Huu ni upuuzi mwingine ulioandikwa na gazeti la porojo za kila siku
Wananchi wailaani, waionya Chadema
Imeandikwa na Waandishi Wetu; Tarehe: 19th November 2010 @ 23:59 Imesomwa na watu: 167; Jumla ya maoni: 0
Habari Zaidi:
Wananchi wailaani, waionya Chadema
KITENDO cha wabunge wa Chadema kutoka ukumbi wa Bunge wakati Rais Jakaya Kikwete alipoanza kuhutubia Dodoma juzi, kimelaaniwa na kuelezwa kuwa utovu wa nidhamu, kukosa busara, uchochezi, kutokomaa kidemokrasia na chuki dhidi ya Serikali iliyoko madarakani.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili jana kuhusu kitendo hicho, walilaani na kuwaonya wabunge hao kutorudia tukio kama hilo kwa vile hawakuwatendea haki wananchi waliowachagua na badala yake wamewadhalilisha na kujidhalilisha pia, chama chao na kujipunguzia heshima kisiasa.
Spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Pius Msekwa, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa na Mbunge wa Vunjo Augustine Mrema (TLP) ni miongoni mwa waliolaani kitendo hicho.
Kiongozi hao walisema kwa nyakati tofauti kuwa kitendo hicho kimedhihirisha jinsi wabunge hao wanavyofanya mambo kwa kukurupuka na jazba, hatua inayowafanya wasahau kuwa wametumwa na wapiga kura wao, wawawakilishe katika chombo hicho ambacho sasa wanakisusa.
Pamoja na kulaani, Msekwa alisema kitendo hicho kimekiuka taratibu za Bunge na wananchi wanapaswa kukikemea na kukilaani kwa nguvu zote, wakati Bunge likitafakari namna sahihi ya kulimaliza, ikiwa ni pamoja na kutumia taratibu rasmi, zinazoweza kuamuliwa na Spika aliyeko madarakani, Anne Makinda kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Bunge.
Kwa mujibu wa Msekwa, Chadema wamepotea, kwa sababu wanatenda makosa huku wakijua madhara yake kwa chama chao, kwa jamii na kwa Serikali na licha ya Bunge kuwa na utaratibu wa kushughulikia suala kama hilo la utovu wa nidhamu, jamii nayo ina nafasi ya kulikomesha.
Msekwa alisema, "mwaka 1995 CUF walifanya mambo kama hayo lakini hawa (Chadema) wamekosea zaidi, kwa sababu wanamkataa Rais aliyewekwa madarakani kwa amani na kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi, ilhali wamekula kiapo cha uti."
Kwa maelezo yake, Chadema wanafikiri hiyo ndiyo njia sahihi ya kumaliza matatizo yao au namna pekee ya kumfedhehesha, kumkomoa na kumdhalilisha Rais Kikwete, huku wakisahau kuwa Kikwete si wanayemwakilisha bungeni, bali wapiga kura wao.
"Wakubali wakatae, Kikwete ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wanalazimika kumheshimu. Kugomea Bunge ili kuonesha kutomtambua kwao, hakusaidii na zaidi kumeonesha kuwa hawana nidhamu, busara na wanahitaji muda zaidi ili wakue kisiasa … wametenda makosa hawa na wanahitaji kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za Bunge."
Tendwa alisema kitendo hicho si cha kiungwana wala ujasiri, bali ni fedheha na kimeidhalilisha Chadema na wabunge wake.
Tendwa alisema wabunge hao wangetumia njia nyingine za kistaarabu, kuonesha hisia zao au kupingana na mambo wasiyopenda na si kususa na kutoka bungeni wakati Rais akihutubia.
Alisema kwa vile wabunge hao wamekiuka sheria na kanuni za Bunge, hakuna sheria nyingine inayoweza kuwaadhibu zaidi ya zile za Bunge kwa vile wamefanya hayo wakiwa ndani ya Bunge.
"Umefika wakati viongozi wa vyama vya siasa, lazima waoneshe ukomavu wao kisiasa na si kufanya uamuzi wa jazba na kuwaumiza wengi. "Chadema inawaumiza wapiga kura wake bila ya wao kuwa na makosa na hii si sahihi.
Wanajaribu kuonesha mambo ambayo si sawa kwa kumkataa Rais aliyechaguliwa kwa kufuata taratibu zote za kikatiba, wameonesha kukosa adabu na busara, siwaungi mkono kwa hilo," alisisitiza Tendwa.
Katika hatua nyingine, Mrema alisema hatasita kuwazomea Chadema kwa kukurupuka, watakaporejea bungeni siku na wakati watakapoona mambo nje ya Bunge yamewashinda.
Mrema alisema, alikuwa miongoni mwa waliowazomea wakati wakitoka bungeni na atakuwa wa kwanza kuwazomea watakaporejea kwa sababu kufanya hivyo kutathibitisha unafiki wao katika siasa.
"Kumkataa Rais halali hakuna tofauti sana na uhaini, sasa wenzetu hawa inabidi waangalie madhara yake kwa chama chao na wapiga kura wao," alisema.
Mrema aliongeza kuwa kwa walichokifanya Chadema, wanastahili adhabu ya Bunge kwa sababu wanachochea chuki miongoni mwa watu dhidi ya Serikali iliyoko madarakani, kutokana na ukweli kuwa inaongozwa na Rais wanayemkataa.
"Waliapa hawa na hiyo ina maana kuwa wanamkubali Rais, sasa ina maana gani kuingia bungeni na kutoka kwa dharau?
