Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

*ANGA LA WASHENZI – 15*
*Simulizi za series*

ILIPOISHIA..

Akagundua gari hilo lilikuwa limefika hapo muda si mrefu. Nani ameingia bar muda si mrefu? Hakuna mwingine mbali na mwanaume yule aliyevalia suti, akili yake ikampa majibu haraka.

Basi akajikuta akitabasamu.

“Naona amenifuata kumaliza kazi yake,” alisema kisha akajirudisha kwenye kiti chake. Akaketi na kumtazama Bigo.

ENDELEA..

Alikunywa maji yake taratibu akiyapanga mambo kichwani. Alipomaliza akamuita mhudumu na kumlipa pesa yake kisha akanyanyuka na kubeba vitu vyake. Taratibu akashika njia ya kwenda nyumbani.

Alitumia njia tofauti na ile kuu. Kadiri alivyokuwa anasonga mbele, basi akawa anaongeza ukubwa wa hatua zake.

Haikupita muda mrefu, akahisi kuna gari linakuja nyuma yake. Pasipo kutazama akajua ni lile Mark 2. Kwa mwendo wake wa ukakamavu akaendelea kukata mbuga. Ndani ya muda mfupi, mbele ya nyumba yake.

Akafungua geti na kuzama ndani.

Hili lilikuwa kosa la kwanza Bigo kulifanya – kumruhusu Jona azame ndani ya nyumba. Hakujua kama amefanya kosa. Alimchukulia Jona kama mchora picha tu. Kwa akili yake akaona Jona amejiingiza kwenye kaburi lake.

Somo la namna mwanaume mwanaume huyo alivyokwepa ajali halikumuingia akilini, au pengine hakulielewa.

Alishuka akaliacha gari ‘on’ kwa minajili kwamba atarejea muda si mrefu na kuhepa zake baada ya tukio. Mkononi alikuwa amebebelea bunduki ndogo, na tayari uso wake ulikuwa umevikwa kinyago cheusi.

Kinyago chenye sura ya fuvu la kichwa cha binadamu.

Akazama ndani kwa kuruka ukuta kama kima. Taratibu akausogelea mlango, akajaribu kuusukuma, ulikuwa umefungwa. Basi hakutaka kuzozana nao kwasababu alitaka mambo yawe kimya kimya.

Alitaka amalize kula pasipo kujaza nzi.

Akazunguka jengo kupitia madirishani, kwa malengo auendee mlango wa uani nao aujaribu, pia amuone Jona yupo pande gani ya nyumba.

Alijuta kwanini hakubebelea kiwamba cha kumezea sauti ya bunduki. Lakini akatafuta ahueni ya juto hilo kwa kujitia hana haja ya kutumia hiyo silaha.

“Nitatumia mikono yangu tu,” akajisemea kifuani. “Huyu si wa kupoteza risasi yangu.”

Akazunguka dirisha la kwanza, hakuona kitu. Dirisha la pili na la tatu pia. Akiwa anasogelea la nne, ambalo ndilo lilikuwa la chumbani kwa Jona, akasikia sauti ya kitu kama karatasi nyuma yake.

Haraka akageuza shingo kutazama. Hakumuona mtu! Akaendelea zake kufuata dirisha, akarusha macho ndani. Hakuona mtu.

Sasa alikuwa karibu na mlango wa uani. Kama hatua tano hivi aukute.

Alipiga hatua tatu, akahisi tena sauti ile ya mwanzoni. Haraka akageuka, saa hii akinyooshea mdomo wa bunduki huko. Hakuona mtu! Aliporejesha uso wake mbele, akakutana na mwanaume amesimama.

Alikuwa Jona.

Kabla hata kichwa cha Bigo hakijajua nini la kufanya, akashangaa kuona Jona yupo juu, kufumba na kufumbua, akala teke lenye kilo nzito lililomtupa chini kama fuko la saruji!

Akanyanyuka upesi kwa kujifyatua na mikono yake. Ila Jona hakumpatia mwanya hata kidogo, akachumpa na kujilaza hewani akijizungusha kama tairi. Akachanua miguu kumzawadia tena teke.

Mara hii Bigo akaliona, akainama kukwepa, kunyanyuka, hajakaa sawa, mkono wenye bunduki ukapigwa, bunduki ikarukia mbali.

Jona akatabasamu. Akatanua miguu yake na kumuita Bigo kwa ishara. Sasa Bigo akajua anapambana na mtu, mwanaume, sio ‘mchora picha’.

