TOKA MAKTABA :
27 November 2019
Jafo atangaza matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, 2019
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amesema kuwa Chama cha Mapinduzi kimeshinda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Vijiji 12,260 sawa na asilimia 99.9, Mitaa 4263 sawa na asilimi 100 huku kikijinyakulia vitongoji 63,970 sawa na Asilimia 99.4.
Ameyasema hayo leo wakati akitoa taarifa ya matokeo ya uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ngazi ya Vijiji, Vitongoji na Mitaa uliofanyika tarehe 24/11/2019 kwa waandishi wa habari Ofisini kwake Mtumba Jijini Dodoma.
Mhe Jafo amesema katika mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 jumla ya nafasi 332,160 zilihusika katika uchaguzi ambapo kulikuwa na Vijiji 12,262, Mitaa 4,263, vitongoji, 63.992, wajumbe kundi la wanawake 106, 622, wajumbe kundi mchanganyiko 145,021.
Amefafanua kuwa jumla ya wananchi 555,036 kutoka vyama mbalimbali vya siasa walifanikiwa kuchukua fomu za kugombea ambapo wananchi waliorejesha fomu ni 539,993 sawa na asilimia 97.3.
Mhe. Jafo amesema kuwa Chama cha Mapinduzi kilipita bila kupingwa kwa jumla ya nafasi za uongozi 316, 474 ambapo nafasi ya Mwenyekiti wa Kijiji waliopita ni 12,028, Wenyeviti wa Vitongoji 62,927, Wenyeviti wa Mitaa 4,207, Wajume kundi la Wanawake 105,953 na Wajumbe kundi mchanganyiko 131, 359.
Ameitaja Mikoa ambayo wagombea wa nafasi zote za uongozi walipita bila kupingwa kupitia Chama cha Mapinduzi ni Tanga, Katavi, Ruvuma na Njombe
Ameendelea kusema kuwa Chama cha CUF kimepata nafasi moja katika ngazi ya wenyeviti wa vijiji, wajumbe kundi la wanawake wamepata nafasi tatu na wajumbe kundi mchanganyiko wamepata nafasi 14.
Mhe. Jafo amesema kwa upande wa Chadema, wenyeviti wa vijiji imeshinda nafasi moja, haikufanikiwa kupata Wenyeviti wa Mitaa, Wenyeviti wa vitongoji imepata nafasi 19, wajumbe kundi la wananawake imepata nafasi 39 na wajumbe kundi mchanganyiko nafasi 71.
Amesema Chama cha ACT wazalendo kilipata uongozi ngazi ya Wenyeviti wa Vitongoji nafasi moja, wajumbe kundi la wanawake nafasi moja na wajumbe mchangayiko 11 wakati chama cha UDP kilipata nafasi moja kwa upande wa wajumbe kundi la wanawake na chama cha DP kikipata nafasi moja.
Amevishukuru vyama vya siasa ambavyo vimeonesha ukomavu wa Kisiasa na kudumisha demokrasia nchini kwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Aidha amewashukuru wananchi, Viongozi wa Serikali katika ngazi ya Wizara , Taasisi, Idara za Serikali Mikoa , Wilaya, Halmashauri, Tarafa, Kata, Vijiji na Mtaa kwa kushiriki kikamilifu kusimamia na kukamilisha uchaguzi kwa amani.