Bajeti yazidi kupata wakosoaji yadaiwa ina mapungufu mengi
Waandishi Wetu, Dar
Mwananchi
WAKATI mjadala wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2008/09 ukitarajiwa kufikia tamati kesho, wanaharakati na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta), wameikosoa bajeti hiyo wakisema kwamba imejaa ahadi nyingi ambazo ni ngumu kutekelezeka.
Licha ya kuikosoa bajeti hiyo kwa kuwa na ahadi nyingi pia wamesema bajeti hiyo haikumwangalia mwananchi wa kawaida hivyo kuwa sawa na kiini macho.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Tucta, Nestory Ngulla, alisema bajeti hiyo imejaa maelezo mengi ya kisiasa badala ya kuelezea na kuonyesha takwimu zinazowezesha kufanyika tathmini yakinifu kuhusu kipato cha wananchi.
"Takwimu zinazotolewa na serikali kuhusu kukua kwa uchumi wa taifa (pato la taifa), bado hazitoshelezi katika kufanya tathmini yakinifu juu ya kukua, ama kushuka kwa kipato cha wananchi. Serikali bado haitoi takwimu zozote kuhusu mgawanyo wa pato la taifa ili kuwezesha wadau kutafakari kama kukua kwa uchumi huu kunawanufaisha wananchi wote," alisema Ngulla.
Alisema bajeti hiyo ni ngumu, kwa kuwa wembe wa kukata kodi bado upo palepale na kwamba, hakuna unafuu wowote kwa wananchi kwa sababu hata kima cha chini kinachosamehewa kodi ni cha mwaka 2007/08 cha Sh100,000.
"Hii ni danganya toto. Hakuna unafuu wowote. Kilio cha wafanyakazi kuhusu kodi inayotozwa kwenye mishahara yao, bado hakijazingatiwa hata kwenye bajeti ya 2008/09. Vyama vya wafanyakazi vimeitaka serikali kutotoza kodi kiwango cha chini ya mshahara unaokidhi mahitaji muhimu ya maisha, lakini hadi leo bado serikali imeng'ang'ania kukusanya kodi kutoka kwenye mishahara ya wafanyakazi ambao wameelemewa na kupanda kwa gharama za maisha, kwa vile tu ni rahisi kuikusanya," alisema Ngulla.
Alisema kiwango cha chini ya Sh100,000 ambacho ni kima cha chini cha serikali kilichotangazwa, kimesema kisikatwe kodi ni cha bajeti ya mwaka uliopita na wakati kuanzia mwaka huu wa fedha wafanyakazi wanatakiwa kulipwa Sh150,000 kama Tume ya Rais ya Kuboresha Mishahara ya Wafanyakazi wa Umma ilivyoshauri.
Ngulla aliwataka wabunge kuishinikiza serikali kuhakikisha kima cha chini cha mishahara ya watumishi ambacho hakipaswi kukatwa kodi kiwe Sh150,000 badala ya 100,000 ya sasa.
Alisema pia kumekuwapo na upotoshaji wa muda kwa umma unaofanywa na serikali kuhusu takwimu za mishahara wanayolipwa watumishi wa umma.
Alisema katika bajeti za serikali, mishahara kwa watumishi huelezwa kama asilimia saba ya pato la taifa au asilimia 45 ya pato la ndani ya serikali.
Alifahamisha kuwa fungu hilo la mishahara kwa wafanyakazi wa umma, limejaziwa utitiri wa posho ambazo mfanyakazi wa kawaida hanufaiki nazo kwa kuwa zinazoingizwa katika fungu la mishahara na kwamba wanaonufaika ni viongozi na maofisa wa ngazi za juu katika utumishi wa umma.
Akizungumzia kuhusu uchangiaji wa mapato ya ndani ya serikali kwa njia ya kodi, Ngulla alisema katika eneo hilo, pia zinahitajika takwimu zenye mchanganuo unaoonyesha mapato ya makundi mbalimbali ya jamii yanavyochangia katika mapato ya ndani ya serikali kwa njia ya kodi.
Ngulla alisema suala la serikali kila mwaka kutenga fedha zaidi kwa ajili ya kuboresha miundombinu nchini, ni ufisadi wa hali ya juu kwa sababu sekta hiyo, imeshindwa kuonyesha kwa vitendo utekelezaji wa miundombinu na kwamba hauendani na hali halisi.
