Bondia Hassan Mgaya amefariki dunia, siku moja baada ya kupigwa TKO katika pambano la raundi sita lililofanyika Tandale kwa Mtogole, Dar es Salaam katika ukumbi wa Dunia Ndogo, na kupoteza fahamu dakika chache baadaye.
Mgaya alicheza pambano hilo lililofanyika Desemba 28, yaani usiku wa kuamkia leo, jijini Dar es Salaam. Pambano hilo, ambalo halikuwa la ubingwa, lilimkutanisha na mpinzani wake, Paulo Elias.
Kwa mujibu wa taarifa za kuaminika Mgaya alidondoka ulingoni na mwamuzi akamhesabia na kumpa mpinzani wake ushindi wa TKO. “Mgaya alipigwa na kwenda chini, mwamuzi akamhesabia, na ikawa TKO kwa sababu marehemu alishindwa kuendelea. Baada ya mwamuzi kumaliza kuhesabu, alitembea hatua kadhaa hapo hapo ulingoni kisha akaanguka na kuzimia,” amesema shuhuda.
Ameongeza; “Baada ya kuzimia, Mgaya alipewa huduma ya kwanza kutoka kwa madaktari waliokuwepo kwenye pambano na akazinduka, kisha akapelekwa Hospitali ya Sinza kwa ajili ya matibabu,” kilisema chanzo hicho.
Baada ya kufikishwa Hospitali ya Sinza, kutokana na hali yake alipatiwa rufaa ya kupelekwa Hospitali ya Mwananyamala ambako umauti umemkuta leo. Pambano hilo liliandaliwa na Golden Gloves wakishirikiana na Ngoswe Uwezo.
Kwa upande wake, bondia Cosmas Cheka, ambaye ni Mweka Hazina wa Chama cha Mabondia nchini Tanzania, amesema suala la msiba wa marehemu Mgaya wanalishughulikia wao kama mabondia kuanzia mwanzo hadi mazishi.
Pia, Cheka amesema chama cha mabondia wapo mbioni kuandaa utaratibu wa kumsimamisha mwandaaji wa pambano hilo, Haji Ngoswe. “Nimemshauri Mwenyekiti wetu wa Chama cha Mabondia Tanzania, Japhet Kaseba, kuandika barua ya kupeleka TPBRC ya kumsimamisha Promota Haji Ngoswe kwa kutoonyesha ushirikiano kwa bondia aliyefariki dunia,” amesema Cosmas Cheka akionesha masikitiko.
View attachment 3188183