Alikuwa ameingia peku kwenye kiwanja chenye mbigiri. Na sasa hakuwa na budi zaidi ya kuonyesha uanaume wake.

Alikunja ngumi akajongea kwa kasi. Akatumikisha kiuno chake kurusha mateke mazito, mateke yakapita kando ya kichwa cha Jona. Akapeleka ngumize, akarudisha viwiko, navyo vikanyimwa mwelekeo.

Baada ya dakika moja, rasmi Jona akaanza kujibu mashambulizi akiwa tayari ameshamsoma adui yake ndani ya muda huo mfupi.

Hakupoteza nguvu, akapiga maeneo dhoofu kwenye mwili wa binaadamu, ambazo kitaalamu kwenye mchezo wa mapigano, martial arts, huitwa pressure points.

Ncha za ngumi yake zilitafuta kingo za kwapa za Bigo, akatia ganzi mikono ya adui. Akampiga pia chini kidogo, katikati ya shingo, penye kashimo kanachotenganisha shingo na kifua, na kummalizia juu ya kitovu kwa hatua moja moja na robo ya vidole.

Bigo akawa hoi.

Jona akamvua kinyago na kumpeleka ndani sebuleni, akamfunga kamba kwenye kiti kisha akachukua kiti kingine na kukisogeza karibu. Akachukua na chupa kubwa ya mvinyo na glasi yake, akamiminia kinywaji humo na kupiga fundo moja akiketi.

“Habari yako? – hatukuwa tumesalimiana,” alisema Jona akimtazama Bigo.

Bigo hakusema kitu. Jicho lake la kushoto lilikuwa jekundu mno. Na kushoto kidogo mwa jicho hilo kulikuwa kuna mfereji mdogo wa damu ukitokea kwenye jeraha la kiasi.

“Haya,” Jona akapandisha mabega yake juu. “Sitajali kama hutaki salamu yangu. Vipi na kinywaji nacho? Hutaki?”

Bigo akaguna kama mtu anayetaka kuangua kicheko. Akasema:

“Siku zako zinahesabika, msanii. Utaenda kuonja udongo muda si mrefu.”

Jona akatabasamu. Akanywa kwanza mafundo matatu ya kinywaji chake.

“Inaonekana unaona kinyume, ndugu yangu. Kwa unavyoona, kati yangu na wewe nani anaenda kuonja udongo muda si mrefu?”

Bigo akaguna kwa kiburi.

“Anyway, sina muda mwingi hapa,” Jona akasema akitazama saa yake ya mkononi.
“Muda si mrefu itanibidi nipumzike kwa ajili ya kesho, nina kazi za kufanya na watu wa kuwaona. Hivyo basi ningependa kwenda moja kwa moja.

Wewe ni nani? Na umetumwa na nani?”

Kimya.

“Najua itakuwa ngumu kwako kusema, ila nisingependa tukaumizana na kutiana ukilema alafu ndiyo useme, so tuokoe muda.”

“Okoa muda wako kwa kuniua, msanii,” Bigo akasema, kisha akatabasamu.

Jona akanywa mafundo mawili kwa staili ya tarumbeta kisha akanyanyuka na kumsachi Bigo, akamchomoa funguo za gari.

“Unaenda wapi?” Bigo akawahi kuuliza.

Jona akamtazama na kumpuuza kisha akaenda zake nje mpaka kwenye gari la Bigo. Akafungua mlango na kuanza kupekua chombo hicho akitazama huku na huko huku akisaidiwa na kurunzi.

Akapata simu mbili, risasi nne, leseni na picha nne aina ya pasipoti. Akarejea ndani.

Akaviweka vitu alivyovipata juu ya meza alafu taratibu akaanza kukipitia kimoja baada ya kimoja.

“So unaitwa Alfonce Bigo,” alisema Jona akitazama leseni. Bigo alikuwa kimya akimtazama kwa macho makali, mdomo ameupinda.

Alimaliza kutazama leseni akaiweka juu ya meza, akatazama pasipoti zile nne: zilikuwa za watu tofauti tofauti.

“Na hawa nao umepanga kuwaua ama?”

“Achana na vitu vyangu, havikuhusu!” Bigo akafoka. Jona asimjali, akaendelea na kazi yake.

Aligeuza pasipoti akazitazama kwa nyuma, akaona zimeandikwa kwa mbali maneno ya kichina. Kila pasipoti ilikuwa na maneno hayo.

