Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

*ANGA LA WASHENZI (MSIMU WA PILI) -- 01*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Alipomaliza kula akalipia na kunyookea ubalozi wa China. Humo ndani hakumkuta balozi bali msaidizi wake. Wakateta kwa lisaa limoja kabla Jona hajatoka ndani ya jengo hilo.

Kitendo cha kutoka tu, ikachukua dakika mbili, Sheng akaarifiwa juu ya ujio wa Jona. Na shuku zake zote alizozileta ubalozini!

ENDELEA

Sheng akaweka simu yake chini kisha akashusha pumzi ndefu akiwaza. Akawasha sigara yake kubwa na kuinyonya akijizungusha na kiti kwenda huku na kule.

Jona ... Jona ... Jona ... kichwa chake kiliimba hili jina. Inawezekanaje mwanaume mmoja akamwangaisha na kumkosesha amani kiasi hiki? Mtu mmoja? Chawa mmoja kwenye nywele?

Hapana! Akang'ata sigara yake na kuitafuna kwa hasira. Huu ulikuwa ni udhalilishaji wa hali ya juu! Na hauvumiliki. Kabla hajanyanyua simu yake kupiga, mara ikaita, akapokea.

Walikuwa ni vijana wake waliopo Nairobi wakimuuliza kama kuna haja ya kuendelea na zoezi lao la kummaliza bwana Kamau Githeri ama waachane naye kwa sasa.

Akawaamuru warudi nyumbani kwanza. Hali si shwari. Lazima bwana Kamau atakuwa analindwa kwa hali ya juu, na macho ya wanausalama yatakuwa kwake muda mwingi tangu tishio hilo.

Aliposema hayo, akawataka vijana warudi nyumbani, kuna kazi ya kufanya. Tena warudi upesi mara moja!

Akaweka simu chini na kutumbukiza mikono mfukoni. Akafuata dirisha kubwa lililopo ofisini mwake alafu akatazama nje akitafakari.

Baada ya kama dakika kumi na tano, akampigia simu mhasibu na kumuagiza atenge shilingi milioni mia moja kwa ajili ya oparesheni kabambe. Majira ya jioni kabla hawajafunga ofisi kuondoka, ahakikishe pesa hiyo inafika ofisini kwake pasipo kukosa.

**

"Hodi!"

Ilibishwa mara moja na kuitikiwa. Ni ndani ya nyumba ndogo ya wastani ipatikanayo maeneo ya Kimara, Dar es salaam.

Kwa kuitazama tu, nyumba hii ilikuwa na takribani vyumba vitatu. Na kama kuna cha zaidi basi ni jiko, choo na bafu. Jona alipekua kwa macho ya haraka akingoja afunguliwe mlango.

Mazingira ya hapo hayakuwa tulivu sana. Si kwasababu ya kelele toka ndani, lah! Bali toka kwa majirani. Uzio kuzunguka nyumba hiyo ulikuwa umejengwa ndani ya muda mfupi. Na kwa Jona alidhani pengine ni sababu ya makelele hayo ayasikiayo, mwenye nyumba alikuwa anataka kujitenga kidogo na muingiliano mkubwa ndani ya eneo hili.

"Karibu," alisema mwanamke mmoja mnene mweupe aliyevalia dira akikatisha uchambuzi wa Jona kichwani. Mwanamke huyu kwa makadirio ya Jona alikuwa na miaka 45 - 50. Na ndiye shangazi yake Miriam.

"Ahsante." Jona akaingia ndani wakasalimiana.

"Nimemkuta Miriam?"

"Ndio, yupo anaoga. Baada ya muda mfupi atakuwa hapa."

"Ahsante. Nitangoja."

"Unatumia kinywaji gani?"

"Maji yanatosha.'

Mwenyeji akamletea Jona maji ya kunywa na kisha akaketi.

"Wewe ndiye Jona?"

"Ndio, ni mimi."

"Naomba umsaidie mwanangu, tafadhali. Naomba sana baba. Hana amani wala raha. Amedhoofu mno. Wale washenzi wamemchakaza haswa!"

"Amekuambia nini kuhusu hao watekaji wake?"

"Mengi tu, nadhani atakueleza mwenyewe kwa undani. Ana taarifa za kutosha kabisa zitakazowasaidia kuwatia nguvuni."

Jona akamiminia maji kwenye glasi na kunywa mafundo matatu akipeleka macho yake hapa na pale. Ndani ya muda mfupi akagundua mama huyo ni mjane kwa kuona picha za mumewe zikiwa zimetundikwa ukutani na maandishi ya kumtakia kheri huko aliko.

