"Makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Falme ya Dubai kama yalivyo kwenye mkataba huu hayakubaliki kwa sababu zifuatatazo:
(1) Makubaliano yataleta mgogoro kati ya wananchi wa Tanganyika na wa Zanzibar na hivyo kuendelea kuhatarisha Muungano.
(a) Wakati mkataba umetiwa ..saini na Waziri Makame Mnyaa Mbarawa, Mzanzibari, kwa mamlaka aliyokasimiwa na Rais Samia Suluh Hassan, Mzanzibari pia, mkataba wenyewe unahusu bandari zote zilizopo upande wa Tanganyika peke yake.
(b) Bandari zote za Zanzibar hazihusiki na mkataba, licha ya ukweli kwamba ..bandari ni mojawapo ya Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Katiba ya sasa.
(c) Swali la wazi hapa ni, je, kama kweli mkataba huu una manufaa makubwa kwa nchi yetu kama inavyodaiwa na serikali na CCM na wapambe, kwa nini bandari za Zanzibar hazimo kwenye mkataba huu?
(d) Katika mazingira haya, Watanganyika wana haki ya kuhisi kwamba Wazanzibari hawa wawili wanagawa mali za Tanganyika kwa wageni kwa faida zao binafsi, wakati wakilinda mali zao wenyewe.
(e) Kuuruhusu mkataba huu kuendelea ni kuruhusu chuki dhidi ya Wazanzibari kuanza kujengeka miongoni mwa Watanganyika. Huku ni kuhatarisha mahusiano katika ya Wazanzibari na Watanganyika jambo ambalo linahatarisha Muungano moja kwa moja.
2. Mkataba huu unahatarisha usalama na uhuru wa nchi yetu moja kwa moja.
(a) Mkataba unakabidhi bandari zote za Tanganyika kwa DP World na washirika wao wa kibiashara kwa muda usiojulikana na kwa manufaa ambayo hayajaelezwa wazi wazi;
(b) DP World sio tu ni kampuni ya kibiashara, bali pia ni kampuni inayomilikiwa moja kwa moja na Serikali ya Falme ya Dubai na inawakilisha maslahi ya kibiashara na ya kisiasa ya Serikali hiyo.
(c) Endapo kutatokea kutoelewana kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ...ya Falme ya Dubai au Falme ya Nchi za Kiarabu (UAE), ambayo Dubai ni mojawapo ya nchi washirika maslahi ya Tanzania yatakuwa kwenye hatari kubwa na ya wazi.
(d) Mkataba unabadilisha au kukiuka sio tu Katiba na sheria za Tanzania, unaweza pia kupelekea kuvunja mikataba na ..sheria za kimataifa na hivyo kupelekea Tanzania kuwa na mahusiano mabaya na jumuiya ya kimataifa.
3. Mkataba utapelekea unyang'anyi mkubwa wa ardhi za wananchi utakaofanywa na serikali yetu ili kutekeleza masharti ya mkataba huu.
(a) Mkataba unataka serikali ya Tanzania kuipatia DP World na washirika wake ardhi yoyote watakayoihitaji kwa ajili ya shughuli zao;
..(b) Mkataba unataka serikali kuhakikisha kwamba ardhi hizo hazina mmiliki au mwenye maslahi mwingine yeyote kwenye ardhi hizo.
(c) Katika mazingira halisi ya nchi yetu ambako serikali imekuwa ndio tishio kubwa la haki za ardhi za wananchi wetu, mkataba huu utachochea ..migogoro mikubwa zaidi ya ardhi na uonevu mkubwa dhidi ya wananchi.
(d) Ardhi ambazo DP World watazikabidhiwa na serikali ya Tanzania chini ya mkataba huu hazina ukomo wa umiliki wake kwa sababu mkataba wenyewe hauna ukomo unaojulikana.
4. Mkataba huu unaendeleza utamaduni wa kuwapa wawekezaji wa nje manufaa makubwa ya kikodi na faida nyingine, ambao umesababisha taifa letu kupoteza utajiri na rasilimali zake asilia, kama vile madini, bila kupata manufaa yoyote ya maana.
(a) Chini ya mkataba huu, misamaha ya kodi na manufaa mengine kwa DP World yamewekewa ulinzi ule ule wa kutobadilishwa wakati wa kipindi chote cha mkataba, kama ilivyokuwa kwenye madini na sekta nyingine za uchumi wetu.
(b) Zaidi ya ahadi za jumla jumla za manufaa kwa nchi yetu, mkataba huu hauonyeshi manufaa ya wazi wazi kwa nchi yetu na kwa uchumi wetu." Mhe. Freeman Mbowe