Asambaza vipeperushi kushutumu viongozi
* Zitto, Dk Slaa watishia kuachia ngazi
* Makani, Mtei waokoa jahazi
* Kamati Kuu yamwonya Wangwe
Na Muhibu Said
KINYANG'ANYIRO cha nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimezua mambo, baada ya Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa na Naibu wake, Zitto Kabwe kutangaza kujiuzulu nyadhifa zao.
Hata hivyo, viongozi hao walibadilisha uamuzi wao baada ya kuombwa na wajumbe wa Kamati Kuu iliyofanya kikao chake jana, jijini Dar es Salaam.
Dk Slaa na Zitto wanadaiwa kuchukua hatua ya kujiuzulu baada ya kuchukizwa na kitendo cha mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo Chacha Wangwe, ambaye ni Mbunge wa Tarime (Chadema) kukishutumu chama hicho kupitia vipeperushi vilivyosambazwa nchi nzima akidai kwamba kimegeuzwa kuwa mali ya ukoo wa baadhi ya viongozi wa makao makuu.
Vipeperushi hivyo ambavyo Mwananchi ina nakala zake, vilisambazwa na wafuasi wa chama hicho wanaomuunga mkono Wangwe katika kinyang'anyiro hicho.
Habari kutoka ndani ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho, kilichofanyika katika Hoteli ya Land Mark, jijini Dar es Salaam jana, zinaeleza kuwa Dk Slaa ambaye ni Mbunge wa Karatu na Zitto Kigoma Kigoma Kaskazini, walifikia uamuzi huo baada ya hoja kuhusu vipeperushi hivyo kujadiliwa katika kikao hicho.
Kutokana na kitendo hicho cha Wangwe, Kamati Kuu imemuonya na kutishia kufuta uchaguzi huo. Hata hivyo, baadaye Kamati Kuu iliridhia kuwa uchaguzi ufanyike baada ya wajumbe wa kamati hiyo kupiga kura, ambapo 14 walisema ufanyike na kumi na moja walisema usifanyike.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, Erasto Tumbo, aliliambia Mwananchi jana kuwa, kikao hicho kilifanyika jana chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kuandaa agenda zitakazojadiliwa katika kikao cha Baraza Kuu la chama hicho leo.
Kati ya agenda hizo ni pamoja na baraza hilo kumchagua mwanachama atakayejaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti iliyoachwa wazi na Amani Walid Kabourou aliyejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka jana.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa waasisi wa chama hicho, Edwin Mtei na Bob Makani walifanya kazi ya ziada kuwashawishi Dk Slaa na Zitto, kubadili uamuzi wao wa kujiuzulu na kuendelea na nyadhifa zao.
"Ni kweli Zitto na Slaa walitangaza kujiuzulu nyadhifa zao kutokana na vipeperushi vya Wangwe lakini baada ya mambo kuwekwa sawa na waasisi hao wa chama walikubali kurejea kwenye nyadhifa zao," kilisema chanzo chetu.
Wakati Mwananchi inakwenda mitamboni, vyanzo vyetu kutoka katika kikao cha Kamati Kuu, vilisema kwamba Zitto na Slaa walibadilisha uamuzi wao huo baada ya Mtei na Makani kuwataka kufanya hivyo ili kulinda chama kisigawanyike.
Pia chanzo hicho cha habari kimesema kwamba Wangwe amepewa karipio kali kutokana na kusambaza vipeperushi vya kutuhumu viongozi.
"Wameamua kurudia viti vyao, uchaguzi upo, lakini Wangwe amepewa karipio kali kwa kusambaza vipeperushi ambavyo wajumbe wameona kama vina lengo la kukigawa chama," kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, pamoja na kuonywa, imeelezwa kwamba Wangwe ameendelea kushikilia msimamo ulioko kwenye vipeperushi vyake.
Vipeperushi hivyo vinawatuhumu baadhi ya viongozi wa Chadema kuendesha chama kwa upendeleo, hasa katika mgao wa ruzuku na ubaguzi wa misingi ya kidini na kikanda.
