Ametupa zawadi ya kitabu ili tujielimishe masuala ya uongozi kwa kusoma kazi zake, kuzitafakari na kujipima tulipotoka, tulipo na tuendako tunapoitizama Tanzania ya leo na ile aliyoiongoza miaka 24 iliyopita.
Tunakupongeza kwa kuweka kumbukumbu ya kazi zako na uongozi wako kwenye maandiko ili tukujue, tujifunze na kujielimisha kutoka kwenye mkusanyiko wa hadithi ya maisha yako kama raia na pia katika nafasi ya kulitumika taifa kama Rais kuanzia mwaka 1995 hadi 2005.
Kupitia kitabu chako cha My life My Purpose, Maisha yangu , Makusudi yangu, umetuonyesha ulipotoka, ulipotembea, ulipo na ushauri kwa nchi yako ambayo umeipenda na kuendelea kuipigania hata sasa unapostaafu lakini si kwenye kuwatumikia Watanzania.
Tunaamini kitabu cha Mkapa kitasomwa iwe kwenye shule za msingi na hata kwenye taasisi za elimu ya juu. Ni Imani yatu kuwa kuwa Rais John Magufuli, wakati akikizindua anawashauri wadau kukitafsiri kwa Kiswahili ili kisomwe na wengi.
Tunaamini kitasomwa na wengi na kufuatiliwa na Watanzania wa aina mbalimbali kwa kuwa kina ujumbe na maudhui yanayowagusa vijana, wanasiasa, wasomi, wanahabari na kwa ujumla kila mmoja popote alipo.
Kitabu hiki kama ambavyo majumuisho yake yametolewa kwa ufupi na Mkuu wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Rwekaza Mukandala, kinaelezwa kuwa ni kitabu cha kwanza kuandikwa na kiongozi wa nchi kuhusu maisha yake binafsi.
Hongera, kwa kiongozi wetu ambaye kitabu chake kitaendelea kubaki kuwa tunu ya taifa na zaidi ya sana tutakitumia kujifunza kupitia kwake fikira na falsafa yake ikiendelea kuishi kwenye mawazo yetu.
Mkapa katika andiko lake ametukumbusha mengi kubwa ni kulipenda na kuhimiza watu kulisimamia taifa letu. Ametukumbusha kuwa na mshikamano na kukumbuka kuwa daima hatutakuwa na maendeleo kama hatutajitegemea.
Rais mstaafu anasema kama nchi ni lazima tuondokane na utegemezi tujitegemee na kutumia rasilimali zetu kwa maendeleo yetu wenyewe.
Lakini, pia anatukumbusha kuwa nchi yetu inapita katika harakati ambazo tunahitaji sana kuwa na uadilifu na uzalendo. Mkapa anatuonya kuwa kuna baadhi ya watu kwa nia zao wanaweza kukwamisha maendeleo ili kutimiza azma zao.
Anatueeleza jinsi ambavyo aliingizwa mkenge kwenye masuala ya fedha za akaunti ya madeni ya nje (EPA) ambayo mtihani wake uliishia kuwa kashfa ya EPA ambayo wengi wanaifahamu, lakini la msingi hapa si kulaumiana ila ni kuonyesha jinsi hamu ya kupata tija binafsi inavyoweza kuliangusha taifa.
Mkapa katika andiko lake anatushauri kuwa na sera na mipango ya kusaidia vijana. Anaeleza kuwa wako vijana wengi mno, lakini kama taifa hatujawa na sera za kuwaendeleza na kuwafanikisha ili wawe na maisha bora.
Rais huyu mstaafu hajawaacha wanasiasa, anawakumbusha kuwa inavyoelekea kila mtu anayejitumbukiza kwenye siasa ana lake jambo. Wapo wanaotaka kupata safari za ughaibuni, lakini pia kuna wafanyabiashara wanaolenga kujinufaisha na kupata mafanikio ya biashara zao.
Yote haya Mkapa anatukumbusha kuyatazama. Anasema ni vyema pia kuwa na baraza la kisheria la kitaalamu kupitia mikataba yetu ya kimataifa ili kuweka mambo kwa uwazi na kwa manufaa ya taifa letu.
Ni maoni yetu kuwa Mkapa ametufundisha na kutushauri, hivyo basi tuzingatie yote mema anayotushauri kwa ajili ya mustakabali wa nchi yetu.
Chanzo: Nipashe