki yake huko. Kwa mbali akona chupa kadhaa zikiwa zimepasuka. Akapiga hatua kusonga.
Pembeni ya chupa hizo zilizopasuka, kwa chini ya meza za sementi zilizokuwa zimejengwa humo, alikuwa amelala Marwa.
Alikuwa ameubana mdomo wake kwa nguvu akijitahidi kutulia lakini alikuwa anasikia maumivu makali sana. Chupa zile zilizoanguka zilimrushia kemikali usoni na alikuwa anahisi kuungua!
**