Zaidi akafahamu mama huyu ajihusisha na shughuli za utengenezanaji bidhaa kwa mikono baada ya kuona vyeti kadhaa za maonyesho na tuzo za utambulisho pia toka SIDO.

"Ulikuwa unayafahamu mahusiano kati ya Miriam na huyo mwanaume aliyemteka?" Jona akauliza.

Shangazi akanyamaza kwanza kidogo. Kuna kitu kilimkaba kuropoka. Alikodoa macho yake na kuyafumba, akang'ata lips.

"Kusema ukweli nilikuwa nayafahamu, japo sikuyaridhia kwakuwa Miriam alikuwa tayari ndani ya ndoa. Japo aliniletea mashtaka kadhaa toka kwa mumewe, sikuona haja ya kumshauri aachane naye, sisi ni wakristo, ndoa ni moja tu."

"Huyo mwanaume ashawahi kuja hapa? Mnajuana?"

"Hajawahi kufika hapa japo namjua kwa sura."

"Ulimwonea wapi?"

"Kwenye simu ya Miriam."

"Miriam alivyopotea ulikuwa unafahamu alipo?"

"Nilikuwa najua yupo Arusha lakini sikujua haswa ni wapi."

"Kwanini Miriam ameamua kuja kwako baada ya kutoka Arusha na si kwenda kwa maa mdogo wake aishiye Kinondoni?"

Kabla shangazi hajajibu hili, Miriam akafika. Alitabasamu kumwona Jona, tabasamu la matumaini. Akamsalimu na kumkaribisha. Shangazi akawapisha.

Pasipo kuchelewa wakaanza maongezi yao. Miriam kwa hisia sana akaeleza namna alivyokuwa anatendewa mpaka alivyojinasua. Akamweleza Jona nini Nyokaa anafanya na wapi anapatikana.

Habari hizo zikamtosheleza Jona. Sasa akapata wapi pa kuanzia kumuwinda Nyokaa. Kufanikisha hilo, Miriam akamuahidi kumuunga mkono kwa asilimia zote, lakini pia hakusita kumpatia tahadhari.

"Kuwa makini, si watu wazuri kabisa. Hawaoni shida yoyote kumuua mtu kisha wakamnyofoa viungo vyake na kwenda kuviuza."

Hili kwa Jona lilikuwa jipya. Hakujua kama Nyokaa, mbali na biashara ya madini, anafanya pia na biashara ya viungo vya binadamu akivisafirisha kwenda Afrika ya kusini.

Kwasababu hii basi, amekuwa akiteka nyara watu na kuwahifadhi baada ya muda kisha akiwaua na kwenda kuuza viungo vyao kama vile: figo, maini na moyo.

Hata hapo wanapoongea na Miriam, kulikuwa kuna watu huko waliotekwa na wengine wakiwa watoto.

Hili likamgusa Jona katika namna ya kipekee.

"Sasa unahitaji kwenda rehab, Miriam," Jona akashauri.

"Nataka, lakini nahofia sana usalama wangu. Hata hapa ninapokaa, Nyokaa anapafahamu, anaweza akatuma watu waje kunimaliza."

Jona akajaribu kumtoa hofu kwa kumwambia atamuweka chini ya ulinzi kwa wakati wote huo atakaokaa hapo lakini bado kwa Miriam hilo halikutosha kabisa.

Hakuna mtu aliyekua anamwamini anaweza kumlinda isipokuwa Jona mwenyewe.

"Usijali, nitakuwa nakuja kukutembelea na tutakuwa tunawasilana mara kwa mara, sawa?"

"Sawa."

Kwa namna Miriam alivyoitikia ilikuwa ni kama anataka kumridhisha Jona. Hata Jona naye alilitambua hilo. Hakupuuzia yale maelezo aliyoyasema Miriam juu ya usalama wake lakini aliona kwa hatua hiyo itakuwa njema huku akitafuta namna bora zaidi.

Akamuaga Miriam anaenda zake. Alikuwa amechoka mno kwa siku hiyo, aliona ni kheri aende nyumbani kupumzika.

Lakini kabla ya kunyookea huko akaenda kituo cha polisi cha karibu na kutoa taarifa juu ya Miriam akitaka mwanamke huyo pamoja pia na makazi yake yatazamwe kwa jicho la kipekee kwani wapo hatarini.

Alipokamilisha zoezi lake hilo akajiweka kwenye daladala kurudi nyumbani.

