SEHEMU YA KWANZA
Salaam na heshima nyingi kwenu; Uongozi, Wanachama, Wapenzi na Wadau wote wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
Waswahili husema; haraka haraka haina baraka, simba mwendapole ndiye mla nyama, polepole ndio mwendo lakini pia haba na haba hujaza kibaba...
Kwanza, napenda kumshukuru sana MUNGU kwa siku hii ya leo; Jumapili tulivu yenye hali njema ya hewa na kuvutia.
Pili, naomba niende moja kwa moja kwenye lengo nililolikusudia kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA). Ninajua na ninafahamu kuwa mioyo yenu inaugua sana kwa sababu ni kwa muda mrefu sasa mmekuwa hamlipati lile ambalo mna shauku nalo na mnalitarajia sana; la kuwa chama tawala ama kwa lugha nyepesi kushika madaraka.
Neno la MUNGU Linasema: "Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua. Bali haja ya mtu ikipatikana ni mti wa UZIMA." (Mithali (Proverbs) 13:12)
Ni kweli mioyo yenu CHADEMA na Wana-CHADEMA inaugua; lakini hii si sababu ya kutaka kuyaambukiza maumivu hayo kwa kila Mtanzania kupitia kuwalisha sumu kwamba CCM hawafai! CCM ni wakatili! CCM ni wabaya! CCM ni wanyama! Halafu CHADEMA ndiyo chama pekee bora na kinachotakiwa kuwa madarakani! La hasha, huu si Uongozi! Si Utanzania na wala si Utu na Uzalendo hata kidogo; hii ni roho ya kichawi, ubinafsi na umimi, ambayo haijawahi kumfanikisha yeyote yule.
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) ambacho mmekuwa mkikivimbishia na kukitunishia misuli huku mkishindana nacho, kukitukana, kuwatukana wanachama na viongozi wake; wala si mchawi wenu, mchawi ni nyinyi wenyewe mnaotaka kulazimisha kushika madaraka wakati muda na wakati wenu bado; huku mkitaka kujenga UKUTA juu ya mchanga kwani msingi hamjauchimba bado.
CCM si CCM kama mnavyodhani; CCM ni Mwalimu Nyerere ambaye alisimama kuwaunganisha watanzania kwanza na si kuwagawa kama mnavyofanya, lakini pia alianzia kwenye ngazi ya jamii kwanza kama mwalimu na mdau wa elimu aliyejitolea kuipigania elimu ya Tanzania na Watanzania; hivyo alisimama kama mtoa Huduma za Kijamii kwa Watanzania na Tanzania kwanza; ndipo baada ya hapo akajiingiza kwenye masuala ya Kisiasa na kuunda Chama cha TANU ambayo baadaye ndiyo ikawa CCM.
Hii ndiyo sababu CCM inawaumiza kichwa CHADEMA, wana-CHADEMA na wapinzani wengine kutoka ndani na nje ya Tanzania; kwani CCM haikulala na kuamka ikajikuta imekuwa Chama Tawala hapana BIG NO! CCM si CCM kama nilivyotangulia kusema hapo awali, bali CCM ni Mwalimu Nyerere na CCM ni Legacy ya Mwalimu Nyerere; ambaye yeye aliujenga msingi wa CCM kwa kuanzia kwenye ngazi ya chini kabisa kwa jamii (akiwa kama Mwalimu); hivyo mtu (au chama chochote) anayetaka kuwa kama CCM inampasa kuwa na vitu vifuatavyo kwanza kabla ya yote ndipo siku moja awaze kupokea kijiti cha madaraka kutoka kwa CCM na wala si kuwapora wala kuwanyang'anya kwa nguvu.
- Afanye kama yale ambayo Mwalimu Nyerere alifanya na zaidi ya Mwalimu Nyerere aliyoyafanya ikiwemo kuanzia chini kabisa kwenye ngazi ya jamii; na hii si kupitia kushika nafasi za Uongozi wa Serikali za Mitaa wala kushika Nafasi za Uongozi wa Kata; bali kupitia mtu au Chama cha Kisiasa kufanya kazi kama Shirika la Kijamii lenye Kubuni na Kutekeleza Miradi midogo midogo na ya kati ya Kijamii yenye kunufaisha na kugusa mioyo ya jamii na mtu mmojammoja moja kwa moja.