Aliziweka kando akateka simu na kuanza kuzikagua. Moja ilikuwa ni smart phone, Nokia Lumia kubwa nyeusi, nyingine ikiwa ndogo ya kawaida, tekno, nayo nyeusi kwa rangi.

Simu zote zilikuwa zimefungwa kwa namba. Mtu kuingia na kutazama ilikuwa ni mpaka atie namba sahihi.

Bigo alijua Jona hataweza kufungua simu hizo, kwahiyo hapa akawa na amani na taarifa zake zilizomo ndani, zipo salama.

Alitegemea muda si mrefu Jona atamuuliza kuhusu hizo namba. Na aliapa kutozisema hata iweje, atazilinda kwa uhai wake.

Kinyume na matarajio, Jona hakumuuliza chochote, bali akanyanyuka na kwenda chumbani alipotoka na tarakilishi mpakato nyeusi aina ya HP, na waya wa kuhamisha data, USB.

Akaweka tarakilishi mezani na kuiwasha kisha akachomeka waya wa kuhamisha data toka kwenye simu kwenda kwenye tarakilishi.

Sasa hapo akawa huru kufikia mafaili yaliyopo kwenye simu ya Bigo pasipo kutia namba zozote. Mafaili yote akawa anayaona kwenye kioo cha tarakilishi yake.

“Wewe mshenzi acha kupekua simu yangu!’ Bigo aliwaka akitikisa mwili wake kwanguvu. Alitaka kujichopoa toka kwenye kamba. Alijitahidi sana kujing’amua lakini akaishia kupata tu maumivu.

Hakufanikiwa.

Jona, kana kwamba hasikii kelele za Bigo, akaendelea kuperuzi mafaili ya simu. Kuokoa muda akayakopi mafaili hayo na kuyahamishia kwenye tarakilishi yake kwa malengo ya kuyapitia atakapopata muda.

Alipomaliza akachomoa waya, akatoka mezani na kumjongea Bigo.


***


Nje ya nyumba ya Jona kulikua tulivu. Watu walikuwa ndani ya majengo yao na familia zao. Mataa yalikuwa yanamulika, na kelele pekee zilizokuwa zinasikika ni za watoto wakicheka ndani ya uzio.

Kama ungelipita hapo, basi usingeliwaza kama kuna tukio linaendelea ndani ya nyumba ya Jona, japokuwa ndiyo nyumba pekee iliyokuwa imepaki gari kwa nje.

Ndani ya muda mfupi, linatokea gari lingine. Kwa mbali halionekani kutokana na mwanga mkali wa taa. Linaposogea karibu na kufifisha taa, laonekana vema – ni Range Rover sport nyeupe.

Ndaniye alikuwamo bwana Kinoo peke yake. Akalipaki gari nyuma ya Mark 2, kisha akashuka.

Kama kawaida, alikuwa amevalia ‘kibody’ cheusi kilichobana kifua chake kipana pamoja na suruali ya jeans na moka nyeusi kwa chini.

Aliitazama Mark 2 kwa muda kidogo akijiuliza ni la nani. Akarusha macho yake ndani ya jengo la Jona, hakuona kitu.

“Ana mgeni au?”

Akalikagua gari lile Mark 2 kabla hajazama ndani kwa kuruka ukuta baada ya kuona mlango umefungwa. Naye mkononi alikuwa amebebelea bunduki ndogo, na mwendo wake ulikuwa wa tahadhari.

Angalau huyu alikuwa amepewa angalizo na Miranda juu ya Jona.

Alisogelea dirisha la sebule, akachungulia ndani. Hakumuona Jona, ila akamuona mwanaume aliyeketishwa kwenye kiti na kufungwa kamba. Hakumtambua mwanaume huyo kwani alikuwa amezibwa na kinyago usoni.

Lakini kinyago hicho kikamgutua. Kilikuwa ni cheusi chenye umbo la fuvu la binadamu. Alikumbuka Miranda aliwahi kumwambia kukihusu. Ya kwamba mwanaume yule aliyemvamia kuchukua kamera, alikuwa amekivaa.

Ina maana ndo’ huyu? Akajiuliza. Anafanya nini hapa akiwa amefungwa kamba?



*NINI KITATOKEA HAPA?*

*JONA KAENDA WAPI KAMWACHA MATEKA PEKE YAKE AKIWA KAMFUNIKA NA KINYAGO?*
 
*JOANA ANAONA KITU USIKU --- 13*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Mama akampa moyo na kumsihi apige moyo konde, atafanya mpango apate chuo hapa hapa nyumbani awe anamuona na kumpatia nasaha.