Akiwa njiani akatathmini kazi yote aliyofanya kwa siku hiyo. Haikuwa mbaya, akajivunia. Kila kesi iliyokuwa mikononi mwake ilikuwa imefikia pazuri na ufumbuzi wake unaonekana.

Akafika nyumbani na kumkuta Marwa akiwa ameketi sebuleni.

"Pole kwa upweke."

"Nilikuwa na mke wangu, sikuwa mpweke."

"Mke wako?"

"Ndio."

Marwa akaonyeshe tarakilishi yake mezani. Jona akacheka.

"Msalimie mkeo, mwambie shemeji anamsalimu."

"Na wewe pia, msalimu wa kwako aliyeko ndani ya jokofu," Marwa akatania. Jona akacheka tena, akamwambia mwanaume huyo ni namna gani hawezi kulala mpaka atie kinywaji mdomoni.

Kichwa chake kimekuwa kikifikiria sana familia yake, haswa wakati wa usiku.

"Huoni sasa ni muda wa wewe kutafuta mtu mwingine?" Marwa akauliza. Jona akamtazama mwanaume huyo na kumkubushia yale maelezo aliyompatia yeye kipindi kile.

Akimpata huyo mwingine, atamuweka hatarini. Alafu kwa sasa yu bize hatokuwa radhi kusumbuliwa na 'calls' na jumbe za mara kwa mara.

"Unajua wanawake muda mwingine wana matatizo. Unaweza ukawa unafuatilia kesi nyeti sana, pengine raisi ameuawa, lakini yeye akakutumia ujumbe ukiwa kazini 'ina maana raisi ni muhimu kuliko mimi?'"

Wakacheka. Jona akaendea jokofu na kutoa kinywaji, akatafuta na glasi akaviwek mezani. Akawambia Marwa kuwa amechoka sana lakini hataweza kulala pasipo kinywaji.

"Nikuwekee kidogo?"

"Hapana!"

"Najua imekupelekesha sana asubuhi ya leo. Wewe si mlevi."

"Umejuaje?"

"Hakuna swali ninaloulizwa sana kama hilo. 'Umejuaje?'," Jona akatabasamu na kuongezea: "Anyways, hauna sura ya pombe. Niambie kama nadanganya."

Wakaendelea kuteta kidogo, na jambo la maana walilozungumza kabla Jona hajapitiwa na usingizi wa kilevi, ni kesho yake waende kuwatembelea wazazi wake Marwa.

Jona alikuwa anataka kuona antidote wanayoitumia. Pengine anaweza kuifutia ufumbuzi.

Marwa akajikuta anapata moyoni. Alitokea kumuamini sana Jona. Aliamini mwanaume huyo atalipatia swala lake ufumbuzi japo hakujua ni kwa namna gani.

Hii inaitwa imani.

Alimtazama Jona akiwa amelala kwenye kiti, akamnyanyua na kumbeba kisha akaenda kumlaza kitandani. Akamfunika na shuka jepesi.

**

Saa mbili asubuhi.

"Jona, hili ni kushangaza kabisa!" Alipayuka Kamanda. "Leo punde nilipofika tu ofisini, nimepokea ujumbe toka kwa mtu nisiyemjua akijiita 'msamaria mwema'. Taarifa zake zimeniogopesha sana, na zaidi zimenifanya nikatafakari kwa kina ni nani mtu huyo na kama ujumbe alionitumia unaweza kuwa kweli."

Kamanda akabofya tarakilishi yake wakati Jona 'aliyekula' suti akimtazama kwa umakini. Kidogo Kamanda akamkabidhi Jona tarakilishi yake apate kusoma ujumbe huo.

Jona akaupitia kwa wepesi kisha akamtazama Kamanda.

"Umeupata ujumbe huu mwenyewe?" Akauliza.

"Sijajua. Ila huyu mtu amejuaje akaunti yangu ya barua pepe?"

Kabla Jona hajajibu, simu ya mezani ya Kamanda ikaita. Akainyofoa kwenye kitako chake na kuiweka sikioni. Alikuwa ni Kamanda mkuu. Naye amepata ujumbe kama alioupata Kamanda kwenye akaunti yake.

Wakateta kwa dakika kadhaa. Kisha,

"Sawa mkuu," Kamanda akamalizia simu yake na kuirejesha kwenye kitako chake alafu akalaza mwili kitini.

"Jona," Kamanda akaita. "Sheng Li ana kesi nzito ya kujibu. Hizi tuhuma si nyepesi hata kidogo. Muite kituoni na hii kesi utaibeba wewe."