- Heshima na Nidhamu kwa Chama Tawala; kwani mzazi ni mzazi siku zote atabaki kuwa mzazi haijalishi mapungufu aliyonayo, hivyo huwezi kumtukana Mama au Baba yako kisha kumpoka madaraka ya Umama au Ubaba wake kwa nguvu kisa kuna mahali amekosea; La hasha! Lazima atatumia Ubaba au Umama wake kukudhibiti kama mtoto wake na hayo madaraka hutayapata. Hii ndiyo sababu Neno la MUNGU Linasema: "Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa MUNGU; na ile iliyopo umeamriwa na MUNGU." (Warumi (Romans) 13:1)
Tafsiri yake ni kuwa; kuitukana mamlaka, kuipinga mamlaka pasipo kutumia hekima, kuiongelea vibaya mamlaka, kutaka kuipanda kichwani mamlaka na kufanya chochote kinachofanana na hayo ni kuenenda kinyume na NENO LA MUNGU; hivyo mamlaka ina uwezo wa kukufanya lolote na NENO LA MUNGU Limekwishasema kuhusu hili: "Kwa maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Fanya mema, nawe utapata sifa kwake; kwa kuwa yeye ni mtumishi wa MUNGU kwako kwa ajili ya mema. Lakini ufanyapo mabaya, ogopa; kwa maana hauchukui upanga bure; kwa kuwa ni Mtumishi wa MUNGU, amlipizaye kisasi mtenda mabaya kwa ajili ya ghadhabu." (Warumi (Romans) 13:3-4)
- Uvumilivu au Subira kwa sababu mchakato utakachukua muda kidogo
Kuanzisha msingi imara kuanzia chini kabisa kwenye ngazi ya jamii ndiyo sababu cheo maarufu cha Hayati Julius Kambarage Nyerere si
Rais (ambacho ni cheo cha juu au ukuta uliojengwa na msingi aliouweka); bali ni
Mwalimu (ambacho ni cheo cha msingi na ndio msingi wenyewe alioujenga)
Na hii pia ndiyo sababu hata ukienda kwenye vijiji vingi leo hii visivyo na mawasiliano ya simu, barabara na vyombo vya habari; lakini bado wanamjua Nyerere na bado wanaijua CCM.
Wazo lenu CHADEMA na chama chochote cha siasa cha upinzanzi kutaka na kupenda kushika madaraka si wazo baya ni wazo zuri sana; lakini naomba niwaulize maswali yafuatayo:-
- Je! Mpaka leo hii kwa kutumia ukubwa wa jina la chama chenu, ukubwa wa majina ya baadhi ya viongozi wenu, wadau wanaowaunga mkono kutoka ndani na nje ya tanzania lakini pia umri mlio nao; ni jambo lipi kubwa mmeshawahi kulifanya kwa manufaa na maslahi ya Tanzania na Watanzania?
- Je! Mpaka leo hii kwa kutumia ukubwa wa jina la chama chenu, ukubwa wa majina ya baadhi ya viongozi wenu, wadau wanaowaunga mkono kutoka ndani na nje ya tanzania lakini pia umri mlio nao; ni miradi mingapi ya elimu, kilimo, madini, ujasiriamali, uchumi au afya hata ile midogo na ya chini kabisa mmewahi kuibuni na kuitekeleza kwa Tanzania na Watanzania?
- Je! Mpaka leo hii kwa kutumia ukubwa wa jina la chama chenu, ukubwa wa majina ya baadhi ya viongozi wenu, wadau wanaowaunga mkono kutoka ndani na nje ya tanzania lakini pia umri mlio nao; ni mara ngapi mmekwishatatua changamoto za Watanzania ambazo CCM wameshindwa kuzitatua (mfano kwenye sekta ya Teknolojia, Kilimo, Elimu, Afya, na nyinginezo ambazo ni za Kijamii na si za Kisiasa)?
- Kama jibu ni hakuna; Je! Mnasubiri mpaka muingie madarakani ndipo muanze kujihusisha na Masuala ya Kijamii?
- Mfano mzuri ni wadau wa maendeleo wa kimataifa au wahisani (wafadhili) wa mashirika ya kijamii ambao wengi wao hutoa ufadhili kwa wingi kwa mashirika (organizations) ambazo zimeshafanya vitu tayari na yameshapiga hatua kufikia kati au mbali, huku baadhi ya wahisani hawa wakiwapa kisogo wale wenye mashirika yenye hatua za awali, changa na ambao bado hawajafanya chochote ila tu wana wazo zuri (good idea) ya kuanzisha shirika. Je! Unadhani ni kwa nini?
BWANA YESU KRISTO Amesema: "Mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu hata kile alichonacho atanyang'anywa" (Mathayo (Mathew) 25:29) (Luka (Luke) 19:26)
Kwa waraka huu, baada ya jana kutangazwa ya kuwa CHADEMA hamtashiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2025 kwa sababu ya nyinyi wenyewe kukataa kwa makusudi kutosaini kanuni za maadili ya uchaguzi; ni vyema sasa mkajipanga kurudi kwa jamii mkaihudumie jamii kwa huduma za kijamii ili mkawa-challenge CCM huko kwa vitendo na wala si kwa maneno kama mfanyavyo na ambavyo mmekuwa mkifanya siku zote.
Nendeni mkatumie ukubwa wa jina la chama chenu, ukubwa wa majina ya baadhi ya viongozi wenu, wadau wanaowaunga mkono kutoka ndani na nje ya Tanzania lakini pia umri mlio nao; mkawe Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mkahudumie jamii na kujenga msingi kwa jamii kwanza kabla hamjataka kuitawala jamii kisiasa...
Itaendelea