Baba wa marehemu Shukran Amos Said, mwanamke anayedaiwa kuuawa na mwanaume aliyefahamika kwa jina la Khatibu Mfaume katika eneo la Maili Mbili, jijini Dodoma, amekataa kuruhusu mwili wa binti yake kuzikwa na familia ya mume wake wa zamani kutokana na mgogoro wa mahari.
Inadaiwa kuwa baada ya tukio hilo, Khatibu Mfaume alijisalimisha kwa Jeshi la Polisi. Wakati familia zikianza kujipanga kwa ajili ya mazishi, familia ya mume wa zamani wa marehemu, ambaye alizaa naye watoto wawili, iliamua kushughulikia msiba huo na taratibu za mazishi.
Hata hivyo, hatua hiyo imekumbana na pingamizi kutoka kwa baba wa marehemu, Amos Said, ambaye amesema hataruhusu mwili wa binti yake kuzikwa na familia hiyo hadi suala la mahari litakapopatiwa ufumbuzi.
Akieleza msimamo wake, mzee Amos Said amesema binti yake alizaa watoto wawili na mume wake wa zamani, lakini hadi wakati huo hakukuwa na malipo ya mahari yaliyokamilishwa kwa familia yake.
Amesema yuko tayari kuruhusu familia ya mume wa zamani wa binti yake kuendelea na mazishi endapo italipa shilingi milioni moja na laki tano (TSh 1,500,000), kiasi ambacho amesema ni mahari inayodaiwa.
Aidha, amesema iwapo familia hiyo itashindwa kulipa kiasi hicho, atachukua jukumu la kumzika binti yake kwa taratibu za Kikristo, licha ya kuwa marehemu alibadili dini baada ya kuolewa na mume wake wa kwanza.
Mgogoro huo umeibuka wakati familia zikiwa katika kipindi cha majonzi kufuatia kifo cha Shukran Amos Said, ambaye kifo chake kinadaiwa kuhusishwa na mwanaume aliyekuwa katika uhusiano naye