Kisha akamtazama Jona kwa macho ya pole, yenye kiini cha msisitizo.

"Anza upelelezi mara moja!"

***

- NI TAARIFA GANI HIZO NZITO ALIZOPEWA KAMANDA NA MKUU WAKE? NA JE ZIMETOKA KWA JONA AMA MWINGINEWE?
- SASA NI RASMI SHENG ANAKUWA CHINI YA UPELELEZI MAALUM, ATAFANYA NINI? MPANGO WAKE WA MILIONI MIA NI WANINI?
 
*ANGA LA WASHENZI (MSIMU WA PILI) -- 02*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

"Jona," Kamanda akaita. "Sheng Li ana kesi nzito ya kujibu. Hizi tuhuma si nyepesi hata kidogo. Muite kituoni na hii kesi utaibeba wewe."

Kisha akamtazama Jona kwa macho ya pole yenye kiini cha msisitizo.

"Anza upelelezi mara moja!"

ENDELEA

Sasa tunda lilikuwa limekwiva. Kifuani Jona akatabasamu akiona sasa muda wa kumuingia Sheng kwa miguu yote umeshawasili.

Alikuwa analingoja hili kwa muda.

Akanyanyuka akibeba jukumu hilo na kurudi ofisini kwake alipotulia na kumpigia simu Marwa. Akamwambia njia yake imezaa matunda. Wamepata kile walichokuwa wanakitaka!

"Sasa mji wa Roma unaanza kuanguka. Kwa ushahidi tulio nao Sheng haweza kututoka abadani!" Jona akatilia muhuri.

Baada ya lisaa limoja akatoka ofisini, akiongozana na wenzake wawili, wakaelekea kwenye ofisi ya Sheng. Huko wakamkuta mwanaume huyo akiwa ana kikao kifupi na wafanyakazi wake wawili wenye asili ya China.

Akapewa taarifa ana ugeni toka polisi. Alipotazama kwenye kamera, akajikuta anatabasamu baada ya kumwona Jona!

Tabasamu lake hili halikuwa la furaha, bali kifo. Hasira na chuki. Alitetemeka kwa hasira na hata kikao chake hakuweza tena kuendelea nacho, akakivunja mara moja akihaidi watakifanya tena pale atakapotoa taarifa.

Jona akaingia ofisini.

"Bwana Sheng, naitwa inspekta Jonathan toka makao makuu, polisi," Jona akaonyeshea kitambulisho chake kisha akaelezea dhumuni la ujio wake kumtaarifu Sheng kuwa yupo chini ya upelelezi maalum kwa kuhusishwa na tuhuma kadhaa za mauaji, biashara za magendo, vilevile umiliki haramu wa jeshi.

Jona akamtajia orodha ya viongozi anaotuhumiwa kuwaua hapa nchini na nchi jirani, Kenya. Akamtajia 'kambi zake za jeshi' iliyopo hapo makaoni na Nairobi na biashara zake anazofanya.

Sheng akabadilika rangi kuwa mwekundu. Lakini akamudu kutabasamu na kumtazama Jona kwa utararibu. Akamuuliza:

"Mbona sielewi unachokiongelea inspekta?"

"Unaelewa kila kitu," Jona akasema kwa hakika. "Kila nilichokieleza hapo kina uthibitisho na ushahidi. N jambo la muda sasa uovu kukaa wazi. Hakuns linalodumu milele, Sheng!"

Sheng akashindwa kuzuia hasira zake, akakunja sura sasa. Moyo wake uligeuka kuwa barafu. Mikono yake ilitetemeka akiwaza kama ana haja ya kutoa bunduki yake kwenye droo awamalize polisi hawa mara moja alafu awazike kwenye himaya yake.

Lakini hapana! Kwa kufanya hivyo ataharibu zaidi. Mpaka polisi hao wamefika hapo ni wazi huko makaoni kuna taarifa zao. Endapo akiwaua, atawakaribisha nzi zaidi kwenye kidonda ambacho anaweza kukificha.

Leo Sheng akawa amejifunza somo moja muhimu sana. Si kila mahali wapaswa kutumia bunduki. Pale mbu anapotoa juu ya korodani, ndipo unapoelewa kwamba si kila jambo husuluhishwa kwa nguvu.

Akairudishia vizuri droo yake yenye bunduki alafu akatabasamu.

"Ni tuhuma," akasema kwa lafudhi yake ya ki-Mandarin. "Sishangazwi na tuhuma hizo, najua mimi ni mfanyabiashara mkubwa siwezi kukosa maadui wa kuniharibia."

