Nimeliokota hili andiko sehemu limetupwa;
Mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ulisitishwa kufuatia majadiliano yenye tija yaliyofanywa mwaka 2018. Serikali ilibaini masharti magumu yanayoweka rehani uchumi wa nchi na kuhatarisha uhuru wa nchi yetu. Kwa mantiki hii wajuvi wa mambo katika mimbali za "Ujasusi wa Kidola na Kiuchumi" watang'amua na kuunga mkono zuio hilo la serikali.
Kupitia majadiliano hayo yaliyojikita katika viunga vya ujasusi wa kidola na kiuchumi, serikali ilibaini baadhi ya masharti yafuatayo ambao ni hatarishi kwa uchumi wetu;
1) Wachina walihitaji kuendesha Bandari hiyo baada ya ujenzi bila kuingiliwa, jukumu la kupanga bei liwe mikononi mwao.
2) Pia ukanda huo wa Bandari ya Bagamoyo (Tanga-Mtwara), kusiwe na uboreshwaji wa Bandari zingine, mathalani Bandari za Tanga, Dar es Salaam, Mafia na Mtwara zibaki kama zilivyo kitu kinachohatarisha ukuaji wake na kwa namna yoyote ile zingekufa kifo cha asili.
3) Eneo lote la ujenzi wa viwanda na mji wa kisasa wachina walihitaji umiliki wa hati kwa zaidi ya miaka 33 (zaidi ya miongo mitatu). Mbaya zaidi walihitaji kama Faida yao itakuwa haijapatikana kwa miaka 33 basi hata kwa miaka 99 wangeweza kuendelea kumiliki na kukusanya kodi.
4) Wachina walihitaji pia wawe wasajili, wasimamizi wa viwanda vyote vitakavyowekezwa eneo hilo sanjari na ukusanyaji wa kodi zote zitakazolipwa eneo huska.
Sintofahamu inaongezeka pale ambapo, ni wachina hao hao ambao wangetumika kutoa tafsiri ya kimahesabu kuhusu faida au hasara kutokana na 100% ya kumiliki au kuratibu mchakato mzima wa mapato katika eneo hilo. Hapa nalazimika kukumbuka usemi wa kiratini, "Quis Custodient, Ipsos Custodes?" Kwa tafsiri isiyo rasmi ni, "Who watches the watchers?" Au "Nani atawalinda walinzi wetu," ilihali wenye mali tumewekwa kando na wageni wamepewa fursa ya kufanya wanavyotaka.
Katika viunga vya ujasusi wa kidola na kiuchumi kwa namna yoyote ile lazima wachina wangetuchakachua ili watuvune vya kutosha. Maana wao ndio wangekuwa walinzi wa 100% wa mapato yanayoingia na hata kampuni za ukaguzi ili ionekane wamepata hasara ili kupata tiketi ya kuongezewa muda wa kumiliki na kukusanya mapato.
Aina hii ya makubaliano kandamizi ndio imepelekea Bandari ya Hambantota, Sri Lanka kuchukuliwa na kumilikiwa na China kwa 99%. Pia Uwanja wa Ndege wa Mattala Rajapaksa, Sri Lanka kumilikiwa na China kwa 70%. Ikiwa ni zao la kushindwa kulipa mikopo iliyotegwa katika mtego wa falsafa za "Quis Custodient, Ipsos Custodes."
Rejea andiko lililoandikwa na Institute for Security Studies Africa mwaka 2017 lenye kichwa cha habari, "Lessons from Sri Lanka on China's 'debt-trap diplomacy."
Aidha, rejea andiko ambalo liliandikwa na The Diplomat mwaka 2017 lenye kichwa cha habari, "Sri Lanka's Debt and China's Money," sanjari na andiko la mwaka 2018 lenye kichwa cha habari, "Does Debt Pay? China and the Politics of Investment in Sri Lanka."
Nawiwa kuwaomba watanzania wenzangu kuyatafta maarifa ambayo yamefichwa katika Vitabu au maandishi ili kubaini propaganda zinazofanywa na baadhi ya watu kutetea mradi wa Bagamoyo uendelee kwa maslahi binafsi paspo kuutizama ukweli kwa maslahi mapana ya taifa.
Aidha, niipongeze serikali ya awamu ya 5 kwa kuonyesha ukomavu wa hali ya juu katika viunga vya ujasusi wa kidola na kiuchumi. Hii ni zaidi ya tafakuri tunduizi ya kukataa makubaliano yanayotweza utu wa Taifa letu, kupoka Uhuru wa nchi na kuweka rehani uchumi wa nchi yetu kwa faida ya China.