Akizungumza na mwandishi wa Mwananchi muda mfupi kabla ya kuingia kwenye kikao hicho jana, Wangwe alisema kutokana na kasoro hizo, atahakikisha analeta mabadiliko ya kweli ndani ya chama ili kukiepusha kuendeshwa kama Shirika lisilo la kiserikali (NGO).
"Tunataka kiwe chama cha siasa chenye lengo la kuking'oa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010," alisema Wangwe.
Alisema jambo kubwa linalokitia dosari chama ni ofisi za wilaya na kata kutokuwa na mawasiliano na makao makuu, hasa katika mgao wa ruzuku na uteuzi wa wabunge wa viti maalum.
Wangwe alidai mgao wa ruzuku pamoja na uteuzi wa wabunge wa viti maalum, vimekuwa vikitolewa na uongozi wa Chadema kwa kuangalia upande mmoja wa wanachama wanaotoka katika Kanda ya Kaskazini nchini.
"Chama kimekuwa mali ya koo na familia fulani. Tunataka kiwe cha wanachama," alisema Wangwe ambaye anawania nafasi hiyo na Mbunge wa Mpanda Kati (Chadema), Said Arfi.
Wakati Wangwe akisema hayo, wafuasi wa chama hicho wanaomuunga mbunge huyo (Wangwe) katika kinyang'anyiro hicho, jana walisambaza vipeperushi vinavyotuhumu kuwapo na upendeleo katika mgao wa ruzuku za chama na ubaguzi wa kidini na kikanda katika chama hicho.
Vipeperushi hivyo vilivyotawanywa Makao Makuu ya Chadema, mikoani na katika eneo ambalo Kamati Kuu ilikutana jana, vinadai kwamba chama hicho kimekuwa kikipata ruzuku ya Sh60 milioni kila mwezi, lakini fedha hizo zimekuwa zikiishia makao makuu matumizi yake hayawekwi bayana.
"Tunasema inawezekana kila mkoa ukapata Sh1.5 milioni kila mwezi na Makao makuu itabaki na zaidi ya Sh10 milioni ambazo zinawatosha kwa shughuli za chama," ilieleza sehemu ya kipeperushi hicho.
Kipeperushi hicho ambacho Mwananchi inayo nakala yake, pia kimedai kuwapo kwa "ubinafsi" katika chama ambao umesababisha karibu wabunge wote wa viti maalum kuteuliwa kutoka katika mkoa mmoja ulioko eneo la Kaskazini mwa nchi.
"Wabunge viti maalum karibu wote wanatoka upande mmoja na kutoa ruzuku ya chama kwa upande mmoja (Kaskazini) haya yote yanatukera," kilieleza kipeperushi hicho na kuwataka wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho kumchagua Wangwe ili kukinusuru chama na mambo hayo.
Wabunge hao ambao wote wanatoka katika Mkoa wa Kilimanjaro, ni Halima Mdee, Grace Kihwelu, Maulida Komu na Lucy Owenya.
"Tumchague Chacha ili aweze kubeba majukumu hayo na kuyavalia njuga ili ruzuku igawanywe katika mikoa yote. Chacha pambana kama unavyopambana na CCM katika Jimbo lako la Tarime," kilieleza kipeperushi hicho.
Kipeperushi hicho kiliwataka wajumbe wa Kamati Kuu na Baraza Kuu kutoingia kwenye mtego wa kidini kwa madai kwamba, chama hicho sio msikiti wala kanisa.
"Ni chama cha siasa kinachotaka kuendelezwa na kiongozi jasiri kama Chacha (Wangwe). Hatusemi kwa ushabiki, angalia ukweli hapo makao makuu. Chadema ni chama chetu sio kampuni ya watu binafsi, tubadilishe hali hii," kilieleza kipeperushi hicho.
Katika kipindi cha mwezi mmoja, Wangwe amekuwa akiibua hoja ambazo zimezua mjadala mkubwa ndani ya chama hicho. Hoja ya hivi karibuni ni ile aliyodai kuwa Zitto hakupaswa kuingia katika Kamati ya kupitia upya mikataba ya madini.
Copied from
http://majira.co.tz/kurasa.php?soma=tanzania&habariNamba=4950