Akaonya.

"Endapo tuhuma hizi zitakapobainika ni za uongo basi wanasheria wangu watahakikisha serikali inanilipa fedha nyingi sana kama fidia ya kunisumbua ... na utambue kabisa, Jona. Hili litahatarisha uhusiano uliojengwa kwa muda mrefu kati ya nchi hizi mbili. Na sina haja ya kukuelezea ni kwa namna gani mnavyonufaika na uhusiano huu, kila mwananchi anajua."

"Lakini si kila mwanachi anajua mnayoyatenda," Jona akamkatiza. "Hawajui pia mnavyonufaika katika haya."

Akanyanyuka na kumtaka Sheng afike kituo kikuu cha polisi kesho yake asubuhi na mapema. Kushindwa kufanya hivyo kutamuweka matatani vilevile kutaweka bayana asubuhi na mapema kuwa tuhuma zake ni za kweli.

Aliposema hayo Jona akaaga na kwenda zake. Sheng akabaki akisaga meno. Alishindwa hata kuongea. Moyo wake ulikuwa unamuenda kasi. Jona alimfanya ajione ni mtoto mdogo asiye na kitu, mdhaifu na hana akili!

Hakuwahi kudhalilishwa kiasi hiki. Akalalama kifuani. Haikuwahi kutoka hata siku moja.

Alinyanyuka akaendea jokofu akafungua na kutoa maji makubwa, akanywa yote kana kwamba alikuwa na kiu cha karne!

Alitaka kupooza hasira zake. Alihisi kifua kinawaka moto. Baada ya hapo, angalau akijihisi ana unafuu, akarejea kitini, akawaza namna ya kufanya.

Ilimbidi awe mwangalifu sasa. Hata kama anataka kumwangamiza Jona basi afanye hilo kwa pole, kwa ustadi, mikono yake isinuke damu kualika nzi.

**

"Mlitumwa na nani kwenda kumvamia Marwa?" Aliuliza Jona akiwatazama wanaume wawili mbele yake. Wanaume hawa mmojawao alikuwa ni dereva, na mwingine akihusika moja kwa moja kwenye tendo la utekaji wa Marwa. Walikuwa wamevalia suruali zao za vitambaa huku vifua vikiwa wazi, mikono na miguu imefungiwa vitini.

"Hatukutumwa na yeyote yule!" Dereva akaropoka. "Tumeshasema tulikuwa tunamdai kwa muda mrefu, tulikuwa tunataka pesa yetu!"

"Pesa gani?" Jona akauliza.

"Ya biashara. Alitudhulumu!" Dereva akaendelea kuropoka. Jona akatabasamu kisha akawasogelea karibu.

"Nimeshaambiwa ninyi ni wabishi. Hampo tayari kusema lolote. Mmefunzwa kukaa kimya, mmefunzwa kupambana na mateso, lakini mimi pia mimefunzwa kutesa. Ebu tuone nani mshindi."

Jona akatumia robo saa tu, akapata kila anachokihitaji. Wanaume wale hawakuweza kustahimili mateso aliyowapa wakaweka bayana kila jambo kwamba walitumwa na Sheng kumchukua Marwa wampeleke akajibu mashtaka yake.

Jona akataka maelezo zaidi kutoka kwao, ni wapi Sheng anapozikia wafanyakazi punde anapowaua? Hapa watumishi hao wakaleta tena ka ubishi, Jona akarejea zoezi lake la kuwabana pumzi akiwapiga nyundo za mbavu!

Hawakustahimili, wakalegea. Wakaeleza. Maelezo yote hayo Jona akayaandika na kumfikishia Kamanda.

"Hakikisha kesho atakapofika hapa, unamtia ndani kisha unaenda fanya msako kwenye himaya yake nzima. Utakapokuta miili hiyo ardhini utakuwa ushahidi mzuri sana. Itasaidia ku 'finalise'," Kamanda akapendekeza.

"Sawa, mkuu, nitalifanyia kazi!" Jona akalibeba hilo kisha akatoka zake nje ya ofisi.

**

Majira ya jioni ya saa kumi na mbili.

"Wèishéme bùshì tā?" (Kwanini sio yeye?) Sauti iliuliza nyuma ya mlango.

"Wǒ gēnběn bù xǐhuān tā," (Simpendi kabisa,) sauti nyingine ikajibu. "Wǒ suǒyào de zhǐshì sǐwáng!" (Ninachokitaka afe tu!)

