Benki hazitoi taarifa za kutosha kuhusu makato ya akaunti, kama vile ada za kadi na makato ya kila mwezi. Mara nyingi, mteja hushawishiwa kufungua akaunti bila kuelezwa kwa uwazi gharama zote, kisha hujikuta akikata pesa bila taarifa ya kutosha.
Nilifungua akaunti CRDB miaka kadhaa iliyopita, lakini sikuitumia kwa muda mrefu. Mwaka huu nilipoanza kuitumia tena, nilifanya miamala kadhaa bila tatizo. Hata hivyo, leo nimekuta nimekatwa Sh 34,000, nikielezwa kuwa ni makato ya miaka miwili ambayo akaunti na kadi yangu vilikuwa havitumiki (dormant).
Kinachonisikitisha zaidi ni kwamba nilipoenda kufufua akaunti yangu, sikupewa taarifa yoyote kuhusu makato hayo. Pesa hizo nilikuwa nazihitaji kwa matumizi yangu ya sasa, na sasa nimejikuta katika wakati mgumu. Laiti ningeelezwa mapema, ningejipanga kulipa makato hayo wakati hali yangu ya kifedha ilikuwa nzuri zaidi, badala ya kukatwa ghafla bila taarifa.
Hili si tatizo pekee. Kuna wakati nilipohamisha pesa kutoka benki kwenda kwenye simu, mfumo haukunionyesha kiasi cha makato kabla ya kuthibitisha muamala. Baada ya kukamilisha muamala, ndipo nilipogundua kuwa Sh 5,000 zilikuwa zimekatwa. Kama ningejulishwa gharama hizo mapema, nisingeendelea na huduma hiyo.
Kwa ujumla, hali hii inanifanya nihisi kuwa huduma za benki hazimjali vya kutosha mteja wa kawaida. Badala ya kumsaidia mtu kupanga na kulinda fedha zake, benki zinaweza kumwongezea mzigo wa kifedha kupitia makato yasiyoelezwa kwa uwazi.
Tunaomba benki zitoe taarifa sahihi na za wazi kuhusu ada na makato yote kabla ya mteja kufungua akaunti, kufufua akaunti iliyolala au kufanya muamala wowote. Mteja anapaswa kuwa na nafasi ya kuelewa gharama na kuamua kama aendelee na huduma husika au la. Transparency na taarifa za mapema ni muhimu ili kujenga uaminifu kati ya benki na wateja wake.