Alisema serikali imeshindwa kuonyesha dhamira yake ya dhati katika kupunguza na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kuondoa matumizi yasiyo ya lazima na badala yake imeendelea kuongeza matumizi mabaya kwa kufanya ununuzi na utumiaji wa magari ya anasa (mashangingi).
Alihoji kwamba kwa nini viongozi wa kitaifa wanaendelea kutibiwa nje ya nchi kwa kutumia gharama kubwa, badala ya kutumia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili kuokoa fedha za umma zinazotumika kutibia viongozi hao pamoja na maafisa wa serikali nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kupunguza fedha zinazotumika kulipa posho na semina kwa viongozi hao.
Baadhi ya wanaharakati waliozungumza katika Ukumbi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), walisema bajeti ya mwaka 2008/2009, siyo ya wananchi kama inavyodaiwa, bali ni ya viongozi waendelee kuishi maisha bora.
Walisema bajeti hiyo imekuwa ni mzigo kwa wananchi wanaoishi kwa kipato cha chini, kwani haijawasaidia zaidi ya kuwapa wakati mgumu wa maisha kwa mara nyingine.
Tulidhani hii bajeti ni kwa ajili ya kuwasaidia wananchi, lakini naona inaendelea kutupa maisha magumu, wakati tulishaahidiwa maisha bora kwa kila Mtanzania. Sasa naona ni maisha bora kwa viongozi,� alisema Zainabu Msangi kutoka Chama cha Wanaharakati cha Hekima.
Kwa upande wake, Gemma Akilimali kutoka Shirikisho la Wanaharakati (FemAct) aliieleza bajeti hiyo kuwa, ni kwa ajili ya viongozi wala sio wananchi kutokana na kutoshirikishwa kwa wananchi katika upangaji wa bajeti hiyo.
Waliopanga bajeti hiyo ni viongozi wenyewe bila ya kuwashirikisha wananchi, hivyo wananchi wataendelea kuteseka huku viongozi wakiwa wanaendelea kuponda raha Masaki,�alisema.
Katika hatua nyingine, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema ina lengo la kupitia sheria ya biashara kwa lengo la kuweka viwango vipya vya kodi ya Sh400 kwa lita ya bia na vinywaji vikali Sh500 kwa kila sigara elfu moja zinazoingizwa Visiwani Zanzibar.
Hayo yameelezwa katika hotuba ya Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2008/09 katika Baraza la Wawakilishi jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi anayeshughulikia (Fedha na Uchumi), Dk Mwinyihaji Makame Mwadini wakati akisoma bajeti hiyo.
Dk Mwinyihaji alisema serikali imekusudia kuchukua hatua za kupunguza matumizi ya vinywaji vikali na sigara kutokana na vinywaji hivyo kukithiri matumizi yake.
Kutokana na athari za kiafya kwa matumizi ya bidhaa hizi, serikali imekusudia kuchukua hatua za kupunguza matumizi yake na sheria ya biashara, itapitiwa kwa lengo la kupunguza matumizi yake pia,� alifafanua Dk Mwinyihaji.
Waziri huyo alisema bajeti ya mwaka huu imepewa jina la Bajeti ya Maendeleo kutokana na fedha nyingi kutegwa kwa lengo la kuwaletea wananchi wa Unguja na Pemba maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.
Ni bajeti ya maendeleo kwa sababu, sehemu kubwa ya bajeti imeelekezwa kwenye matumizi ya maendeleo kuliko matumizi ya kawaida kama ilivyokuwa katika bajeti zilizopita, alisema waziri huyo.
Alisema kwamba katika mwaka ujao wa fedha, matumizi ya maendeleo yamekuwa makubwa ikilinganishwa na matumizi ya kazi za kawaida kwa Sh42.8 bilioni ikiwa sawa na asilimia 28.7
Alisema ukuaji wa uchumi wa Zanzibar ulifikia asilimia 6.5 na kupelekea pato la taifa kufikia Sh588.5 bilioni mwaka 2007 kutoka ukusanyaji wa asilimia 6.1 mwaka wa 2006 ikiwa ni sawa na kuwa, wastani wa pato la mtu binafsi umeongezeka kwa asilimia 13 kutoka Sh 459,000 na kufikia Sh518,000 kwa mwaka.
