*ANGA LA WASHENZI --- 34*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
“Hakikisha.”
Nigaa akajua nini cha kufanya na pasipo kuuliza akatoka zake nje. Mkuu akalalia kiti na kushusha pumzi. Akatafakari zile picha, ila kwa macho yake zilikuwa sahihi na si za kubandikwa kiteknolojia. Ila hakuamini uwezo wa Panky kiasi hicho.
Amewezaje kitu ambacho Bigo ameshindwa?
Alitamani kujua.
ENDELEA
“Tayari, nimefanikiwa.” Ujumbe ulifika kwenye simu ya Jona toka kwa Panky. Jona akaupokea na tabasamu alafu akaujibu ujumbe huo.
“Basi fanya kama vile tulivyopanga.”
Panky akaupokea ujumbe huo, na kisha akaujibu:
“Hamna shida,” huku akielekea eneo lao la kazi. Mbele yake kulikuwa kuna mlango mkubwa wa chuma ukiwa umepachikwa bandiko jeupe lililosomeka ‘SPACE BUTTON’. Pembezoni mwa mlango huo kulikuwa kuna kifaa cha kuandikia ‘password’.
Panky akabofya hapo mara kadhaa na mara mlango ukafunguka. Akazama ndani na kupokelewa na wenzake ambao walimkumbatia na kumkaribisha kwa bashasha. Hawakutegemea kama Panky angerejea salama.
Baada ya muda kidogo, na hali kutulia, Panky akamtafuta Marwa ndani ya eneo lao. Eneo lilikuwa kubwa lililotapakaa mashine na tarakilishi. Kwa mbali kwenye kona akamwona mlengwa wake.
Ndani ya ofisi hiyo kuna vitengo kadhaa: ukarani, graphics, hacking na coding, na Marwa alikuwa kwenye kitengo cha graphics. Yeye na jamaa wawili.
Marwa alikuwa ni mwanaume mweusi mwenye nywele nyingi na chunusi kadha wa kadha usoni. Vidole vyake vilikuwa katika keyboard akichapa jambo. Macho yake yalikuwa yamezama kwenye kioo cha tarakilishi.
Kwa kumtazama tu, alionekana yupo bize. Panky akamjongea na kumsalimu. Akajibiwa pasipo kutazamwa. Marwa alikuwa anafanyia kazi picha fulani ambayo Panky aliona inapendeza sana ikikaa ukutani.
Marwa akasimamisha shughuli yake na kumtazama Panky. Alikuwa anamwona anampotezea muda ingali ana kazi lukuki za kufanya. Akauliza:
“Una shida gani?”
Panky akatabasamu. Kisha akamwambia Marwa kuna picha fulani aliiona akiifanyia kazi, ilimvutia na angependa kuiona.
“Nafanyia kazi picha nyingi Panky, unamaanisha ipi?”
Panky akajitahidi kuielezea picha yake iliyokichwani. Marwa akamwelewa, ila akamuuliza pasipo kumtazama:
“Unajua miiko ya kazi?”
“Najua, Marwa. Usijali, Moderator hatajua,” Panky akajibu.
Moderator ni msimamizi wa mule ndani. Ni mchina kwa utaifa na kazi yake ni kuhakikisha kila mtu anafanya kazi yake pasipo kuingiliana. Kuhakikisha wafanyakazi hawapangi jambo lolote kwa pamoja mule ndani, aidha kugoma, kuharibu mashine kwa kudhamiria, ama kupanga jambo la kitaaluma likaathiri kampuni.
Macho ya Moderator yanakuwa yanaambaa muda kwa muda, mahali kwa mahali, na masikio yake yanasikiza muda wote. Ujuzi wake pia kwenye mambo ya tarakilishi na mifumo yake yote, upo juu.
Kabla Marwa hajasema jambo, akasikia vishindo vya miguu. Na mara vikakoma na sauti ikauliza:
“Kuna tatizo hapa?” sauti nyembamba yenye lafudhi ya ki-mandarin. Alikuwa ni Moderator, mwanaume mfupi mwenye nywele za wastani. Macho yake yakisaidiwa na miwani maana yameshaharibiwa na mwanga wa tarakilishi kupitiliza.
