Wiki iliyopita mbunge wa Kigoma mjini Mh. Peter Serukamba alitenda kosa la jinai ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia lugha ya matusi. Nimekuwa nikijiuliza kuhusu uwezo wa kufikiri wa Mh. Serukamba. hivi unawezaje kutoa tusi kubwa kiasi hicho bila kufikiria wanaokusikiliza? Mh hana watoto, mke , wazazi, marafiki, majirani na watu anaowaheshimu? Je akirudi nyumbani mtoto wake mdogo akimuuliza maana ya lile neno atamjibu vipi? Atawaangaliaje wapiga kura wake? Au ndio kauzu kuliko dagaa?
Lakini cha ajabu zaidi, mamlaka zinazohusika, kuanzia ofisi ya spika, kamati ya maadili ya bunge, Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Jeshi la Polisi havijamchukulia hatua yoyote licha ya ushahidi wa video uliopo. Spika , Mh Makinda ameshindwa kusimamia kauli yake ya kumpeleka Polisi mbuge atakayetoa lugha ya matusi bungeni. Kamati ya maaadili nayo iko kimya, CCM nayo imeshindwa kusema chochote kuhusu hilo na mwisho jeshi la polisi limekaa kimya badala ya kumkamata, kumhoji na kisha kumfikisha mahakani Mh Serukamba kwani ushahidi wa picha za video upo. Leo Bw. Lwakatare anakabiliwa na kesi mahakani kwa ushahidi wa video uliowekwa kwenye mitandao ya kijamii, kwanini isiwe hivyo kwa Mh. Serukamba?
Mwisho najaribu kujiuliza, ingekuwa ni Mh. Godbless Lema ametoa matusi hayo bungeni sijui ingekuwaje?