KWA NINI ASKOFU AONGOZE KAMPENI YA KUUNDA TUME HURU YA UCHAGUZI NA KUANDIKWA KWA KATIBA MPYA?
Usiku wa Tarehe 3 Desemba 2020, niliwatangazia umma wa Watanzania na ulimwengu kwa ujumla kuhusu adhma yangu ya kuongoza Kampeni ya Kuunda Tume Huru ya Uchaguzi na Kuandikwa kwa Katiba Mpya ya Tanzania. Kampeni hiyo ambayo itaanza Januari 2021 itafanywa kwa njia ya Matembezi ya Hiali katika nchi nzima ambapo nitasafiri katika kila Mkoa na Wilaya za Tanzania (Bara na Visiwani). Pia, nitaweza kusafiri kwenda nje katika baadhi ya nchi kuonana na Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora).
Suala la Katiba Mpya na Tume Huru sio suala la vyama vya kisiasa pekee! Ni suala ambalo linamhusu kila Mtanzania. Huko nyuma, zoezi hili liliachiwa wanasiasa na tumeona madhara yake. Siku mwanasiasa mmoja aliposhika madaraka na kutamka kuwa Katiba Mpya sio kipaumbele chake, zoezi la kuandika Katiba Mpya likakoma mara moja pasipo kujali gharama zilizotumika huko nyuma.
Upinzani ambao ungelitegemewa kupiga kelele Bungeni kwa niaba ya wananchi sasa umeondolewa na hivyo Bunge limebaki la Chama kimoja ambacho Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais alitamka wazi kuwa Katiba Mpya sio kipaumbele kwake. Hii ina maana kuwa hata Tume Huru ya Uchaguzi ambayo kwa kiasi kikubwa ni zao la Katiba Mpya haiwezi kupatikana.
Tukikaa kimya sote, kuna hatari ya Bunge la Chama kimoja kufanya mabadiliko makubwa ya Katiba iliyopo kwa lengo la kuzidi kuongeza madaraka na mamlaka kwa watawala na hata kuoondoa zaidi mamlaka ya watu. Vyama vya Siasa ambavyo vimekatazwa kufanya Mikutano ya Hadhara na hata kufanya Maandamano, vimezidi kumalizwa nguvu kwa kuondolewa Bungeni kupitia Uchaguzi Mkuu ulioghubikwa na kila aina ya ubabe, nguvu za vyombo vya dola na ufisadi. Kwa sababu hiyo, sauti mbadala iliyokuwa itokee kupitia Vyama vya Upinzani sasa tusiitegemee kuwa itakuwa na nguvu ya kutosha! Tuna imani kuwa vyama vya Siasa vitatiwa nguvu kubwa baada ya kuona jitihada hizi za Kiaskofu. Bila shaka navyo vitaunga mkono juhudi hizi sambamba na asasi za kiraia!
Ni kwa sababu hiyo, mimi niliye Askofu, nimesikia msukumo mkubwa kutoka moyoni mwangu kuwa yanipasa kuchukua hatua ya kuwahamasisha na kuwaandaa Watanzania kwa ajili ya mabadiliko makubwa ya kijamii, kimwili, kiroho na kiuchumi yatakayotokana na Kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Kuandikwa kwa Katiba Mpya (Isaya 6:8-10).
Ni wazi kuwa kila jambo lazima liwe na mahali pa kuanzia na lazima pawepo na mtu au watu wa kulisemea. Ni dhahiri kuwa Watanzania katika wingi wa mamilioni yao wanataka na wanapenda mabadiliko makubwa. Changamoto iliyopo sasa ni nani wajitokeze kuwaongoza watu hawa kuelekea katika kilele cha mabadiliko hayo.
Hata wanachama na viongozi walio wengi wanaotokana na CCM wanapenda mabadiliko hayo lakini wanakosa ujasiri wa kupingana na Mwenyekiti wao aliyetamka wazi mbele ya hadhara kuwa Katiba Mpya sio kipaumbele kwake. Viongozi wengi wakuu wastaafu wa CCM na Serikali wangelipenda kuona na kushuhudia Katiba Mpya ikiandikwa, lakini itifaki za kiuongozi zinawazuia kupingana hadharani na mtazamo wa Rais aliyepo madarakani. Kwa sababu hiyo wanabakia kunung'unika chinichini.
Ni kwa sababu hiyo, Kampeni hii kuongozwa na Askofu ina umuhimu wake. Itakuwa ni Kampeni ya aina yake itakayoungwa mkono na makundi mengi ndani na nje ya nchi. Hata Malawi, Vyama vya Siasa viliposhindwa kuleta mabadiliko ya kidemokrasia, shinikizo kutoka kwa Maaskofu liliwezesha nchi kuyabusu mabadiliko mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Kwa neema ya Mungu mimi nipo tayari kwa ujasiri mkubwa. 'Nimeshamfunga paka kengele'! Maaskofu wengi pamoja na viongozi wengine wa dini wapo nyuma yangu katika hili. Lililo muhimu zaidi ni kuwa Mungu yupo nyuma na mbele yangu! Shime Watanzania! Tuungane wote pamoja pasipo kujali vyama, itikadi, dini, elimu, ukabila nk.
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Mkuu Emmaus Bandekile Mwamakula - Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania & Afrika Mashariki na Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Makanisa ya Moravian ya Uamsho Duniani