Kukawa kimya kidogo.

"Nàme nǐ yǒu shé me jìhuà?" (Kwahiyo nini umepanga?)

"Wǒ xiǎng qiēduàn tā yīlài de shǒu," (nataka kukata mkono anaoutegemea,) kisha akaongezea, "Nǐ huì bāng wǒ ma?" (Utanisaidia?)

"Wǒ huì bāngzhù," (Nitasaidia,) mwingine akajibu.

"Názhe tā. Nǐ huì zài jiǔdiàn de àn biān kàn dào tā." (Chukua hii. Utamwona kwenye fukwe ya hotel.)

Baada ya muda wa dakika tano, ndani ya ofisi ya Sheng akatoka mchina aliyebebelea mkoba mkubwa mweusi. Akapanda Range rover modeli ya zamani, rangi ya grey, akaelekea Sea View hotel.

Baada ya mwendo wa dakika kadhaa akawasili, akaingia hotelini na asichukue muda mrefu akatoka akiwa na mikono mitupu. Akazama ndani ya gari na kupiga simu.

"Tā yǐjīng shōu dàole. Dàn zhè hái bùgòu!" (Amepokea. Lakini amesema haitoshi.)

"Tā xiǎng yào duōshǎo?" (Anahitaji kiasi gani?) Sauti ikauliza simuni.

"Bǎ jiàgé fān bèi nàme gàosù nǐ zěnme xiǎng!" (Ongezea mara mbili alafu sema unatakaje!) Mtumishi akajibu.

"Méiguānxì!" (Sawa!) Sauti ikamjibu simuni.


***
 
*ANGA LA WASHENZI (MSIMU WA PILI) -- 03*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

"Tā xiǎng yào duōshǎo?" (Anahitaji kiasi gani?) Sauti ikauliza simuni.

"Bǎ jiàgé fān bèi nàme gàosù nǐ zěnme xiǎng!" (Ongezea mara mbili alafu sema unatakaje!) Mtumishi akajibu.

"Méiguānxì!" (Sawa!) Sauti ikamjibu simuni.

ENDELEA
Baada ya kuteta huko na kukubaliana, mtumishi akawasha chombo chake na kutimka. Sheng akatabasamu akiwa ofisini. Sasa mambo yalienda kama alivyotarajia.

Akajilaza kwenye kiti na kunyanyua simu kumpigia mhasibu, akamwambia amletee tena milioni mia moja. Alipoirudisha simu mezani, akatabasamu tena. Hakika hakutegemea kama siku hiyo ingeisha vizuri.

**

Bado mpaka saa moja usiku ...

"Tuondoke, muda umewadia," akasema Jona akimtazama Marwa. Walikuwa wameketi ndani ya sebule ndogo ya kawaida lakini ikiwa imepambwa kwa usafi wa hali wa juu.

"Hatumngojei baba?" Marwa akauliza.

"Muda umeenda, Tutakuja siku nyingine," Jona akashauri na mara kidogo akatokea mama mtu mzima, makadirio miaka sitini kasoro kidogo. Alikuwa mwembamba mwenye nywele za mvi, lakini akiwa mwenye nguvu na uchangamfu.

Akaketi kitini.

"Naona baba amechelewa sana leo," akasema. "Sijui atakuwa amepitia wapi!"

"Usijali, mama," Marwa akamtoa hofu. "Tutakuja siku nyingine kumwona. Kwa sasa tunaomba tukukimbie."

"Mbona mnawahi hivyo na mmekuja muda si mrefu?" Mama akashangaa. "Kaeni mumngoje kidogo. Nadhani ndani ya muda mchache, atawasili."

"Kuna mahali tunatakiwa kupitia mama," Jona akaeleza. "Tungekaa mpaka usiku mzito."

Mama hakuwa na budi, akawatakia safari njema lakini kabla hawajaondoka akahitaji aongee kidogo na Marwa. Jona akatangulia kwenda nje.

"Vipi? Mbona unaondoka haujatupatia dawa?" Mama aliuliza, na kuongezea. "Unajua imebakia kiasi kidogo sana!"

Akafungua fundo lake la kanga na kutoa kachupa kadogo kumwonyeshea.

"Unaona?"

Ndani ya kachupa hako kulikuwa na kama katone hivi ka maji ambacho kukaona ilihitaji umakini wa hali ya juu.

"Nimeona, mama," Marwa akasema kwa upole. "Nitakuletea tu."

