Kuna kila dalili kwamba SGR itakapokamilika bado tutakuwa na reli ya zamani ikitoa huduma. Hapo mwanzo nilifikiri kwamba reli ya zamani itaendelea kutoa huduma kwa matawi ya Tabora - Mpanda, na labda Dar -es Salaam kwenda Tanga, Moshi na Arusha, ambako sijasikia lolote juu ya kuwepo kwa SGR.
Lakini kila habari zinapotolewa, sisikii hili likiwekwa wazi. Ninasikia tu kuhusu SGR sambamba na reli ya zamani, na manunuzi yakifanywa kwa ajili ya reli zote mbili.
Kwa nini tuendelee kuhudumia na kuwekeza kwenye reli zote mbili? Ni kupanua wigo wa huduma katika bei, kwamba SGR iwe kwa mabwana na reli ya zamani watwana?
Ninachelea kwamba uwepo wa SGR utafanya reli ya zamani iendeshwe kwa hasara iwapo tutaendelea kuitumia. Nilidhani labda SGR ikikamilika reli ya zamani itauzwa kama vyuma chakavu.
Labda ni ule uswahili wetu tu wa kiafrika, tunaendelea kutaka kumiliki vitu vya zamani, tunashindwa kuvitupa hata kama tumenunua kitu kipya mbadala
India ni moja ya mataifa yenye mtandao mrefu zaidi wa reli duniani ikiwa na jumla ya km 65000, katika mtandao huo mrefu kuna track gauge za upana tofauti, zipo Broad gauge, Narrow gauge, Standard gauge na Meter Gauge. Reli zote hizi zinafanya kazi hazijatelekezwa, baadhi ya maeneo yaliyokuwa na meter gauge imebadilishwa kuwa Broad gauge.
USA ndiyo taifa lenye mtandao mrefu zaidi duniani ikiwa na jumla ya km 250,000 katika mtandao huo zipo reli za guage tofauti ikiwemo Wide gauge, Broad gauge nk
Hata wakoloni wetu Waingereza nao wana reli za upana tofauti na zote zinafanya kazi.
Ikiwa hao wakubwa walijenga reli mpya au kubadilisha baadhi na hawakuua za zamani sisi ni nani tutelekeze ya zamani?
Mleta mada unaweza tueleza madhara ya kuwa reli zenye upana tofauti?
Kwa Tanzania kuendelea na matumizi ya meter gauge kuna faida kubwa sana, yapo maeneo muhimu ambayo bado hayajafikiwa na SGR, mfano Tanga, Moshi, Arusha, Mpanda, Singida nk. huko kote kuna reli ya MGR lakini hakuna reli SGR.
Bandari ya Tanga ni moja ya bandari zenye kupokea mzigo mkubwa, kuna tatizo gani ikiendelea kuhudumiwa na MGR?
Hivi karibuni ilijengwa bandari ya Kalema iliyopo mkoa wa Katavi, hii ni bandari ya kimkakati inayotarajiwa kuhudumia jirani zetu hasa Congo kusini, tunajua kwamba Katavi haijafikiwa na mradi huu wa SGR, je bado tu hamuoni umuhimu wa kuendeleza reli ya mkoloni?
Kitu ambacho ningeshauri Serikali yetu ifanye ni kukaribisha wawekezaji binafsi kati usafirishaji wa reli ili kuleta ushindani kwa TRC, hii ndiyo njia pekee itakayo saidia kutoa huduma nzuri kwa wateja, mashirika mengi ya umma yameonyesha ufanisi duni, hata mataifa makubwa kama USA yana makampuni binafsi yanayofanya kazi kwenye mtandao wao wa reli.
Miundombinu ya reli ibaki kuwa mali ya serikali, yakaribishwe makampuni binafsi kufanya biashara ya usafirishaji relini na serikali ichukue tozo kwao, huku ikijikongoja na TRC yake, kwa kufanya hivyo tutashuhudia tofauti kubwa ya huduma kama ilivyo sasa kwenye mawasiano ya simu, TTCL vs Binafsi, ili nia njema ya Serikali ya kukuza sekta ya usafiri wa reli ifanikiwe hakuna namna nyingine zaidi ya kukaribisha sekta binafsi