Alikuwa amevalia shati jeusi kama vile sweta likimbana mpaka koo. Pamoja na suruali pana ya kitambaa cha rangi ya fedha, na mokasin nyeusi.
“Hamna tatizo,” Panky akawahi kujibu akitabasamu. “Nilikuwa namuuliza kama angeweza kuhudhuria sherehe ya mdogo wangu.” Akasema kwa haraka akijua fika Moderator hakuwa mzuri kwenye lugha hiyo.
Kisha akanyanyuka na kurejea tarakilishi yake. Kuna kazi akawa anazifanya ila akifikiria ni kwa namna gani anaweza kumuingia Marwa.
***
Baada ya maongezi yaliyokuwa yanafanyika kwa sauti ya chini chini, Mkuu, ama Sheng’ kama aitwavyo na wachache, akiwa anaongea na mwaname fulani mweusi mwenye nywele ndefu na macho madogo akiwa amevalia suti, akatikisa kichwa na kusema:
“This must be a plot.” (Huu lazima utakuwa ni mpango.) alisema kwa sauti yake ya kichina kiasi usijue kama ameongea lugha ya kiingereza. Mwanamke naye akatikisa kichwa kwa kukubali.
Watu hawa walikuwa wanaongelea mauaji ya kushtukuza ya Brokoli. Nani aliyeshiriki, na pia sababu iliyopelekea tukio hilo.
Mwanamke huyu mweusi ambaye yupo hapa, alikuwa ndiye yule ambaye Brokoli alikuwa akiwasiliana naye wakati akifanya tukio la mauaji ya Mudy na hata akiwa njia kumtafuta yule ambaye Mudy amemkabidhi nyaraka, yaani Kinoo.
“The document should be fetched! Otherwise we may awake the dead demon.” (Nyaraka lazima ipatikane! La sivyo tunaweza tukaamsha jinni lililolala.) alisema Sheng’ kwa msisitizo akimwambia yule mwanamke.
Punde mwanamke huyu akasimama na kuinamisha kichwa chake. Alafu akaondoka akitembea kikakamavu. Chini alikuwa amevalia viatu vya visigino virefu lakini akitembea kana kwamba amevaa raba.
Mwanamke huyu akaendea gari lake alilolipaki nje, IST nyeupe new Model, akazama ndani na kuondoa chombo.
Kwa jina waweza kumwita Gee.
***
Saa moja usiku …
Simu ilinguruma … ggrrrrrmmmm! Mara mbili kabla Glady hajaipokea na kuweka sikioni. Alikuwa amejilaza kitandani akiwa na mashoga zake wawili wote wakiwa wamevalia nguo za ndani tu.
“Vipi?” akauliza .
“Njoo hapa nje,” sauti ya kiume ikamjibu na mara simu ikakata. Wenzake wakawahi kumuuliza kama ni mteja, Glady akatikisa kichwa chake na kusema ni fala fulani aitwaye Mustapha.
Akajiveka khanga na kutoka nje. Akamkuta huko mwanaume aliyevalia ‘form six’ ya bluu na suruali nyeusi ya kadeti. Mkono wake wa kulia ulikuwa upo ndani ya POP, ameuning’iniza ukibembeshwa na kamba uliyodaka shingo.
Mwanaume huyu alikuwa ndiye yule aliyezama matatizoni na Lee kwa kushikilia nyaraka isiyo ya kwake. Glady akamtazama mkono wake uliovunjwa, alafu akamuuliza:
“Unataka nini?”
Mustapha akamwambia yupo pale kwa ajili ya kupata taarifa za yule mchina, Lee. Kwa alimchofanyia, kamwe hawezi kumwacha salama!
“Vita aliyoianzisha, kamwe haitaisha. Nitahakikisha ananijua mimi ni nani, na si kila mtu ni wa kumchezea!”
Glady akaangua kicheko.
“Mustapa, ulishindwa siku ile. Au unataka uuawe kabisa?”
Mustapha akamsisitizia apewe taarifa za huyo mchina alafu atakuja kumpatia taarifa baadae juu ya nini alichomfanyia. Glady akamwambia hana taarifa yoyote ya Lee. Alikutana naye klabuni na kuachana huko huko.