Dk Mwinyihaji alisema angezeko la asilimia 34.5 katika thamani ya shughuli za ujenzi kutoka Sh 38.3 bilioni mwaka 2006 hadi Sh 51.5 bilioni mwaka 2007.
Ni matarajio yetu kwamba kwa mwelekeo huu, kasi ya ukuaji wa uchumi itakuwa kubwa zaidi kwa mwaka ujao na hivyo hali za maisha za wananchi zitakuwa bora ,� alisema Dk Mwinyihaji.
Alisema vichocheo vingine vinavyochangia mapato ni kuongezeka kwa idadi ya watalii walioingia nchini kutoka 137,111 mwaka juzi hadi jumla ya watalii 143,265 mwaka 2007 sawa na ongezeko la asilimia 4.5.
Dk Mwinyihaji aliwaeleza wajumbe kwamba, sekta ya huduma ya jamii bado inaendelea kuongoza katika mchango wa pato la taifa, ambapo mchango wake uliongezeka kidogo kutoka asilimia 43.5 kwa mwaka 2006 hadi asilimia 43.9 kwa mwaka 2007.
Pia aliitaja sekta ya viwanda kuwa nayo iliongezeka kutoka asilimia 14.8 kwa mwaka 2006 na kufikia asilimia 15.4 kwa mwaka 2007 ongezeko ambalo limetokana na mchango wa sekta ya ujenzi ulioongezeka kidogo kutoka asilimia 7.5 mwaka 2006 hadi asilimia 8.8 mwaka 2007.
Kwa upande wa mchango wa sekta ya kilimo, Dk Mwinyihaji alisema umepungua kutoka asilimia 30 kwa mwaka 2006 kufikia asilimia 27 mwaka 2007 kutokana na ukuaji wake kwa mwaka 2006 kutokuwa wa kawaida kufuatia ukuaji mkubwa wa asilimia 19 kutoka mwaka 2005.
Katika hatua nyingine, Midraji Ibrahim anaripoti kutoka Dodoma kuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo amekiri kutofautiana kwa takwimu kwenye vitabu vinne vya bajeti, huku akibainisha sababu mbalimbali.
Akitoa tamko la serikali bungeni jana usiku, Mkulo alisema, hatua hiyo ilisababishwa na vitabu hivyo kuchapishwa mwishoni mwa Mei, huku bajeti aliyowasilisha ikiidhinishwa na serikali saa mbili kabla ya kusomwa.
Pia, Mkulo alisema, kikao cha mawaziri wa fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kilikuwa kifanyike mapema, lakini Kenya waliomba kusogezwa kwa tarehe kutokana na matatizo yaliyotokea na kilifanyika Juni 2, mwaka huu.
Alisema kutokana na vitabu hivyo kuchapishwa mapema, baadhi ya mambo mbalimbali ikiwemo utekelezaji umebadilika na hivyo kusababisha takwimu zilizomo kutofautiana na zile za bajeti aliyowasilisha.
Aliongeza kuwa, bajeti aliyowasilisha bungeni ilitoa hali halisi na kwamba, tayari marekebisho yamefanywa ili kugawiwa wabunge ambayo yataoana na kitabu cha bajeti.
Waziri Mkulo alisema, pia hisa za NMB nazo zimesababisha kutofautiana kwa bajeti hiyo kwa sababu, zilithaminiwa kwa bei ndogo, lakini thamani imeongezeka na kufikia Sh60 bilioni.
Sababu nyingine ni wafadhili kutothibitisha mapema kuunga mkono bajeti na kwamba, walichelewa na kuthibitisha mwishoni mwa Mei tofauti na miaka mingine wanavyofanya.
Aliwasifu wapinzani kwa kubaini kasoro hizo na kwamba, serikali ni sikivu huku akiwataka kuendelea kwa sababu, inaonyesha wanasoma sana.
Mbunge wa Karaatu (Chadema), Dk Willibroad Slaa juzi akichangia bajeti hiyo alisema, hataunga mkono hadi vitabu hivyo vitakaporekebishwa kwa sababu vinatofautiana kwa Sh130 bilioni.
Imeandaliwa na Tausi Mbowe, Hussein Issa, Fatma Aziz Dar na Salma Said kutoka Zanzibar.