Inabidi Chadema waelewe kuwa Rais ni wa wote na kama wana yao, basi wafute taratibu zinazostahili ili kuyawasilisha na si ‘nataka sitaki' zao za kugoma wakati Bunge wanalihitaji."
Kituo cha Utawala Bora na Maendeleo Tanzania (Cegodeta), kimesema kitendo cha Chadema kutomtambua Kikwete, ni sawa na uasi unaoweza kusababisha uvunjifu wa amani na hatimaye machafuko na kinajiandaa kuifikisha mahakamani.
Taarifa ya Kituo hicho iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wake, Thomas Ngawaiya, iliitaka Chadema kuacha mara moja msimamo wake huo kwa kisingizio cha matokeo ‘kuchakachuliwa'.
"Cegodeta haiamini kwamba matokeo ya kura za urais yalichakachuliwa, kwa sababu Chadema walikuwa na mawakala kwenye kila kituo, kila kata na kila jimbo … mawakala wa vyama vya upinzani walikuwa wengi kwa ujumla wao, kuliko wa chama tawala," ilisema taarifa.
Ilikiri kuwa zilikuwapo kasoro ndogondogo katika takwimu za baadhi ya majimbo ambazo zilirekebishwa kama vile kurudiwa kwa uchaguzi katika baadhi ya majimbo, lakini hata hivyo, hizo zingeweza kubadilisha matokeo yaliyompa ushindi Kikwete.
"Chadema iache kudanganya wananchi. Inashangaza kwamba kati ya vyama saba vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi wa urais ni Chadema peke yake, ndiyo inayokataa kutambua matokeo, pengine inafanya hivyo kuridhisha wafadhili wao wa nje walioifadhili wakati wa kampeni," iliongeza.
Ilisema kutomtambua Rais ni kosa la jinai hasa baada ya wabunge wa Chadema kuapa kutii na kuiheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
"Kutii Katiba ya nchi ni pamoja na kumtambua Rais aliyechaguliwa kwa mujibu wa Katiba," ilisema.
Taarifa hiyo ilisema kwa kuwa Rais ni sehemu ya Bunge kitendo cha wabunge hao kususia huku wakipokea mishahara na posho ambayo ni jasho la wananchi, ni makosa na ni sawa na utapeli wa kisiasa.
C
egodeta imeipa Chadema mwezi mmoja kubadili msimamo wake huo vinginevyo itaifikisha mahakamani kwa kuvunja Katiba ya nchi.
Nayo CCM imesema tamko la Chadema kutotambua matokeo ya urais ni la uasi, na uhaini dhidi ya demokrasia na utawala wa nchi.
"Hii ni dalili kwamba Chadema wamechoshwa na amani iliyopo nchini; na sasa wanaandaa mazingira ya vurugu," ilisema katika tamko lake lililosainiwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati.
Iliitaka Chadema kutambua, kwamba uchaguzi ulishuhudiwa na waangalizi wa ndani na nje ya nchi na wote wakatoa taarifa kwamba ulikuwa huru na wa haki.
Ilisema ni muhimu Chadema ielewe, kwamba kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya nchi, matokeo ya Rais yakishatangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi hayawezi kuhojiwa na Mahakama au chombo chochote.
"Hivyo katika hatua hii matakwa ya Katiba yametimizwa na Rais yupo madarakani kwa mujibu wa Katiba.
Nia yao wanataka tuache kazi ya kushughulikia maendeleo ya wananchi ili tuingie katika mgogoro wa kikatiba utakaodumu muda mrefu na kuiingiza nchi katika misuguano na mzozo wa kisiasa na kuchelewesha maendeleo ya wananchi," CCM ilisema.
Iliongeza kuwa Chadema iliacha jukumu la msingi na la lazima la kuhamasisha watu kujitokeza kupiga kura, na badala yake ikawa bingwa wa kuhamasisha wafuasi wake kufanya fujo, vitisho na vurugu kulikosababisha watu kuogopa kujitokeza kupiga kura.
CCM ilisema Chadema wanataka kumridhisha na kumfariji Dk. Willibrod Slaa baada ya kushindwa katika uchaguzi. "Ni vema wamtafutie shughuli ya kufanya kuliko kutumia mbinu ya kukataa matokeo.
Kuhusu wabunge na madiwani wa Chadema, CCM ilishangaa kuona wanaendelea na kazi wakati hawatambui matokeo ya Rais, na hawamtambui Rais na Serikali yake na kusema huo ni unafiki wa hali ya juu.
"Vipi wanajiandaa kuunda Serikali kivuli wakati Serikali yenyewe kwa maoni yao haipo? Unapataje kivuli wakati kitu cha kutoa kivuli hakipo?" ilihoji.
"Tunawashauri wajiondoe bungeni haraka, vinginevyo wajiandae kuondolewa kwa Azimio la Bunge, hadi watakapogundua kwamba Rais yupo na Serikali ipo," ilisema taarifa.
Ilisema Chadema wanadhihirisha uongo wao kwa kuwa kila chama kilijaza Fomu Na. 21A, 21B na 21C kwa ajili ya matokeo ya urais, ubunge na udiwani.
Jambo la ajabu wanakataa matokeo ya Fomu Na. 21A na kukubali Fomu Na. 21B na 21C ambazo zinawahusu wabunge na madiwani.
"Tunawashauri viongozi wa Chadema, kwamba uchaguzi umekwisha, sasa tuache malumbano na misuguano ya kisiasa na tuanze kazi kwa pamoja ya kujenga nchi yetu," ilisema taarifa
Chanzo: Habari Leo