Mustapha hakuamini. Na kwa kutaka taarifa hiyo ya Lee, akamwambia Glady kwamba ile nyaraka ambayo Lee alikuwa anaitaka na kuichukua, wanayo. Na muda si mrefu watajua kuna nini ndani yake.
Glady akaagua tena kicheko. Alijua Mustapha anaongopa.
“Unatolea wapi na uliitoa?” akauliza. Mustapha akatoa simu yake kubwa na kumwonyesha Glady picha. Kumbe mwanaume huyo alikuwa amepiga picha ile nyaraka ya Lee, picha zimetunzwa kwenye gallery!
Glady akashangazwa.
“Ila we Mustapha una hatari!”
“Hii lazima itakuwa dili. Kwa namna alivyokuwa anaitafuta vile, itakuwa dili tu!”
“Sasa utaelewa nini humo na kimeandikwa kichina?”
“Aaaggh! Unadhani hakuna watu wanaojua kichina? Wachina wapo wangapi Kariakoo?”
Mustapha akamtaka sasa Glady amsaidie kupata taarifa za Lee, ili na yeye aweze kunufaika na chochote kitu kitakachopatikana humo. Taarifa hizo za Lee si tu kwamba zitamsaidia Mustapha kulipiza kisasi, bali pia zitawasaidia kujua namna gani watanufaika na nyaraka ile endapo wakiona kuna mhitaji wa yule ‘mchina’.
“Mustapha, kweli sina!” Glady akajibu. “Lakini naahidi kukutafutia. Nipe muda kidogo.”
Wakaachana kwa ahadi hiyo.
***
Saa tatu usiku…
Jona amesimama mbele ya karatasi zake za kuchorea, anatazama jambo.
Anafungua karatasi ya kwanza na kisha ya pili. karatasi hizo zina picha ya mkewe na mwanae. Anazitazama kwa muda kabla hajapindua karatasi nyingine mpya na kuanza kuchora mchoro mpya akitengeneza msingi kwa penseli ya kawaida.
Ilikuwa ni picha ya mtoto anachora. Na hakuwa anarejelea popote pale isipokuwa kichwani kwake.
Akiwa anaendelea kuchora mchoro huo, akili yake ipo kwenye amani na macho yake yakizingatia kazi anayoifanya, mara anasikia sauti ya honi huko nje. Anasita na kujiuliza ni nani huyo. Hakuwa na miadi na yoyote, na ule ulikuwa ni muda wa usiku.
Akaendea dirisha na kuchungulia. Akaona gari kubwa, VX rangi ya fedha. Akiwa hapo hapo anatathmini, akaona kuna mtu mmoja ameshuka toka kwenye gari hilo. Macho yake nyuma ya miwani yakatambuo umbo la mgeni huyo.
Alikuwa ni Mh. Eliakimu!
Muda huo! Akastaajabu. Akateka bunduki ndogo na kuikobeka nyuma ya kiuno, alafu akaendea geti na kumkarimu mgeni. Alikuwa amebeba tahadhari zote akiwa tayari kwa lolote linaloweza kutokea.
Mheshimiwa alikuwa ameongozana na bodyguard, mwanaume mrefu mweusi mwenye misuli mipana. Bodyguard huyo akaamriwa abakie nje wakati Mheshimiwa akiingia ndani na kuketi kochini.
“Sikutegemea ujio wako, vipi mheshimiwa?”
Mh. Eliakimu akashusha kwanza pumzi ndefu. Hakuwa anajua wapi pa kuanzia. Kujileta kwake kwa Jona kulikuwa hatari kwake na kwa siri zake, ila ndiyo hivyo hakuwa na namna! Maji yalikuwa yamemfika shingoni.
“Jona,” Mheshimiwa akaita. “Achana na yote yaliyopita. Najua kuna mambo ambayo yalitokea hapa kati, nisingependa kuyaongelea kwa sasa maana si muda muafaka. Nimekuja hapa maana nina shida na ninahitaji tena msaada wako.”
Jona alikuwa kimya akimtazama. Mheshimiwa akameza kwanza mate, alafu akasema:
“Nade ametekwa, naomba unisaidie kumuokoa.”
***