Bei za mafuta zawakamua Watanzania wakati migogoro ya Mashariki ya Kati ukiendelea

Bei za mafuta zawakamua Watanzania wakati migogoro ya Mashariki ya Kati ukiendelea

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,310
Reaction score
1,265
VCG31N1350174301.jpg


Kila asubuhi kabla ya jua kuchomoza, Herry Msese huwa anaendesha daladala yake na kupita mitaa yenye shughuli nyingi ya Dar es Salaam, Tanzania, akiwasafirisha abiria wengi katika barabara yenye msongamano mkubwa.

Hata hivyo, katika wiki za hivi karibuni, mafuta yamekuwa yakimtia wasiwasi mkubwa.

"Hii ni changamoto kubwa," alisema dereva huyo wa daladala. "Kila siku, lazima nipeleke shilingi 110,000 za Tanzania (karibu dola 43 za Marekani) kwa mmiliki wa gari."

Awali, gharama za mafuta zilikuwa kwenye shilingi 90,000 kwa siku, lakini hivi karibuni zimefikia karibu shilingi 150,000.

Katika siku ambayo biashara ndio inakuwa nzuri zaidi, daladala hiyo inaweza kuingiza shilingi 260,000 tu. "Hii ina maana kwamba karibu kila senti ninayopata inatumika kwenye mafuta," alisema.

Ongezeko kubwa la bei ya mafuta linafuatia mzozo unaoongezeka katika Mashariki ya Kati unaozihusisha Marekani, Israel, na Iran. Minyororo ya usambazaji wa mafuta duniani iliyovurugika imesababisha bei ya mafuta ghafi kupanda na kuathiri nchi zinazoagiza mafuta kama Tanzania.

"Sijui nini kifanyike," Msese aliongeza. "Labda serikali inapaswa kupunguza kodi, au kushusha bei ya mafuta. Muhimu zaidi, vita hivi vinapaswa kuisha."

Baada ya kutoa gharama zote za kila siku, alibakiwa na shilingi 7,000 tu. "Ikiwa mambo yatakuwa mabaya zaidi, huenda nikalazimika kutafuta kazi nyingine."

Kwa sasa Tanzania ipo kwenye ongezeko kubwa zaidi la bei ya mafuta katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na viwango vipya vya bei vilivyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Chini ya viwango vipya vya bei, petroli sasa inauzwa kwa shilingi 3,820 kwa lita, kutoka shilingi 2,864 mwezi Machi. Dizeli imepanda hadi shilingi 3,806, huku mafuta ya taa sasa yakigharimu shilingi 3,684 kwa lita.

Ongezeko la bei ya mafuta linaenea kwa kasi katika uchumi wa Tanzania, na kuathiri usafiri, gharama za chakula, na bajeti za kaya.

Kwa upande wa Zena Omary, mama mwenye umri wa miaka 28 mwenye watoto watatu na mmiliki wa kibanda cha chakula katika soko la Mawasiliano, husafiri kila siku kutoka Kitunda hadi Ubungo, akitegemea usafiri wa umma na wakati mwingine bajaji.

"Nauli hazijaongezwa rasmi, lakini madereva wanatoza zaidi," alisema.

Zena alibainisha kuwa wateja wake, ambao wengi wao ni wasafiri wa kawaida, mara nyingi wana matatizo kama hayo. "Wananielezea hali yao, na ninaelewa kwa sababu na mimi pia ni mhanga."

Kadri bidhaa nyingi zinavyosafirishwa hadi jijini kwa magari yanayotegemea mafuta, Zena alilazimika kuongeza bei ya sahani ya chakula kutoka shilingi 2,000 hadi 2,500.

"Sikuwa na jinsi," alisema. "Gharama ya viungo na usafiri imeongezeka."

Licha ya marekebisho hayo, alikuwa na picha isiyoeleweka ya siku zijazo. "Katika wiki chache zijazo, sijui kitakachotokea," Zena alisema. "Nina wasiwasi kuhusu kama biashara yangu itadumu."

Katika Soko la Kariakoo, kitovu kikuu cha biashara jijini Dar es Salaam, Erick Matemba alikuwa akipambana kuweka biashara yake ya simu za mkononi iweze kuendelea.

"Simu nyingi tunazouza zinaagizwa kutoka Dubai. Lakini kwa takriban wiki tatu sasa, hatujapokea bidhaa mpya," alisema Mtanzania huyo mwenye umri wa miaka 35.

Usumbufu wa usambazaji ulipunguza usafirishaji, na kusababisha uhaba wa simu na vifaa vingine. Gharama kubwa za mafuta pia ziliongeza gharama za usafirishaji, huku safari ambayo hapo awali iligharimu shilingi 5,000 sasa inafikia kwenye shilingi 8,000.

"Tunalazimika kuongeza bei kidogo ili kufidia gharama hizi," Matemba alielezea.

Katika sehemu za mikoani kama vile Ngorongoro katika mkoa wa Arusha, bei za petroli zimepanda hata kupindukia shilingi 4,000 kwa lita. Miji mingine, ikiwemo Dodoma na Mwanza, pia imerekodi ongezeko kubwa.

Wachumi wanaonya kwamba kupanda kwa bei za mafuta kunaweza kusababisha shinikizo kubwa la mfumuko wa bei. Kadri gharama za usafiri na uzalishaji zinavyoongezeka, wafanyabiashara wanaweza kupitisha gharama hizi kwa walaji.

Pia kuna wasiwasi kuhusu shinikizo la sarafu. Kadri Tanzania inavyotumia dola zaidi za Marekani kuagiza mafuta, mahitaji ya fedha za kigeni yanaweza kuongezeka, na hivyo kudhoofisha shilingi ya Tanzania na kufanya uagizaji kuwa ghali zaidi.

Wakati uchumi wa Tanzania ukiendelea kuwa imara kiasi, huku ukuaji ukiendelea na viwango vya mfumuko wa bei vinavyoweza kudhibitiwa, kaya zinapitia mazingira magumu ya kiuchumi yanayotokana na nguvu zilizo nje ya mipaka yao.

Akirudi kwenye barabara za Dar es Salaam, Msese anaendelea na utaratibu wake wa kila siku. "Tunasubiri kuona tu jinsi mambo yatakavyokuwa," alisema. "Lakini kama mambo hayatabadilika, wengi wetu hatutaweza kuendelea."
 
Hili suala la mafuta kwa serikali hii isiyojali watu familia nyingi zitarudishwa kwenye umaskini
 
Back
Top Bottom