Zikapita siku mbili akiwa nyumbani. Siku ya tatu Joana akapata habari kwa kupitia runinga. Lisa alikuwa ameuawa na mtu asiyejulikana!

ENDELEA

Habari hizo zilimshtua na kumpa jakamoyo. Lisa kwake hakuwa rafiki tu bali mtu mwenye umuhimu mkubwa. Japokuwa alimjulia chuoni walitokea kutengeneza urafiki mpana wenye tija.

Alijikuta anaumia sana rohoni kila alipokumbuka sura ya Lisa na tabasamu lake. Namna alivyopambana kumfichia siri yake na kusimama upande wake siku zote hizo tangu anamjua.

Alishindwa kuzuia machozi kumbubujika. Ndoto yake ya kuonana na Lisa siku za usoni zilikata. Ina maana hatomuona tena.

Lakini zaidi ya yote, alijihisi atakuwa anahusika na kifo cha Lisa kwa namna moja ama nyingine, nafsi yake ilimwambia vivyo. Ilimshtumu, ilimshtaki.

Alijiona mkosefu na mkono wake ndiyo ambao umempeleka Lisa machinjioni.

Ila ngoja kwanza kabla ya kujihukumu, akaona basi ni vema akapata taarifa ya kutosha juu ya kifo hicho. Aliapa endapo akiwa anahusika kwa namna yoyote na mauaji hayo, hatasamehe nafsi yake kwa kuangamiza nafsi moja zuri aliyowahi kukutana nayo ulimwenguni.

Usiku kwake ulikuwa mgumu sana kwani hakulala kwa amani kabisa. Kila alipolala alimuona Lisa kando yake. Aidha akiongea, kucheka ama kutabasamu.

Alikurupuka kila mara, na kulia pia.

Asubuhi ilipowadia, akanyanyuka na kwenda kupata gazeti. Hakuwa na ‘smart phone’ hivyo hiyo ilikuwa ndiyo njia pekee kwake kupata taarifa kwa kina.

Akanunua gazeti moja la Kijerumani ambalo lilikuwa limeweka taarifa ya Lisa ukurasa wake wa kwanza kabisa, ila ikiwa pembeni kidogo ya habari kuu iliyobeba gazeti kwa ujumla.

Picha ndogo ya Lisa iliyo kwenye ‘black and white’ akiwa anatabasamu ilivuta machozi ya Joana kwa haraka sana. Akilipokea gazeti hilo alikuwa tayari anamwaga machozi na kubanwa kwikwi za kilio.

Akalifungua gazeti na kulisoma papo hapo.

Lisa aliuawa kwa kunyongwa majira ya usiku na mtu asiyefahamika ila akihisiwa ni muuaji fulani ambaye amekuwa akifanya mauaji maeneo hayo maeneo ya chuoni.

Kwa mujibu wa maelezo ya gazetini, Joana akajua ni Moa ndiye ambaye amehusika na kifo hicho. Ushahidi uliotolewa na wanafunzi wengine ulimwendea yeye kama mtu aliyewahi kuonekana hapo majira ya usiku mzito.

Lakini zaidi ya yote, Joana akatajwa kama mojawapo wa watu wanaotafutwa na polisi akituhumiwa kuhusika.

Kwanini aliondoka pasipo kuaga wakati alikuwa kwenye uchunguzi? Mbona kuondoka kwake na kufa kwa Lisa kwafuatana? Pia Moa, ambaye ndiyo mtuhumiwa wa kwanza wa mauaji, anahusishwa na yeye.

Joana akatetemeka akisoma gazeti hilo. Alihisi kichwa chake kimekuwa cha moto wakati kiwiliwili kikiwa kwenye baridi kali.

Haraka alirejea nyumbani kwao, akajifungia chumbani. Aliwaza na kuwazua. Alijiona akienda jela karibuni. Alikata shauri kumwambia mama yake juu ya taarifa hizo huenda anaweza kumsaidia kimawazo.

Baadae jioni mama yake aliporejea akamwambia. Mama yake akashtushwa sana na hizo taarifa, ila akampa moyo mwanae asipate shaka kwani atamsaidia kwa kumpatia wakili mzuri atakayemsaidia kumsafisha.

“Hatuwezi kukimbia hili, kadiri tutakavyolikimbia ndivyo tutakavyoonekana wahusika,” Mama alisema na kumalizia: “Itabidi twende huko tukakabiliane nalo.”