"Kaburini?" Mama akastaajabu. "Unadhani haka katatuweka hai mpaka lini, Marwa?"

Marwa hakuwa na la kusema, akatazama chini.

"Kuna shida gani, Marwa? Naomba uniambie. Dawa imeisha?"

"Hapana."

"Sasa nini shida? Niambie mwanangu."

Marwa akajikuta macho yake yanakuwa mekundu. Sauti ya mama yake ilikuwa inatafuna moyo wake. Alitamani kumwambia hayupo tena kule apatapo dawa lakini alihofia. Angeweza kumuua mamaye kwa presha.

Akamtia tu moyo ampe kitambo kidogo, atakuwa ameshaleta dawa hapo nyumbani.

"Kama kuna shida tuambie," Mama akamwambia akimshika bega. "Sisi ni wazazi wako, hauna mtu mwingine wa kumwaminini."

"Hakuna shida mama," Marwa akakazana. Alikaza uso wake usionyeshe majonzi. Akamkumbatia mama yake na kumuaga. Lakini alipogeuka tu chozi likamshuka haraka. Moyo wake ulikuwa unamuuma. Alikuwa anashuhudia wazazi wake wakifa mbele ya macho yake.

Alienda kukutana na Jona wakaenda zao. Hakusema jambo mpaka wanafika nyumbani.

"Marwa, it's going to be ok!" Jona akamfariji. "Tutapata antidote tu."

Marwa akajikuta anadondosha chozi. Akamtazama Jona na kumwambia shida si kuipata, bali muda. Antidote aliyoiona inawatosha kwa usiku huo wa leo tu. Kesho yake hawatakuwa na cha kutia mdomoni, wataanza kuteseka mno.

"Kwa umri wao ilibidi wawe wamepumzika, si kupitia shida hizi," alisema Marwa kwa uchungu.

Jona akamtazama kwa huruma. Baada ya mafikirio kidogo, akamuuliza:

"Unajua antidote hiyo ilipo?"

"Kivipi?"

"Unafahamu mahali wanapoihifadhi antidote hiyo kule kwa Sheng?"

"Hapana," Marwa akajibu akitikisa kichwa. "Lakini nafahamu ilipo maabara."

"Si mbaya," Jona akateta. "Basi jiandae saa tano tunaenda huko!"

"Wapi?" Marwa akatahamaki kwa woga.

"Ilipo antidote!" Jona akafafanua. Na asingoje maelezo zaidi, akaenda zake chumbani. Marwa akabaki anamtazama kwa mshangao.

**

Baada ya kunyata kidogo,

"Upande huu!" Marwa akaelekeza kwa sauti ya chini. Alikuwa amevalia nguo nyeusi na kinyago usoni. Na Jona pia.

Walikuwa tayari wameshazama kwenye ngome ya Sheng katika majira haya ya saa sita usiku. Lengo lao likiwa moja, kwenda kuinyaka antidote ndani ya maabara.

Wakatembea tena kwa utaratibu wakichukua kila tahadhari, walipokaribia maabara, wakamwona mwanaume mmoja aliyebebelea bunduki kubwa ndefu mkononi. Jona akaitambua ni SMG.

Mwanaume huyo alikuwa ni mlinzi. Alikuwa ameketi kwenye kibaraza cha jengo la maabara akichokonoa meno yake kwa kijiti.

Jona akampanga Marwa.

"Utatoka na kunyata kuelekea upande huu," akamwonyeshea upande wa kushoto. "Lazima atakutazama na aidha anaweza kukuita. Lakini kabla hajafanya kitu, atakuwa tayari yupo mikononi mwangu."

Marwa hakupewa muda wa kufikiri, Jona akaanza kutekeleza mpango. Haraka akanyanyuka na kutembea upesi kuelekea upande wa kulia, lakini akifanya hayo miguu yake haikutoa sauti hata kidogo.

Basi muda mchache, mlinzi akamwona Marwa akikatiza, haraka akanyanyuka na kuishikilia vema silaha yake. Akapaza sauti:

"Wewe nani?"

Marwa akasimama na kumtazama.

"Mimi? Mimi naitwa Marwa!"

"Marwa?" Mlinzi akatahamaki. Hakuwa analijua jina hilo katika orodha ya walinzi. Akamtaka Marwa anyooshe mikono juu na kupiga magoti.

"Sina tatizo na wewe," Marwa akasema akishuka chini. "Mwenye tatizo ni huyo aliyepo nyuma yako."

Haraka mlinzi akageuza shingo kutazama. Mara shingo hiyo ikadakwa na kuendelezewa safari. Akadondoka chini kama mbuyu.

