Miss Zomboko
JF-Expert Member
- May 18, 2014
- 4,599
- 9,532
Makada watano CHADEMA mbaroni kwa tuhuma za makosa mtandaoni
MAKADA watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Arusha, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuingilia mifumo ya mawasiliano ya kibenki.
Vilevile, wanatuhumiwa kuendesha mafunzo batili yanayolenga kutenda uhalifu wa kijinai katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu.
Jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Salum Hamduni, alithibitisha jeshi hilo linawashikilia watu hao baada ya kuwakamata Oktoba 5 mwaka huu majira ya saa 11:45 jioni.
“Polisi ilipokea taarifa kuwapo kwa watu hao kwenye ofisi binafsi za aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini (Godbless Lema) zilizoko Mtaa wa Esso, ambako kumekuwa na kawaida ya watu kukusanyika kuendesha mafunzo ya kulenga kutenda uhalifu wa kijinai unaohusishwa na kuingilia mifumo ya mawasiliano ya kibenki.
“Sasa, baada ya taarifa hizo kupokewa, wapelelezi walifika eneo hilo kufanya uchunguzi. Askari wapepelezi walikwenda kwa nia ya kufanya upekuzi kwenye ofisi hizo na kukamata watu wote.
“Kumekuwa na taarifa ambazo zilikuwa zinazagaa kwenye mitandao ya kijamii watu wasiofahamika wamevamia, hapana! Ni Jeshi la Polisi na askari wake walikuwa wamevaa 'uniform' (sare)," alisema.
Kwa mujibu wa Kamanda Hamduni, waliokamatwa ni mdogo wake na Lema aitwaye Nelson Lema (31), mkazi wa Arusha ambaye ni mfanyabiashara.
Wengine ni Lazaro Viola (46), ambaye Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Arusha, mfanyabiashara Wilbad Tarimo, Joshua Lukumay, mfanyabiashara na Mohamed Omar (45) ambaye ni wakala wa mabasi.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kuhusiana na taarifa hizo na inakusudia kuchukua hatua nyingine za kisheria kwa kadri ambavyo ushahidi utapatikana.
Katika taarifa yake, Kamanda Hamduni, alisema taratibu za dhamana kwa watuhumiwa hao ziko wazi na zinaendelea kushughulikiwa, hivyo taratibu zikikamilika watapewa haki hiyo.
Alisema Jeshi la Polisi halijihusishi na siasa na kwamba wajibu wa jeshi hilo umeelezwa kwenye katiba.
KAULI YA LEMA
Akizungumzia tukio hilo katika mkutano wake na waandishi wa habari jana jijini hapa, mgombea ubunge wa Arusha Mjini ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Lema, alilaani kitendo akidai kuwa ni kinyume cha sheria.
Alisema askari polisi zaidi ya 30 walifika katika ofisi hizo huku wakiwa wamebeba silaha za moto na kufanya upekuzi kwenye ofisi hizo kwa zaidi ya saa tatu.
Kwa mujibu wa Lema, askari polisi hao walidai kuwa ofisini huko kulikuwa na wahamiaji haramu kutoka mataifa ya Kenya na Israel.
Lema alidai kuwa vitu vilivyochukuliwa na polisi ni pamoja na nyaraka za siri za chama, simu nane na kompyuta mpakato mbili.
Lema alisema: “Juzi majira ya saa 6:30 jioni, nilipokea taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa CHADEMA Arusha Mjini, kwamba maofisa wa Jeshi la Polisi walifika katika ngome hiyo na kuwakamata viongozi watano wa chama na kuchukua baadhi ya vifaa na nyaraka.
Alisema kuwa kutokana na polisi kuwakosa wahalifu waliodai kuwa wapo kwenye ofisi hizo, walibadilisha maelezo na kusema kuwa watu hao walikuwa kwenye mpango wa kuingilia mifumo ya kibenki kwa ajili ya kujipatia fedha za kuendesha uchaguzi.
Chanzo: IPP Media