Mama akawasiliana na mwanasheria wake. Akampanga tayari kwa ajili ya kesi ya mwanae. Wakakubaliana wakutane siku ya kesho majira ya mchana.

Kesho wakakutana na Joana akaeleza kila kitu kwa mwanasheria huyo ambaye alijitambulisha kwa jina la Stewart McCoy. Alikuwa ni mwanaume mrefu aliyependezea ndani ya suti yake ya bluu.

Nywele zake zilikuwa nyekundu akizichana utamu. Alikuwa na macho ya kujiamini na sauti ya mamlaka.

Alitabasamu na kumshika bega Joana, akamwambia:

“Hiyo kesi yako ni ndogo sana. Wala usikose usingizi kwa kuiwaza.”

Baada ya hapo wakaongea maneno machache na mama yake Joana kabla hawajaagana.

“Kesho tutaenda Ujerumani,” mama alimwambia Joana. “Mwanasheria atafanya mawasiliano na polisi wa huko watarajie ujio wetu.”

Kweli kesho yake wakajipaki kwenye ndege kwenda Ujerumani. Waliripoti polisi ambapo huko Joana hakusema lolote lile kwa kigezo cha kumwachia kazi mwanasheria, Stewart McCoy.

Polisi wakaongea na mwanasheria. Baada ya siku moja tu siku ya kusikilizwa kesi ikapangwa.

Siku hiyo inspekta Westgate pamoja na walinzi wawili wa chuo, na msimamizi wa bweni – Cecillia walikuwa ndani ya mahakama wakiwa upande pinzani na Joana.

Joana alikuwa anatetemeka mno. Alihisi mwili wake umekuwa mzito na miguu yake haiwezi tena kumbeba, lakini Stewart akamtia moyo. Alimtazama kwa tabasamu pana akimwambia:

“Tunashinda hii kesi. Amini.”

Stewart alifanya mahakama kama chumba chake cha uani. Aliitawala na kuipelekesha atakavyo. Alikosoa ushahidi wote ulioletwa hapo kwa kusema ni wa kufikirika tu. Na ukitazama kesi hii ilikuwa na mlengwa wa kiroho zaidi, kiimani, mambo ambayo hayawezi kuthibitishwa na logiki ya kawaida. Mambo haya hayaaminiki mahakamani.

Nyundo ya hakimu ikagongwa, Joana akashinda.

Mahakama ikiwa inatawanyika, Inspekta Westgate akamfuata Joana na kumpatia mkono kumpongeza kwa kushinda kesi. Ila akamwambia:

“Najua unahusika, Joana. Ni swala la muda tu.” akaongezea: “Kama sitakushika mimi, atakushika mwingine.”

Akaenda zake akimwachia Joana parazo la mawazo alilokuja kutolewa na mama yake aliyemkumbatia kwa furaha.

“Umeshinda!” mama alisema kwa tabasamu akimtikisa mwanae. Walipanga kuondoka kurejea Ubelgiji kesho yake mapema.

“Utasoma huko huko, sawa?”

“Ndio, mama.”

Furaha hii ya Joana ilikuwa ni ya halaiki tu. Akiwa mwenyewe alikuwa anaumia na kuteswa na mawazo. Picha ya Moa na Lisa zilimjia na kumnyima raha.

“Nimemuua Lisa …” kuna sauti ilikuwa inajirudia masikioni mwake kila alipotulia. Hata akifumba masikio alikuwa bado anasikia. “Nimemuua Lisa …”

Alitazama mkufu aliopewa na Moa, machozi yakamdondoka.

“Moa yupo wapi?” alijiuliza. “Yule Moa yupo wapi?”

Maisha yake hayakuwa sawa … hayakuwa sawa … hayakuwa sawa.

Usiku mzima hakulala mpaka pale alipokuja kuamshwa kwa ajili ya safari. Walikwea ndege na ikawachukua muda mfupi tu kuwa ndani ya Ubelgiji.

Siku hiyo Joana akashinda kutazama ‘movies’ ili kupumzisha ubongo wake dhidi ya mawazo. Alitazama movies bandika bandua mpaka usiku wa saa sita.

Akapitiwa usingizi akiwa ameshikilia rimoti ya televisheni.

Kwenye mishale ya saa nane usiku, akashtushwa na hodi mlangoni. Alitazama televisheni, bado ilikuwa inaongea na kuonyesha. Akatazama saa, akaona ni saa nane.

Akatazama mlangoni.

“Nani?”




***
 
Back
Top Bottom