Wakamficha, kisha chap wakaufuata mlango mzito wa maabara. Ulikuwa ni mlango wa chuma wenye kitasa kipana. Wakajaribu kuufungua pasipo mafanikio.

"Jona, inabidi tukachukue funguo!"

"Wapi?"

"Stoo. Kule wanapozihifadhi."

"Hatuna muda huo Marwa. Mlinzi mwingine anaweza kutokea akagundua uwepo wetu. Na endapo akirusha risasi moja tu, atakuwa keshatibua mambo."

"Sasa tunafanyaje?"

Jona akavua mkanda wake na kuchomoa kichuma cha kushikilia vitundu mkandani. Akakipinda kichuma hicho kwa mdomo, akitumia sekunde kadhaa kama ishirini, alafu akakidumbukiza hicho kichuma ndani ya kitasa.

Akapeleka mkono kushoto na kulia, mara mlango ukalia - kat! Wakajaribu kuufungua. Hola! Mlango haukufunguka.

"Shit!" Jona akalaani.

Akakirepea tena kile kichuma kwa kukibadili muundo wake, alafu akajaribu tena. Mlango ukalia tena - kat! usifunguke.

"Jona, tunapoteza muda. Twende kule," Marwa akashauri.

"Hapana, Marwa," Jona akatikisa kichwa. "Mlango huu umelokiwa mara tatu, utafunguka tu ... ngoja uone ..."

Jona akachokonoa tena kitasa, mlango ukalia tena - kat! Na mara hii walipougusa ukatii amri! Wakazama ndani.

Maabara ilikuwa kubwa. Wakitumia kurunzi kuangaza, wakaanza kupekua upesi upesi. Wakachukua dakika nyingi humo. Baadae ndipo wakaona chumba kidogo ndani ya maabara kikiwa kimeandikwa antidote mlangoni.

Jona akafanya ufundi kufungua kitasa kisha wakazama humo ndani, baada ya muda kidogo wakatoka Jona akiwa amebebelea flask - chupa ya kioo yenye mdomo mwembamba chini ikiwa imejitanua mithili ya pembe tatu. Ndani ya chupa hiyo kulikuwa na kimiminika mithili ya maji.

Kwa haraka wakajongea kuufuata mlango wa maabara, lakini kabla hawajaufikia, Marwa akajikwaa. Mguu wake ulidumbukia ndani ya vifereji vidogo vya kutolea uchafu, akajikuta yu chini kwa kukosa namna ya kujiokoa!

Kabla hawajafanya jambo, ndani ya muda mfupi, wakasikia chupa kadhaa nazo zikidondoka na kusababisha kelele!

Mara huko nje, sauti nzito ikauliza:

"Nani huyo?"

Alikuwa ni mjibaba wa miraba minne, mkononi akiwa ameshikilia bunduki ndogo.

Mwili wake mpana kama gogo ulikuwa umesitiriwa na nguo nyeusi. Chini ana buti kubwa rangi ya kaki. Kichwa chake kinameremeta kwa kukosa nywele. Na mdomo wake ukiwa umefunikwa na mustachi mzito wenye afya tele.

Jibaba hilo likalalama.

"Yani hawa panya sasa naona wananipanda kichwani!"

Likapiga hatua nzito kuufuata mlango lakini kabla hajaugusa, akauliza:

"Isak yupo wapi?" Akitazama huku na kule kisha akalalama;

"Hawa panya watamaliza vitu vyote humu ndani. Experiment gani hizo za kila siku kutumia panya!"

Akasonya.

"Hakuna mnyama namchukia ka --"

Akashtuka kuona mlango una upenyo. Asiamini macho yake akausukuma kwa kidole, mara ukafunguka na kuachama. Akapata wasiwasi. Akashikilia vema bunduki yake na kuzamisha mkono ndani, akabofya switch, taa zikawaka!

Akaangaza akinyooshea bunduki yake huko. Kwa mbali akona chupa kadhaa zikiwa zimepasuka. Akapiga hatua kusonga.

Pembeni ya chupa hizo zilizopasuka, kwa chini ya meza za sementi zilizokuwa zimejengwa humo, alikuwa amelala Marwa.

Alikuwa ameubana mdomo wake kwa nguvu akijitahidi kutulia lakini alikuwa anasikia maumivu makali sana. Chupa zile zilizoanguka zilimrushia kemikali usoni na alikuwa anahisi kuungua!

**
 
Back
Top Bottom